Polisi Dar yaahidi kumnasa anayedaiwa kumuua mkewe

Dar es Salaam. Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linamsaka kijana anayetuhumiwa kufanya mauaji ya Paulina Mathias (40), Mkazi wa Kibonde Maji B, Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam.

Tukio hilo linadaiwa kutokea Machi 10, 2025 eneo la Kibonde Maji alikokuwa amepanga mwanamke huyo.

Inadaiwa mwanamke huyo aliuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali tumboni baada ya kumnyima kijana huyo anayedaiwa kuwa mmewe Sh50,000 kulipia kodi ya pango

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Machi 17, 2025 Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Faustine Mafwele amesema jeshi hilo linamsaka kijana huyo.

“Hatuangalii walichogombana, tunaangalia kosa la jinai alilotenda kwa hiyo Jeshi la Polisi tunamsaka kokote alipo na hivi karibuni litamkamata,” amesema Mafwele, alipojibu swali la Mwananchi lililotaka kujua nini kinaendelea juu ya tukio hilo.

Taarifa zikidai mgogoro baina ya wawili hao ulianza tangu Februari mwaka huu.

Kwa mujibu wa mdogo wa marehemu, Happy Athuman alisema kabla ya mauaji kutokea mwanaume alimuomba mkewe Sh50,000 fedha zake za kikoba alipie kodi na alimpatia kwa sharti la kurejesha.

Baada ya muda, Happy amedai dada yake alimpatia Sh50,000 mwanamume huyo kwa ajili ya kulipa kodi lakini, alitoweka na fedha hizo na baada ya muda baba mwenye nyumba alifuata kodi yake.

Amesema kwa kuwa shemeji yake tayari alishapatiwa fedha hizo, Happy alisema Paulina alimpigia simu kumwambia tayari mwenye nyumba amefika akihitaji kulipwa deni lake.

Amedai, mwanamume huyo alirudi na Sh48,000 na kumrejeshea Paulina akimwambia aongeze ifike Sh50,000 ili itoshe kulipa kodi, lakini Paulina alihoji kwa nini fedha hiyo ni pungufu (wakati awali alimpa Sh50,000).

Inadaiwa tangu hapo kulianza kutokea mzozo wa pande hizo mbili hadi kusababisha mauti ya Paulina yanayodaiwa kutendwa na kijana huyo ambaye taarifa zinadai walitengana tangu Februari mwaka huu.

Related Posts