LIGI itapasuka vipande vipande ni maneno ya kocha wa Namungo, Juma Mgunda, ambaye aliyasema siku chache zilizopita kutokana na ushindani uliopo katika makundi tofauti. Wapo wanaosaka ubingwa, nne bora, huku wengine wakihangaika kujinasua na hatari ya kushuka daraja.
Achana na vita ya ubingwa ambayo inahusisha Simba, Yanga na Azam FC, pamoja na ile ya nne bora ambapo Singida Black Stars na Tabora United wanawania nafasi hiyo, kuna vita nyingine kubwa ya kusalia kwenye ligi.
Ushindani huu umefanya kila mchezo kuwa wa muhimu, huku kila timu ikihitaji matokeo mazuri ili kujiweka katika nafasi salama.
Kwa mujibu wa msimamo wa Ligi Kuu Bara, lolote linaweza kutokea kwa timu zilizo kuanzia nafasi ya saba hadi ya 16, kwani tofauti ya pointi baina yao ni ndogo mno. Katika michezo saba iliyosalia, kila timu itapambana kwa nguvu ili kuepuka kushuka daraja, huku ushindani ukiwa mkali zaidi kwa timu zinazoshika nafasi za chini.
Ukiwaondoa Yanga, Simba, Azam, Singida BS, Tabora United na JKT Tanzania ambao wamekusanya kuanzia pointi 30 na kuendelea, timu zilizo salama ni chache. Wananchi wanaongoza msimamo wakiwa na pointi 58, huku timu nyingine zikihangaika kujiweka katika nafasi salama.
Kundi jingine lenye timu 10, ambazo ni Fountain Gate (28), Dodoma Jiji (27), Coastal Union (25), Mashujaa (24), KMC (24), Namungo (23), Pamba Jiji (22), Kagera Sugar (19), Tanzania Prisons (18) na Kengold (16), ndilo linaloonyesha ushindani mkali wa kupambana kusalia kwenye ligi.
Hali ya mambo inafanya hata timu zilizoko juu kidogo kutojihisi salama, kwani mechi mbili hadi tatu zinaweza kupindua msimamo kabisa.
Ushindi wa mechi mbili zilizopita dhidi ya Prisons na KMC umeifanya Fountain Gate kusogea juu katika msimamo wa ligi. Hata hivyo, bado wana kazi kubwa mbele yao, kwani michezo saba iliyosalia si rahisi hata kidogo.
Ratiba inaonyesha wana michezo mitatu nyumbani dhidi ya Singida BS, Yanga na Azam. Hii ina maana kuwa hawatakuwa na mechi nyepesi hata moja, kwani Singida wanapigania tiketi ya michuano ya kimataifa, Yanga wapo katika mbio za ubingwa, na Azam wanataka kumaliza msimu wakiwa katika nafasi nzuri zaidi.
Mechi nne za ugenini ni dhidi ya Mashujaa, Pamba Jiji, JKT Tanzania na Coastal Union. Rekodi inaonyesha Fountain Gate imeshinda mechi tano, sare nne na kupoteza tatu kati ya mechi 12 ambazo wamecheza nyumbani msimu huu. Wakiwa ugenini wameshinda tatu tu na kupoteza mara nane kati ya mechi 11.
Baada ya mchezo wao wa kiporo dhidi ya Simba, Dodoma Jiji, wanakabiliwa na ratiba ngumu katika michezo yao saba iliyosalia. Wana mechi nne za ugenini dhidi ya JKT Tanzania, KMC, Azam na Yanga, ambazo zote ni mechi ngumu kwao.
Mechi zao za nyumbani ni dhidi ya Kengold, Kagera Sugar na Singida BS. Rekodi yao ya nyumbani inawapa matumaini, kwani katika michezo 12, wameshinda saba, sare moja na kupoteza nne. Lakini changamoto kubwa kwao ni rekodi yao ya ugenini ambapo hawajashinda hata mechi moja msimu huu.
Mabingwa wa zamani wa Ligi Kuu Bara, Coastal Union, hawapo katika hali nzuri, kwani kwenye michezo mitano iliyopita wameambulia pointi tatu pekee kwa kutoa suluhu dhidi ya Dodoma Jiji, Namungo na Azam FC. Kocha Juma Mwambusi ana kazi kubwa kuhakikisha wanajinasua kwenye hali hii.
Kwa kuangalia ratiba yao, wana mechi dhidi ya Kagera Sugar, Yanga, Singida BS, KenGold, Tanzania Prisons, Fountain Gate na Tabora United. Wanahitaji kupata ushindi katika mechi zao nyumbani, huku wakijitahidi kupunguza idadi ya mechi wanazopoteza ugenini.
Mashujaa wanakabiliwa na michezo saba iliyosalia ambayo ni: dhidi ya Fountain Gate, Tabora United, Namungo, Simba, Kagera Sugar, KMC na JKT Tanzania. Wanahitaji angalau kushinda mechi tatu ili kuwa katika nafasi salama.
Ratiba ya KMC ni ngumu kwani wanakabiliana na Tanzania Prisons, Namungo, Dodoma Jiji, Simba, Tabora United, Mashujaa na Pamba Jiji. KMC wanapaswa kuimarisha safu yao ya ulinzi na kuhakikisha wanatumia michezo ya nyumbani kupata ushindi.
Namungo wanakabiliana na ratiba yenye changamoto kubwa ambapo wanakutana na Pamba Jiji, KMC, JKT Tanzania, Mashujaa, Yanga, Kagera Sugar na KenGold. Kama wanataka kusalia Ligi Kuu, wanapaswa kushinda mechi zao za nyumbani na kutafuta sare angalau mbili ugenini.
Pamba wanakabiliana na ratiba ngumu, ikiwamo mechi dhidi ya Namungo, Tabora United, Fountain Gate, Simba, KenGold, JKT Tanzania na KMC. Ushindi wa mechi mbili kati ya hizo unaweza kuwa msaada mkubwa kwao.
Kagera Sugar wanakabiliana na Coastal Union, Tanzania Prisons, Dodoma Jiji, Azam, Mashujaa, Namungo na Simba. Kwa hali yao ya sasa, wanapaswa kuongeza juhudi kubwa ili kuepuka kushuka daraja.
Tanzania Prisons wanakutana na KMC, Kagera Sugar, KenGold, JKT Tanzania, Coastal Union, Yanga na Singida BS. Rekodi yao si nzuri, hivyo wanapaswa kufanya kazi ya ziada kuhakikisha wanapata ushindi kwenye michezo yao ya nyumbani.
KenGold wanakutana na Azam, Dodoma Jiji, Tanzania Prisons, Coastal Union, Pamba, Simba na Namungo. Kwa kuwa wapo nafasi ya mwisho kwa sasa, wanapaswa kushinda mechi kadhaa ili kujinasua kwenye janga la kushuka daraja.
Juma Mgunda (Namungo): “Tunahitaji kila mechi kucheza kama fainali. Hatutakubali kushuka daraja.”
Kwa upande wake, Juma Mwambusi (Coastal Union): “Ushindani ni mkubwa, lakini tunajiamini kuwa tunaweza kupata matokeo mazuri katika mechi zetu zilizobaki.”
Juma Kaseja (Kagera Sugar): “Tunahitaji ushindi katika mechi zijazo ili kujihakikishia nafasi ya kusalia kwenye ligi.”
Kwa jumla, vita ya kuendelea kusalia Ligi Kuu Bara imekuwa kali zaidi. Matokeo ya michezo saba ijayo yataamua hatma ya timu nyingi.