‘No Reform, No Election’ yawapeleka Chadema kwa Msajili

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeweka wazi kuhusu kupokea wito wa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Chadema, kikao na Jaji Mutungi kitafanyika kesho Jumanne, Machi 18, 2025 huku ajenda kuu ikiwa ni ‘No Reform, No Election.’

Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Jaji Mutungi amethibitisha bila kufafanua kwa kina sababu ya wito wake.

Chadema ilitangaza kampeni ya No, Reform No Election (bila mabadiliko, hapa uchaguzi) ikilenga kushinikiza mabadiliko ya kisheria kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka huu.

Kwa mujibu wa msimamo wa chama hicho, pasi na mabadiliko hayo kufanyika chama hicho kitaushinikiza umma kuzuia uchaguzi usifanyike.

Kaulimbiu hiyo iliwahi kujibiwa na viongozi mbalimbali wa CCM, wakisema mabadiliko yameshafanyika na uchaguzi utafanyika.

Mbali na CCM, Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi aliwahi kujibu hilo, akisema kama kuna nia njema ya mabadiliko, ofisi za wizara hiyo ziko wazi kwa yeyote kwenda kujadiliana.

Alisema kwa kuwa Serikali inaongozwa kwa kuamini katika maridhiano, wanamkaribisha yeyote kwenda kuridhiana naye kuhusu mabadiliko.

Hata hivyo, alisisitiza Chadema pekee haiwezi kuzuia uchaguzi kwa kuwa mchakato huo unawahusisha wananchi na chama zaidi ya kimoja.

Taarifa ya Chadema, imetolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi, Brenda Rupia leo Jumatatu, Machi 17, 2025.

Brenda katika taarifa hiyo, amesema kesho chama hicho kitakwenda katika ofisi ya Msajili jijini Dar es Salaam kuitikia wito.

Amesema:“Ajenda kuu ya wito huo ikiwa “No Reforms, No Election.”

Amesema Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika ataongoza ujumbe wa kwenda kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, kisha taarifa ya mrejesho wa kitakachojili itatolewa.

Related Posts