Mke, wanawe watoweka kipigo chatajwa chanzo

Dar es Salaam. Mama na wanawe wawili wamekimbia katika nyumba waliyokuwa wakiishi na mumewe, Yangeyange Kata ya Msongola wilayani Ilala, jijini Dar es Salaam.

Ni mama anayefahamika kwa jina la Faraja Ng’andu (32) na mke wa John Mtulya, ambaye ugomvi, kipigo na kufungiwa ndani na mumewe ilikuwa sehemu ya maisha kabla ya kutoweka kwake.

Juhudi za kutoa taarifa ya kutoweka kwake, zilianzia katika Kituo cha Polisi Msongola na baadaye Sitakishari, lakini imefika siku ya nne haijajulikani ni wapi Faraja wala wanawe walipo.

Mume ndiye alikuwa wa kwanza kutoa taarifa kwa wakwe zake na kwa mujibu wa baba mzazi wa Faraja, Samweli Ng’andu ndiye aliyemshauri Mtulya kuripoti Polisi Msongola.

Katika mazungumzo yake na Mwananchi jana Jumapili, Machi 16, 2025, baba yake Faraja amesema taarifa za kutoweka kwa mwanawe alizipata kwa mkwewe (mume wa Faraja) na alimshauri akaripoti polisi.

“Baada ya kunieleza mkewe hayupo nyumbani na ameondoka na watoto na simu yake haipatikani nilimwambia aende polisi lakini alipofika aliambiwa asubiri saa 24 ndipo arudi kutoa taarifa,” amesema Ng’andu.

Baada ya mume kutekeleza hilo na kupewa RB iliyotolewa Machi 13, Ng’andu amesema naye alikwenda kuripoti katika Kituo cha Polisi Sitakishari, kuweka msisitizo wa taarifa zaidi.

Mzazi huyo amesema alikaa kusubiri mrejesho wa taarifa kutoka kwa mkwewe, lakini hakupata ndipo Machi 14, 2025 alipoamua kwenda Polisi Msongola kufuatilia.

“Nilipofika kituoni hapo nilimkuta mume wa mwanangu, mama mkwe wake na watu wawili wakiwa kama mashahidi akiwepo mjumbe wakichukuliwa maelezo na ndipo baba yule alishangaa na kuuliza kwanini sikutoa taarifa ya ujio wangu,” amesema.

Kwa mujibu wa Ng’andu, hakuna aliyetarajia kama angefika kituoni hapo kwa kuwa hakutoa taarifa kabla. Lakini alipokelewa na kuchukuliwa maelezo.

Akiwa kituoni hapo, amesema askari aliyekuwa akichukua maelezo aliwaambia jalada linatakiwa kwenda kwa OCD (Kamanda wa Polisi wa Wilaya) siku hiyo kwa kuwa siku zimepita na kupotea kwa watu wa tatu si jambo la kawaida.

“Aliponihakikishia kuwa jalada litafika kwa OCD siku ambayo amechukua maelezo hivyo niliamua kumpigia simu jana (Jumamosi) ili kujua maendeleo lakini alinijibu bado hajalipeleka na kudai bosi huyo alikuwa na kikao na akimaliza angempatia,” amesema Ng’andu.

Hata hivyo, amesema amekuwa akifuatilia kwa polisi kwa kupiga simu lakini hazipokelewi na kuna wakati hazipatikani, jambo linalomuongezea mashaka.

Mwananchi limemtafuta mume wa Faraja kwa simu yake ya mkononi bila mafanikio na juhudi za kumtafuta zinaendelea.

Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Yustino Mgonja simu yake iliita bila kupokewa, kama ilivyokuwa kwa Kamanda Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro. Mananchi limefika hadi ofisini kwa Muliro na kuelezwa hayupo.

Historia ya maisha ya Faraja na mumewe Mtulya kwa mujibu wa Ng’andu imegubikwa na ugomvi na vipigo, matukio ambayo aghalabu yalimkabili mwanawe.

Katika simulizi yake hiyo, baba huyo amesema ipo siku amewahi kumtembelea mwanawe akakuta anapigwa na mumewe na mkwewe (mama wa Mtulya).

“Kiukweli nilijiuliza ni maisha gani haya na hii ilitokana na mumewe alikuwa anaishi kwa mama yake mzazi hivyo siku ambayo tumekwenda niliumia sana na nikamwambia hiki nini na nikaondoka na binti yangu,” amesema.

Pamoja na juhudi hizo, amesema nguvu ya mapenzi ilimshinda Faraja na baadaye mumewe alipomfuata alirudi wakaendelea kuishi.

Tangu mwanawe huyo alipochukuliwa na mumewe, Ng’andu amesema hakuwahi kumwona hadi Septemba 2024, baada ya kupigwa na kuvunjiwa simu.

Amesema mwanaye aliwahi kumwambia mumewe amemzuia kuwasiliana na wazazi, ndiyo sababu hawakuwa wakiwasiliana na kupotezana.

“Nasema kuwa alikuwa kama mfungwa kwa maana ya ule uhuru haupo na hiyo ilikuwa inamtia wasiwasi na uoga yaani maisha yake hayakuwa ya furaha,” amesema.

Mwanawe huyo amesema ana watoto wawili wa kiume (4) na wakike (3) na kwa mara ya kwanza amewaona mwaka jana.

Mjumbe wa Mtaa wa Mtumishi yaliko makazi ya Faraja na mumewe, Joseph Mwita amesema kuna siku Faraja alisikika akipiga kelele akidai anauawa, watu walikusanyika na kukuta anapigwa, ilibidi wampigie Ng’andu.

Kikao kilifanyika kusuluhisha ugomvi na binti alitaka kurudi nyumbani kwao, akidai amemchoka mumewe.

Ukiachana na kisa hicho, Mwita amesema hivi karibuni alipokea ujumbe mfupi akiambiwa mwanamke huyo anataka kuuawa, alilazimika kumwagiza mjumbe msaidizi kufuatilia.

Amesema mjumbe msaidizi alikuta ugomvi uliokuwepo ulihusu mume kumtuhumu mkewe kuwa na ujauzito asiohusika nao, kwa kuwa alikuwa safarini kitambo na aliporudi alikuta Faraja ametuma picha za utupu kwa mwanaume mwingine.

“Juzi mumewe akiwa kazini mwanamke aliondoka akiwa ameacha milango na madirisha wazi, simu kaacha nyumbani na hakuondoka na viatu kwani kila kitu chake aliacha hapo huku nguo na sehemu nyingine zikiwa zimepekuliwa,” amesema.

Related Posts