Dar es Salaam. Zaidi ya nusu ya taka jijini Dar es Salaam hazikusanywi kutokana na changamoto kadhaa, miundombinu ikitajwa.
Kutokana na hali hiyo, Jiji la Dar es Salaam lenye wakazi milioni 5.3 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, kwa asilimia kubwa wananchi wanaishi katika mazingira yaliyozungukwa na takataka majumbani, hofu ikiwa juu ya usalama wa afya zao.
Hali hiyo inatokana na jiji hilo kuwa na uwezo wa kukusanya na kuzipeleka dampo chini ya nusu ya kiwango cha takataka zinazozalishwa kwa siku, ambazo ni zaidi ya tani 4,500.

Taka zikiwa zimeachwa barabarani eneo la Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam. Picha na Edwin Mjwahuzi
Utaratibu wa usafi wa mazingira
Kumekuwa na mifumo tofauti ya uzoaji taka katika halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam, baadhi zikitumia makandarasi na nyingine zikitumia vikundi vya kijamii kukusanya na kuzoa taka kuzipeleka dampo.
Hata hivyo, kumekuwa na tatizo la ufuatiliaji wa ratiba za uzoaji taka, hivyo nyingi kubaki mitaani.
Si hivyo tu, mfumo wa makusanyo ya ada ya taka na utaratibu wa malipo ya makandarasi na watoa huduma ya taka, yakiwamo magari ya kukodi kupeleka taka dampo, umekuwa na changamoto.
Baadhi ya wananchi wamekuwa wakilipa Sh3,000 kwa mwezi lakini taka hazizolewi, huku makandarasi wakizidai halmashauri fedha kwa kazi walizofanya.
Katika ripoti maalumu iliyofanywa Februari 2023 na tovuti ya Down to Earth ya India inayojihusisha na masuala ya mazingira, inaeleza kuwa uzalishaji wa taka jijini Dar es Salaam umeongezeka mara tatu katika kipindi cha miaka 16 iliyopita. Jiji linazalisha karibu tani 4,500 za taka ngumu kwa siku, lakini ni asilimia 50 hadi 70 tu ndio zinazokusanywa.
Tafiti hiyo ilieleza kuwa taka zote zinazokusanywa hatimaye huishia kwenye dampo la Pugu lililoko kilomita 35 kutoka katikati mwa jiji.
“Ratiba za huduma za ukusanyaji katika jiji si za kawaida na zisizofaa kutokana na idadi isiyotosheleza ya magari ya kukusanya, misongamano ya magari na miundombinu isiyopangwa vizuri,” inaeleza ripoti ya Down to Earth inayohusika na ufanisi katika usafi wa mazingira.
Fatuma Kuwa, mkazi wa Tabata Kisiwani jijini hapa, anasema ukusanyaji takataka katika eneo hilo si wa kuridhisha kutokana na uwezo mdogo wa kampuni inayokusanya taka.
“Kuna wakati magari ya kubeba taka yanapita lakini bado uchafu unasalia, hii ni kutokana na wingi wa taka ukilinganisha na idadi ya magari hayo.
“Nyumbani kwangu nina wapangaji watano, gari hupita mara moja au mbili kwa mwezi, kwa hiyo muda mwingi tunaishi na takataka zikiwa majumbani,” anasema.

Taka zikiwa zimewekwa pembeni ya barabara eneo la Magomeni kagera jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga
Hali hiyo pia inazungumzwa na Agnes Sapi, mkazi wa Gongo la Mboto jijini hapa, anayeeleza kuwa idadi ya magari yanayokusanya takataka mitaani haitoshelezi, hivyo kusababisha mlundikano wa takataka maeneo ya makazi.
“Kwa nionavyo, magari ya kubeba takataka hayatoshi, mahitaji ni makubwa. Mfano, huku kwetu yakipita mara moja, yanakaa muda mrefu bila kurudi na kusababisha takataka zijae na tunaishi nazo nyumbani,” anasema.
Wakati wakazi hao wakieleza hayo, uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa katika mitaa kadhaa jijini hapa, ikiwemo iliyopo wilayani Ilala, kuna mlundikano wa taka licha ya wananchi kusema magari hupita kuziondoa.
Mmoja wa makandarasi wa kukusanya taka jijini Dar es Salaam, Issaya Juma wa Kampuni ya Jonerry Enterprises, anasema miongoni mwa changamoto zinazofanya wasichukue taka kwa wakati ni kucheleweshwa kwa malipo kutoka serikalini.
“Miongoni mwa kinachoturudisha nyuma ni mfumo wa malipo wa Serikali kusuasua. Unaweza kukaa hadi miezi mitatu hujapewa fedha, tukiuliza tunajibiwa kuwa mfumo unasumbua. Hii inachangia kudorora kwa ufanyaji kazi wetu,” anasema Juma.
Ili kuondoa adha hiyo, Juma anaishauri Serikali kuboresha mfumo wake mpya wa malipo au kurudi kwenye ule wa zamani sambamba na kutoa elimu ya umuhimu wa fedha za taka kwa wananchi.
Kuhusu kusuasua kwa uzoaji wa taka, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, Septemba 24, 2022, katika zoezi la usafi wa pamoja katika Kata ya Kariakoo, aliziagiza Halmashauri kuhakikisha zinatoa zabuni za usafi kwa kampuni zenye sifa na vifaa vya uhakika, na si kutoa zabuni hizo kwa kampuni hewa au kwa kujuana.
“Nawataka makandarasi wa usafi mhakikishe mnabeba taka kwa wakati na kuwahimiza wananchi kulipa ada ya taka ili kusitokee mkwamo wa huduma hii,” aliagiza.
Zainabu Hussein, daktari wa binadamu na mtaalamu wa afya ya jamii, anasema mlundikano wa takataka katika makazi unaweza kusababisha magonjwa ya mlipuko.
“Mlundikano wa takataka unaweza kusababisha hatari kubwa kwa afya kwa kuwa huchochea kuzaliana kwa vimelea vya magonjwa kama bakteria, virusi na fangasi, ambavyo husababisha magonjwa kama kuhara, homa ya matumbo na magonjwa ya ngozi.
“Pia, takataka zinapooza huzalisha gesi hatari kama methane na sulfidi hidrojeni (ni gesi ya sumu, inayowaka na yenye harufu ya mayai yaliyooza), ambazo zinaweza kusababisha matatizo ya kupumua na mzio,” anasema.
Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004, kifungu cha 4 (1) na (2) vinaeleza mtawalia: “Kila mtu anayeishi Tanzania atakuwa na haki ya kuwa na mazingira safi, salama na ya kiafya.
“Haki ya kuwa na mazingira safi, salama na ya kiafya itahusisha haki kwa kila raia kutumia elementi za umma au sehemu mbalimbali za mazingira kwa madhumuni ya burudani, elimu, afya, ibada, utamaduni na uchumi.”
Sheria hiyo, katika sehemu ya pili, inaeleza kila mtu anayeishi eneo husika ana wajibu wa kutunza mazingira, huku kifungu cha 8 cha sehemu hiyo kikiwataja watumishi wa umma katika eneo husika kuwajibika katika hilo.
“Mtu yeyote anayefanya kazi ya umma, ambaye katika kutekeleza kazi hiyo anatakiwa kuchukua hatua yoyote, kutoa uamuzi, kuandaa, kurejea au kutekeleza sera, mpango, mkakati, sheria, mwongozo au taratibu zozote zinazoweza kuathiri usimamizi, uhifadhi au uendelezaji wa mazingira au usimamizi endelevu wa maliasili na rasilimali za kiutamaduni, atazingatia misingi ya usimamizi wa mazingira,” kinaeleza kifungu hicho.

Taka zikiwa zimewekwa pembeni ya barabara eneo la Magomeni jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga
Taarifa ya Jiji la Dar es Salaam
Taarifa ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam iliyochapishwa katika tovuti ya jiji hilo mwaka 2020 inaeleza ongezeko la aina tofauti za taka ngumu, zikiwemo za majumbani, viwandani na hospitalini, ambazo hutupwa maeneo mbalimbali na hivyo kusababisha uchafuzi wa mazingira (hewa, maji na ardhi).
“Jiji la Dar es Salaam linakadiriwa kuzalisha zaidi ya tani 4,600 za taka kwa siku. Kati ya hizo, ni asilimia 45 hadi 50 tu zinazopokelewa dampo, sawa na tani 1,200 hadi 2,000 za taka zinazokisiwa kuzalishwa kwa siku. Taka zinazobaki huishia kwenye maeneo ya wazi, mitaro ya maji, barabara na makazi.”
“Hali ya usafi wa Jiji la Dar es Salaam, hususan udhibiti wa taka ngumu, ni tatizo la muda mrefu ambalo lina changamoto nyingi. Tabia iliyozoeleka miongoni mwa jamii ya utupaji ovyo wa taka katika maeneo yasiyostahili imechangia Jiji kuwa chafu,” inaeleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa kuzagaa kwa taka kunaweza kuwa kichocheo cha milipuko ya magonjwa kama vile kipindupindu na mengine ya kuhara na kutapika.
“Hali ya uchafu jijini inachangiwa pia na elimu ndogo juu ya usafi wa mazingira, kutotii sheria zilizopo kwa upande wa wananchi, na usimamizi hafifu wa sheria za usafi wa mazingira,” inaeleza taarifa hiyo kuhusu chanzo cha tatizo hilo.
Inaelezwa katika taarifa hiyo kuwa:
“Ili kupunguza uchafuzi wa mazingira, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeandaa sera ya urejelezaji wa taka ngumu ambayo itakuwa ni msingi muhimu kwa taasisi za Serikali kuanza kutambua na kurasimisha sekta ya urejelezaji taka, ambayo awali ilikuwa ikiendeshwa na taasisi binafsi na vikundi visivyokuwa rasmi.”
Pia, inaelezwa kuwa katika kuhakikisha hilo linafanyika, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inalenga kufanya yafuatayo:
Kubuni miradi ndani ya jiji itakayohusisha wadau mbalimbali inayolenga urejelezaji taka na masoko ya uhakika ya taka zilizorejelezwa au bidhaa zilizotokana na taka rejea.
Kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa kurejeleza taka, ikiwa ni pamoja na kushirikiana na halmashauri za manispaa katika kuhakikisha utenganishaji wa taka unafanyika kuanzia ngazi za uzalishaji.
Jiji limesema litawatambua na kuwaunganisha wadau wanaojihusisha na teknolojia za urejelezaji taka ndani ya Jiji la Dar es Salaam na kutenga maeneo ya viwanda vidogo-vidogo au karakana ndani ya dampo au katika maeneo yake ambayo yatafaa kwa kazi zinazohusiana na urejelezaji taka.
Taarifa inaeleza kuwa jiji litahamasisha teknolojia zinazolenga uzalishaji na utumiaji wa bidhaa zitokanazo na taka rejea.
Litahakikisha linaweka mazingira bora yatakayowezesha ukuaji wa sekta ya urejelezaji taka ngumu kwa kuongeza viwanda na ubora wa bidhaa zake ili ziweze kupata soko ndani na nje ya nchi na hatimaye kukuza pato la jamii na Taifa.
“Kuwezesha wananchi wa maisha ya chini, wakiwemo vijana na wanawake, kushiriki katika ubunifu na utumiaji wa teknolojia za urejelezaji taka na hatimaye kuboresha usafi,” inaeleza taarifa hiyo.
Halmashauri ya jiji inalenga kuhakikisha kiwango cha juu cha uzuiaji wa uchafuzi wa mazingira kwa kuweka taratibu zitakazowezesha aina nyingi za taka zinazozalishwa katika jiji zirejelezwe ili kuwa na jiji safi.
Urejelezaji wa taka, fursa na changamoto
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni inayojihusisha na urejelezaji wa takataka ya Rootgis, Antidius Kawamala, anaunga mkono matokeo ya tafiti ya Down to Earth na ile taarifa ya Jiji la Dar es Salaam kuhusu kiwango kidogo cha jiji hilo kukusanya taka.
Kawamala anasema taka nyingi zinazoachwa katika makazi ya watu ni zile zinazotokana na masalia ya chakula kutokana na uchache wa miundombinu ya kukusanyia na kampuni za kufanya urejelezaji.
“Uhalisia ni kuwa zaidi ya asilimia 50 ya taka zinasalia majumbani, lakini pia nyingi ni za chakula ambazo si tu kuwa miundombinu ya ukusanyaji haitoshi, lakini fursa ya urejelezaji haijapewa kipaumbele kutokana na teknolojia,” anasema Kawamala.
Kawamala anasema kama kungekuwa na kampuni nyingi za urejelezaji zenye vifaa vya kiteknolojia, pengine kiwango cha taka kinachobaki majumbani kingepungua.
“Wakati mwingine shughuli ya urejelezaji inahitaji vifaa vya kiteknolojia ambavyo vitasaidia kuchambua na kuhifadhi taka kwa muda mrefu, ambazo mwisho wa siku zingeunda bidhaa mbalimbali,” anasema Kawamala.
Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya Rootgis anasema kuwa katika kuangalia fursa za taka, kwa sasa wapo katika tafiti ya namna ya kuzibadilisha na kutengeneza kamba kwa matumizi mbalimbali.
Nyongeza na Mintana Hunda