WAKATI katika Ligi Kuu Bara zimepigwa hat trick tatu tu hadi sasa kupitia mechi 181, huku kwenye Ligi Kuu ya Wanawake (WPL), kama hujui zimepigwa jumla 12, huku nyota wa JKT Queens, Stumai Abdallah akifunika kwa kupiga nne peke yake hadi sasa.
Hadi sasa katika ligi hiyo ya wanawake zimeshachezwa mechi za raundi 12, huku watetezi Simba Queens ikiwa kileleni kwa kukusanya pointi 34, ikifuatiwa kwa karibu na JKT yenye 32, lakini utamu ni jinsi mastaa wa kike wanavyotupia hat trick za kutosha wakati ligi ikisaliwa na raundi sita kufika tamati.
Katika hat-trick hizo 12, mshambuliaji wa JKT, Stumai Abdallah amefunga nne, Jentrix Shikangwa akiweka tatu, Neema Paul (Yanga Princess), Asha Djafar (Simba Queens), Ariet Adong (Yanga Princess), Milembe Ndalahwa (Alliance Girls) na Annastazia Lucian (Mashujaa Queens) wakifunga moja.
Mlandizi Queens ndiyo timu iliyofungwa hat-trick nyingi, ikiruhusu sita kati ya 12.
Stumai ndiye mchezaji aliyeifunga Mlandizi hat-trick nyingi, mbili, mzunguko wa kwanza akifunga mabao manne kwenye ushindi wa 7-0 uliopata JKT Queens, Novemba 05 na Februari 04 zilipokutana tena, JKT ilipata ushindi wa mabao 12-0, akafunga mabao saba peke yake.
Timu nyingine alizozifunga mshambuliaji huyo ni Alliance, Januari 21 kwenye ushindi wa mabao 4-0 na Machi 12 akikamilisha hat-trick ya nne dhidi ya Get Program.
Shikangwa pia aliifunga Mlandizi mabao manne pekee kwenye ushindi wa 11-0, Januari 22, akafanya hivyo tena Novemba 20 dhidi ya Get Program akiweka kambani mabao matatu kwenye ushindi wa 6-2.
Hat-trick ya tatu aliifunga dhidi ya Fountain Gate, Januari 28 kwenye ushindi wa mabao 4-2 iliyopata Simba.
Kwa upande wa Neema, aliifunga Get Program mabao manne peke yake kwenye ushindi wa mabao 5-0 iliyopata Yanga Machi 01.
Milembe naye alifunga mabao matatu dhidi ya Mlandizi, Desemba 21, Alliance ikiondoka na ushindi wa mabao 5-1.
Kwenye ushindi wa mabao 7-0 iliyopata Mashujaa Desemba 27 mwaka jana dhidi ya Mlandizi, Anastazia alifunga matatu.
Wengine waliofunga hat trick ni Udong aliyeweka kambani mabao matatu dhidi ya Ceasiaa, Yanga ikishinda mabao 4-1 huku Djafar wa Simba akifunga matatu dhidi ya Mlandizi Januari 22.