OCD afariki ajalini, askari mwingine avunjika mkono

Dar es Salaam. Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linamtafuta dereva wa daladala aliyesababisha ajali ya barabarani ambayo imekatisha maisha ya Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kipolisi Chanika (OCD), Awadh Chico na kumjeruhi askari, Zubeda Sadala.

Ajali hiyo imetokea saa 1:20 asubuhi ya leo Jumatatu, Machi 17, 2025 katika barabara ya Nyerere maeneo ya Pugu Mwisho wa Lami jijini Dar es Salaam ikihusisha gari aina ya Tata inayofanya safari zake kati Zingiziwa Chanika na Machinga Complez Ilala ikitokea Pugu kwenda Gongo la Mboto iligongana na gari ndogo aina ya Toyota Prado.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Faustine Mafwele amesema ajali hiyo imetokea baada ya dereva wa daladala kuyapita magari yaliyokua mbele yake bila kuchukua tahadhari na kusababisha kungongana uso kwa uso.

“Jeshi la Polisi linamtafuta dereva wa daladala ambaye hajafahamika aliyetoroka baada ya kusababisha ajali hiyo na linakanusha taarifa zilizotolewa kuwa aliyefariki ni Kamishina wa Operasheni na Mafunzo Tanzania, CP Awadhi Juma Haji,” amesema Mafwele.

Amesema mkuu huyo wa Polisi wilaya ya kipolisi Chanika alitokea Gongo la Mboto kuelekea Pugu baada ya ajali alifariki dunia na majeruhi ambaye alikuwa abiria amevunjika mkono wa kushoto.

Hata hivyo, amewataka waendeshaji wa vyombo vya moto kuzingatia alama zilizowekwa barabara kwa kipindi hiki cha matengenezo yanayoendelea ili kuepuka ajali zinazosababishwa na uzembe kwa madereva.

Related Posts