Namna ya kuishi na mabosi wanaofoka

Dar es Salaam. Kama una ‘bosi’ au kiongozi katika eneo la kazi ambaye kuzungumza kwake ni kufoka, basi huenda unajua jinsi hali hii inavyoweza kukera na kuleta mashaka kwenye ufanisi wako wa kazi.

Hali hii ni ngumu na mara nyingi hutufanya tujiulize,”Kwa nini bosi wangu anafanya hivi?” Ingawa inapotokea, inaweza kuwa vigumu kujibu moja kwa moja, lakini wataalamu wa saikolojia na akili wanasema.

Kiongozi mwenye hulka ya kufoka au kutawala kwa hasira anaonyesha dalili za kutoshinda changamoto za mihemko.

James Christopher mwajiriwa jijini Dar es Salam amesema ukali wa viongozi ofisi huathiri utendaji wa mfanyakazi.

“Yapo mambo ambayo wafanyakazi huhitaji kuongea na viongozi wao lakini kama bosi anakuwa ni mtu wa kufoka kila siku lazima wafanyakazi muogope hata kuzungumza naye kila mtu anatulia na lake,” amesema.

Amesema viongozi maeneo ya kazi kufokea wafanyakazi wakati kutokana na kazi kutofanyika kama inavyohitajika na wakati mwingine ni tabia ya kiongozi husika kufoka.

 “Hali hii inaweza kuwa ni matokeo ya msongo wa mawazo au hali ngumu anayopitia, anaweza kuhamishia hasira na msongo wake kwa watu aliowekwa kuwaongoza,” Mtaalamu afya na Magonjwa ya akili Dk Raymond Mgeni wa Hospitali ya Rufani kanda ya Mbeya.

Mtaalamu huyo ameyasema hayo leo Jumatatu Machi 17, 2025 akizungumza na Mwananchi.

Dk Mgeni amesema mtu anapokuwa na changamoto za haiba hubadilika na kuwa mtu wa kukaripia.

Ameongeza watu wengine wenye tabia hiyo huonyesha hali hiyo akiwa na taarifa nyingi ambazo zinamkanganya.

Sababu nyingine na kiongozi kufoka kwa kila jambo eneo la kazi ni malezi aliyoyapata ambayo Dk Mgeni amesema kwa kiwango kikubwa mhusika amewashuhudia wazazi wake wakikaripiana mara kwa mara hivyo kuchukua tabia hiyo na kuishi nayo.

“Ili kuishi na mtu wa namna hii lazima umuelewe ana tabia gani na uepuke kufanya mambo ambayo ukigusa anaanza kukaripia, mfano kama hapendi kucheleweshewa kazi muwaishie,” amesema.

Dk Mgeni amesema kama kiongozi eneo la kazi anakuwa mkali sana huathiri utendaji wa wafanyakazi wa chini na kusababisha ufanisi mdogo wa taasisi.

Mtaalamu wa saikolojia Ramadhani Masenga amesema ili kuishi na watu wenye haiba hiyo kwanza wafanyakazi watambue viongozi wao hawana ugomvi binafsi na wao.

“Unapaswa kutambua kuwa kuwa huyu ananijibu majibu mabaya au makali kwasababu hayupo sawa, unatakiwa kumkubali alivyo na uende naye kama mgonjwa kwasababu huenda ana matatizo nyumbani kwake au anapata shinikizo la kazi kutoka kwa wakubwa zake,” amesema Masenga.

Masenga ameongeza kuwa sababu nyingine ya watu wa namna hiyo kuendelea kufoka ni kutaka sababu ya jambo fulani kutofanyika na huhitaji kuombwa msamaha.

“Baada ya kumaliza kufoka unaweza kumfuata na kuzungumza naye tena na ukampa sababu ya tukio lililotokea na ni kosa kubwa mtu huyo anapofoka nawe mkaendelea kujadiliana naye ataongeza hasira zaidi na kukupa adhabu kali zaidi,”amesema.

Mbali na hayo Masenga amesema kwa kawaida watu wenye hali hiyo wanashida ya kutojiamini na anapofanya hayo hutaka kuonyesha ukubwa wake.

Masenga amesema ni muhimu kiongozi ndani ya ofisi akafahamu mfanyakazi anapokuwa amekosea aonyeshe staha kwa namna unavyoshughulika makosa.

“Lazima ajifunze kudhibiti hasira hata pale unapokuwa na sababu ya kuhalalisha kuudhika mbele ya kadamnasi,” amesema.

Related Posts