Mkazi wa Yangeyange wilayani Ilala, Dar es Salaam, Faraja Ng’andu na wanawe wawili wametoweka kwenye nyumba waliyokuwa wakiishi na hawajulikani walipo.
Ni zaidi ya siku tano sasa tangu Faraja na wanawe hao wa kiume na wa kike huku jitihada za familia kuwatafuta kwa kulihusisha Jeshi la Polisi zikiendelea.
Faraja (28), alitoweka nyumbani hapo Jumamosi, Machi 12, 2025 na tayari taarifa za kutoweka kwake zimeripotiwa kwenye Kituo cha Polisi Msongola na Kituo cha Polisi Sitakishari.
Awali, ilielezwa kuwa mume wa Faraja, John Mtulia ndiye alitoa taarifa za kupotea kwa mkewe kwa wakwe zake (Familia ya Faraja) ambao, walimshauri kwenda kuripoti Kituo cha Polisi Msongola kwa hatua zaidi.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Faustine Mafwele amesema uchunguzi wa awali unaonyesha Faraja aliondoka nyumbani Machi 12,2025 huu saa 5:00 asubuhi kutokana na mgogoro wa ndoa yake na Mtulia.
Jana Jumapili, Machi 16, 2025, Mwananchi limezungumza na baba wa Faraja, Samwel Ng’andu aliyedai kuwa taarifa za kutoweka kwa binti yake na wajukuu zake wawili, alizipata kutoka kwa mkwewe (Mtulia) na alimshauri akaripoti polisi.
“Baada ya kunieleza mkewe hayupo nyumbani na ameondoka na watoto na simu yake haipatikani, nilimshauri kwenda kutoa taarifa polisi. Alipofika huko aliambiwa asubiri hadi saa 24 zipite ndipo arudi kutoa taarifa,” amesema Ng’andu.
Mtulya alitekeleza hilo na kupewa RB iliyotolewa Machi 13, 2025 huku Ng’andu naye akienda kutoa taarifa Kituo cha Polisi Sitakishari.
Baba mzazi huyo amedai kuwa alikaa kusubiri mrejesho kutoka kwa mkwewe, lakini hakupata ndipo Machi 14, 2025 alipoamua kwenda Polisi Msongola kufuatilia.
“Nilipofika kituoni nilimkuta Mtulia na watu wawili pamoja na mjumbe wakichukuliwa maelezo na waliponiona walipigwa butwaa kwa sababu nadhani hawakutarajia kuniona,” amedai Ng’andu.
Akiwa kituoni hapo, amesema askari aliyekuwa akichukua maelezo aliwaambia jalada linatakiwa kwenda kwa OCD (Kamanda wa Polisi wa Wilaya) kwa tukio la kupotea kwa watu watatu si jambo la kuchukuliwa kawaida.
“Aliponihakikishia kuwa jalada litafika kwa OCD siku ambayo amechukua maelezo, niliamua kumpigia simu jana (Jumamosi-Machi 15,2025) ili kujua maendeleo, lakini alinijibu bado hajapelekwa kwa kuwa alikuwa na kikao,” amedai Ng’andu.
Jitihada za kumpata Mtulia kuzungumzia kuhusu kutoweka kwa mkewe na wanawe, hazijafanikiwa.
Kwa mujibu wa Kamanda Mafwele amesema kuwa wanandoa hao wametofautiana kwa muda mrefu na kwamba, Faraja amewahi kuondoka nyumbani na kwenda kwa wazazi wake hadi Machi 2, 2025 aliporejea baada ya kusuluhishwa.
“Katika mahojiano na polisi, Mtulia alieleza kuwa walihitilifiana na mke kwa muda mrefu na kusababisha kuondoka kwenda kwa wazazi wake wanaoishi Kipunguni B. Machi 2, 2025 mkewe alirejea nyumbani baada ya kwenda kumuomba msamaha,” amesema Kamanda Mafwele.
Pia, amesema kuwa Faraja alimweleza mumewe kuwa ana ujauzito ambao ni wa mwanaume mwingine aitwaye Maliki hivyo, hawezi kuendelea kuishi kwake tena.
Kamanda Mafwele amesema kuwa Machi 12, 2025 Faraja aliondoka nyumbani kwa Mtulia kwa kutumia bodaboda na kushushwa maeneo ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
“Baada ya kufikishwa hapo na bodaboda aitwaye Pondamali, Faraja alikodi bajaji ambayo iliyompeleka kusikojulikana. Kwa sasa uchunguzi wa mahali alipo Faraja na Maliki anaendelea,” amesema Mafwele.
Tuhuma za ugomvi ndani ya nyumba
Kumekuwepo na taarifa mbalimbali kuhusu maisha ya Faraja na Mtulia, ambapo kwa mujibu wa Ng’andu wawili hao wamekuwa na ugomvi wa mara kwa mara.
Baba huyo anadai kuwa kuna wakati aliwahi kwenda kumtembelea Faraja nyumbani na alipofika akawakuta wanapigana na mumewe.
“Kiukweli nilijiuliza ni maisha gani haya, ni tukio ambalo liliniumiza na siku hiyo niliamua kuondoka nab inti yangu,” amedai Ng’andu.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Mtaa wa Mtumishi yaliko makazi ya Faraja na Mtulia, Joseph Mwita amedai kuna siku Faraja alisikika akipiga kelele ya kuomba msaada.
Amedai kuwa siku hiyo walifika nyumbani kwa wawili hao na kuwakalisha kikao kusuluhisha ugomvi huo na baadaye maisha yakaendelea.
“Kuna matatizo ndani ya ndoa yao, ugomvi huko nyuma. Juzi mwanamke ameondoka nyumbani na watoto wake,” amedai Mwita.