Timu 5 Ligi Kuu hazijawahi kupata ushindi ugenini Ligi Kuu Bara 2024/256

COASTAL Union na Kagera Sugar ni kati ya timu tano kati ya 16 zinazoshiriki Ligi Kuu Bara ambazo hazijapata ushindi ugenini msimu huu kwenye ligi hiyo.

Wakati msimu huu mambo yakiwa hivyo kwao zikisalia mechi saba, msimu uliopita timu hizo zilikuwa kati ya nane zilizoshinda mechi nyingi ugenini, huku Tabora United ambayo unaweza kusema kwa sasa imejipata, msimu uliopita ndiyo ilikuwa pekee haijashinda ugenini.

Kando ya Coastal Union na Kagera Sugar ambazo hazijashinda ugenini msimu huu, kuna KenGold, Tanzania Prisons na Dodoma Jiji.

Takwimu za Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya timu hizo kucheza jumla ya mechi 23, zinaonesha kwa ugenini pekee, KenGold ndiyo timu yenye matokeo mabaya zaidi ikicheza mechi 12 na kukusanya pointi mbili ilipotoka sare dhidi ya Tabora United (1-1) na JKT Tanzania (1-1). Katika mechi 12 za ugenini imepoteza 10 huku pia ikiwa ndiyo timu iliyoruhusu mabao mengi zaidi (26).

Inafuatia Kagera Sugar yenye pointi tatu ugenini baada ya sare dhidi ya Pamba Jiji (1-1), Mashujaa (1-1) na Singida Black Stars (2-2) ikiwa imecheza mechi 11 ikipoteza 8.

Tanzania Prisons iliyokusanya pointi nne ugenini ilikuwa sare dhidi ya Pamba Jiji (0-0), Mashujaa (0-0), Tabora United (0-0) na Kagera Sugar (0-0), huku ikipoteza mechi 8 kati ya 12.

Dodoma Jiji ina pointi tano za ugenini kwa matokeo ya sare dhidi ya Pamba Jiji (0-0), Fountain Gate (2-2), Tanzania Prisons (0-0), KenGold (2-2) na Namungo (2-2). Nayo imepoteza mechi 6 kati ya 11.

Coastal Union kwa timu ambazo hazijashinda ugenini ndio yenye pointi nyingi (8) baada ya kutoka sare dhidi ya KMC (1-1), Simba (2-2), Singida Black Stars (0-0), KenGold (1-1), Tabora United (1-1), Mashujaa (0-0), Namungo (0-0) na Dodoma Jiji (0-0). Imepoteza mechi 4 kati ya 12.

Ukiangalia msimamo wa ligi kwa mechi za ugenini pekee, Yanga inaongoza kwa kukusanya pointi 31 sawa na Simba zote zikikishinda mechi 10 na sare moja, ndiyo timu pekee zisizopoteza ugenini.

Singida Black Stars ya tatu pointi 22, Azam (19), Tabora United (15), Namungo (14), JKT Tanzania (12), Pamba Jiji (9), Fountain Gate (9), Coastal Union (8), Mashujaa (8), KMC (7), Dodoma Jiji (5), Tanzania Prisons (4), Kagera Sugar (3) na KenGold (2).

Mambo yakiwa hivyo ugenini, takwimu za mechi za nyumbani pekee, zinaiweka Namungo mkiani ikiwa na pointi 9, wakati Azam inaongoza ikiwa na 29.

Chini ya Azam kuna Yanga (27), Simba (26), Singida Black Stars (22), Dodoma Jiji (22), Tabora United (22), Fountain Gate (19), JKT Tanzania (18), Coastal Union (17), KMC (17), Kagera Sugar (16), Mashujaa (16), KenGold (14), Tanzania Prisons (14) na Pamba Jiji (13).

Related Posts