Unguja. Wakati Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ikihitimisha shughuli ya uandikishaji wapigakura wapya awamu ya pili, Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud Othman ni miongoni mwa wapigakura waliojitokeza siku ya mwisho huku akisema uandikishaji umeenda vyema.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Machi 17, 2025 baada ya kumaliza kujiandikisha katika Kituo cha Mpigakura cha Sekondari ya Mpendae Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi, Othman ambaye pia, ni Mwenyekiti wa Chama cha ACT- Wazalendo Taifa, amesema hatua ya watu kujitokeza kwa wingi ni ishara kazi imefanyika vizuri.
“Ninaamini kazi imekwenda vizuri na ndio maana unaona wamejitokeza kwa wingi kujiandikisha,” amesema Othman ambaye ameshatangaza nia ya kugombea urais wa Zanzibar kupitia chama chake iwapo kikimteua kuwania nafasi hiyo.
Othman amesema hakuwa kwenye daftari la mpigakura kwa kuwa, wakati watu wanaandikishwa mwaka 2020 alikuwa kwenye majukumu mengine nje ya nchi kwa hiyo hakupata nafasi ya kujiandikisha.
“Kwa hiyo wakati ule (daftari) linafanyiwa marekebisho sikuwapo nilikuwa nje ya nchi, kwa hiyo nilidhani tu kinachohitajika pengine ku-update taarifa zangu kwenye kitambulisho, lakini nilipouliza nikaambiwa kiutaratatibu natakiwa nijiandikishe upya maana kila baada ya miaka 15 unajiandikisha,” amesema.

Ofisa mwandikishaji wapiga kura, Aisha Rajabu Omar akimchukua alama za vidole Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud alipojiandikisha katika awamu ya pili ya uandikishaji wapiga kura wapya kituo cha Sekondari ya Mpendae Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi leo Machi 17, 2025. Picha na Jesse Mikofu
Kuhusu kujiandikisha eneo tofauti na makazi yake ya Chukwani anapoishi sasa, Othmana amesema kwa mujibu wa sheria inamtaka mtu ajiandikishe eneo ambalo amekaa miaka mitatu, lakini kwa makazi aliyopo hivi sasa bado hajafikisha muda huo.
“Suala la ukaazi ni la kisheria nilipohama Mpendae nikaenda Maisara kisha Chukwani, lakini kote nilipohamia sijatimiza miaka mitatu kuwa mpigakura kwa hiyo sheria inanitaka hapa Mpendae ndio nijiandikishe maana nilikaa zaidi ya miaka mitatu,” amesema.
Alipoulizwa kuhusu huenda angekosa fursa hiyo ya kujiandikisha iwapo asingezuiwa kuingia Angola, Othman amesema walikuwa wanajua namna ya kufanya.
“Hili la Angola sisi wenyewe tulikuwa tunajua utaratibu wetu wa kurudi kujiandikisha kupiga kura,” amesema.
Othman alizuiwa kuingia nchini Angola Machi 13, 2025 hivyo kwa ratiba ya mkutano huo uliotakiwa kufanyika nchini humo, alitakiwa kurejea nchini Machi 18, 2025.
Mkurugenzi wa Uchaguzi ZEC, Thabit Idarous Faina amesema Othman ameandikwa kama mpigakura mpya na sheria inamruhusu kujiandikisha katika eneo hilo kwa kuwa, katika maeneo mengine alikuwa hajafikisha miaka mitatu.
“Kwa kazi hii tunayofanya ni mpiga kura mpya, tumeboresha mwaka 2023 na mwaka huu ndio tunamalizia ambao hawakujiandikisha, kwa hiyo kama kutakuwa kuna mtu anadhani hana sifa anaweka pingamizi kwa mujibu wa sheria namba nne ya mwaka 2018,” amesema Faina.
Naye Mwenyekiti wa ZEC, Jaji George Joseph Kazi amesema uandikishaji umeenda vizuri katika vituo vyote na kubwa zaidi ni usalama na amani vimetawala katika vituo hivyo, licha ya changamoto ndogondogo ambazo hata hivyo hazikuleta madhara wala kuzuia kazi isiendelee.
Ametaja miongoni mwa changamoto ni taarifa za kutoonekana kwa baadhi ya wananchi kutokana na vitambulisho vyao kuwa vipya lakini tatizo hilo limetatuliwa.
Amesema walikadiria kuandikisha wapigakura 78, 922 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi mwaka 2022 lakini watu ambao tayari wameandikishwa makadirio yamevuka.
“Tumevuka lengo lakini hatuwezi kutoa takwimu kamili kwasababu mpaka tukamilishe kila kitu, kwa hiyo tutakaa na kuchakata taarifa na kuangalia kwa mujibu wa rika zao, labda waliokuwa na miaka 18 mpaka 35 ni wangapi, lakini kuanzia hapo hadi miaka 50 na kuendelea nao ni wangapi,” amesema Jaji Kazi.
Amesema baada ya kufanya tathmini watakaa na wadau vikiwamo vyama vya siasa kwa ajili ya kutoa tathmini yao.
Jaji Kazi amesema baada ya kumalizia hilo, watatoa orodha ili wale ambao wamejiandikisha waangalie taarifa zao kama zipo sahihi au zinahitaji kufanyiwa marekebisho na kama kuna watu wanadhani wameandikishwa lakini hawana sifa wawekewe pingamizi.