Moto wateketeza vibanda 30 vya wafanyabiashara wa mbao Mwanza

Mwanza.  Moto ambao bado chanzo chake hakijafahamika umeunguza vibanda vya wafanyabiashara zaidi ya 30 wa mbao katika soko la mbao Sabasaba Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.

Akithibitisha kutokea tukio hilo leo Jumatatu Machi 17, 2025, Kaimu Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza, Elisa Kamugisha amesema moto huo ulianza saa saba usiku na hata hivyo walifanikiwa kuwahi kuuzima usienee sehemu nyingine.

Amesema soko hilo linakadiriwa kuwa na wafanyabiashara zaidi ya 1,000 lakini walioathirika na moto huo ni wafanyabiashara takribani 30.

“Tulipokea taarifa na kufika hapa ndani dakika tisa baada ya kupokea taaira, lakini tulikuta moto ni mkubwa sana lakini tumeweza kuudhibiti ili usisambae.

“Hapa ni biashara ya mbao na sehemu kubwa iliyoathirika ni yenye magogo, mbao pamoja na mashine, lakini tumeweza kupambana. Kwa ujumla waathirika wakubwa ni kama 12 na wengine wadogowadogo jumla wanafika kama 30 japo soko hili lina watu kama 1,000,” amesema Kamugisha.

Akizungumzia moto ulivyoanza, mfanyabiashara wa mbao eneo hilo, Idrisa Kinunga amesema amepigiwa simu na watu saa 10 alfajiri akiambiwa ofisi yake inaungua moto, hata hivyo alikuta bidhaa zake zote zimeteketea na moto akidai zikiwa na thamani kati ya Sh40 milioni hadi Sh50 milioni.

 “Hasara niliyoipata ni kubwa, siyo kidogo ni fedha isiyopungua Sh40 milioni au Sh50 milioni…Hakuna nilichookoa chochote,” amesema.

Mwenyekiti wa soko hilo, Amon Sobuki amesema alipata taarifa ya tukio hilo saa nae usiku kisha kuchukua hatua ya kupiga simu zimamoto.

“Tumeshirikiana vizuri sana na zimamoto mpaka tukafanikiwa kuudhibiti saa 11 alfajiri,” amesema.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda ametaka uchunguzi ufanyike ili kujua chanzo cha moto huo huku akiwatka waathirika kuwa watulivu wakati uchunguzi ukiendelea.

Akizungumza nao mara baada ya kutembelea maeneo yaliyoathirika na moto huo, Mtanda amesema mara baada ya taarifa ya uchunguzi kukamilika, ofisi yake itakutana na wafanyabiashara hao pamoja na taasisi za fedha ili kuona namna ya kuwapa muda zaidi wa marejesho ya fedha kwa wale waliokopa.

“Natoa rai kwa vyombo vya dola kuharakisha uchunguzi huu ili kutambua chanzo na kujua nini kifanyike na wafanyabiashara hao waendelee na shughuli zao mapema iwezekanavyo kama Serikali inavyohimiza wananchi kuwajibika,” amesema Mtanda.

Aidha, amewataka wafanyabiashara hao kuzingatia matumizi ya vifaa vya kuzimia motopamoja na bima ambayo itawasaidia kuepuka hasara kubwa yanapotokea majanga ya moto.

“Serikali kuna maeneo ya majanga inawajibika moja kwa moja kuwagharamia wananchi na mengine haiwajibiki nayo kama hili, narudia kuwakumbusha kuzingatia sheria zinavyotaka ili kujihakikishia usalama wa muda wote wa mali zenu,

“Niwapongeze pia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kufanya kazi hii kwa weledi na kuokoa sehemu kubwa ya mali za wafanyabiashara hawa,” amesema Mtanda.

Related Posts