Njombe. Wakati uunganishwaji wa umeme katika maeneo ya vijiji ukiwa ni Sh27,000 na Sh320,960 mijini, Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wameagizwa kubandika gharama halisi za kuunganisha umeme katika ofisi za serikali za vijiji.
Gharama hizo ziende sambamba na hatua ambazo mwananchi anapaswa kuzifuata akitaka kuunganishishiwa umeme ili wananchi wazifahamu kwa ufasaha kabla ya kufanya maombi.
Maagizo hayo yametolewa leo Jumatatu Machi 17, 2025 na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mathayo David katika Kata ya Mang’oto wilayani Makete mkoani Njombe wakati wa ziara ya kukagua miradi ya usambazaji wa umeme.
Mathayo amesema ili kuondoa mkanganyiko kwa wananchi juu ya gharama halisi za kuunganisha umeme ni wakati sasa kwa Tanesco na Rea kubandika bei hizo katika Ofisi za Serikali za Vijiji husika pamoja na hatua za kufuata pindi mteja akitaka kuunganishiwa umeme.
“Wananchi wamekuwa wakizungumza tu kuhusu gharama za kuunganishiwa umeme, hakuna aliyekuwa na taarifa sahihi hasa vijijini, hii inawapa hofu wanapohitaji kuunganisha umeme na pia wanapata ugumu wa kufuata huduma ofisi za Tanesco, wekeni taarifa wazi watu wazijue itaondoa mkanganyiko,” amesema Mathayo.
Licha ya kuwapo kwa bei hizo elekezi lakini bado kumekuwa na mkanganyiko wa kiasi cha fedha kinachotozwa katika baadhi ya maeneo licha ya kuwa katika maeneo ya vijijini.
Katika kufafanua hilo, Januari 30, 2025, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga akiwa bungeni jijini Dodoma alisema licha ya kuwapo kwa bei hizo lakini si kila eneo zinatumika hususani za kijijini.
“Sio kila eneo linakidhi vigezo vya kuunganisha umeme kwa Sh27,000,” amesema.
Kapinga aliyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Kilombero, Abubakari Asenga aliyetaka kufahamu kwa nini maeneo ya Katinduka bado yanalipia umeme kwa Sh360,960 wakati ni maeneo ya vijiji, Kapinga amesema. maeneo ya vijiji yanaunganishwa kwa Sh27,000 kutokana na Serikali na wafadhili kutoa fedha za kutekeleza miradi ya umeme vijijini.
Majibu hayo pia yalijibu swali la la Mbunge wa Bukene, Selemani Zedi aliyetaka kufahamu kwa nini maeneo ya Bukene na Itobo hayaunganishiwi umeme kwa gharama ya Sh27,000.
Naibu Waziri Judith Kapinga ambaye pia alikuwa katika ziara hiyo ya Kamati ya Bunge aliitaka Rea na Tanesco kuongeza kasi ya kuwahamasisha wananchi kuungananisha umeme ikiwemo kusuka nyaya katika nyumba zao ili kuunganishiwa umeme hasa wakati miradi inapokuwa inatekelezwa katika maeneo husika.
“Hii itasaidia mradi unapokamilika wananchi wengi wawe wamepata huduma ya umeme,” amesema Kapinga.
Pia ametumia nafasi hiyo kuwataka kutumia simu ya kupitia namba 180 ili waweze kutatuliwa changamoto zao moja kwa moja na kwa haraka.
Ziara hiyo imeshirikisha viongozi wakuu kutoka Wizara ya Nishati, akiwemo Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, Khatib Kazungu, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Viongozi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara pamoja na Maafisa wengine.