Muya atuliza presha Geita Gold

LICHA ya Geita Gold kupoteza michezo mitatu mfululizo, ila kocha mkuu wa timu hiyo, Mohamed Muya amesema matokeo hayo hayajawatoa mchezoni, ingawa ni changamoto anayokabiliana nayo ya kukitengeneza kikosi hicho kuongeza ushindani zaidi.

Kauli ya kocha huyo inakuja baada ya kuchapwa mabao 5-0 na Mtibwa Sugar, akachapwa tena bao 1-0 na maafande wa Polisi Tanzania, kisha akatandikwa 1-0 na Mashujaa kwenye Kombe la Shirikisho (FA) hatua ya 32 bora na kuaga mashindano.

“Ni upepo mbaya ambao umetukuta kwa siku za hivi karibuni lakini bado hatujatoka kwenye malengo tuliyojiwekea, ushindani ni mkubwa sana hasa hii ya michezo ya mwishoni, hivyo kwetu tumeichukulia kama changamoto mpya ya kuzidi kutuimarisha.”

Timu hiyo iliyoshuka daraja msimu uliopita, inashuka kwenye uwanja wake wa Nyankumbu, mkoani Geita leo kuikaribisha Mbeya Kwanza, huku ikiwa nafasi ya nne na pointi zake 45, baada ya kushinda michezo yake 14, sare mitatu na kupoteza mitano.

Muya amejiunga na Geita baada ya kutimuliwa Fountain Gate kufuatia kuchapwa mabao 5-0, dhidi ya Yanga Desemba 29, mwaka jana, akienda kukifundisha kikosi hicho kwa kuchukua nafasi ya Amani Josiah aliyejiunga na maafande wa Tanzania Prisons.

Related Posts