Dodoma. Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umewataka waajiri wenye wafanyakazi waliojiunga na mfuko huo kupeleka kwa wakati michango ya watumishi kabla hawajachukuliwa hatua za kisheria ikiwamo kufikishwa mahakamani.
Wito huo umetolewa leo Jumatatu Machi 17, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita jijini Dodoma.
Mkurugenzi huyo amesema ni jukumu la mwajiri na mwajiriwa kufahamu hali ya michango yake kwenye mfuko wa hifadhi za jamii na ndiyo maana kwa sasa kuna huduma za mtandao ambazo mwanachama anaweza kuingia kwenye mtandao wa NSSF na kuona mwenendo wa michango yake.
Amesema pale mwanachama atakapogundua hachangiwi amwambie mwajiri awasiliane na NSSF kwa sababu jukumu lao pia kumfuatilia mwajiri ili awasilishe michango hiyo.
Mshomba amesema jukumu hilo lipo pia kisheria kwa hiyo wanawafuatilia kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara, kwa mwaka wanatakiwa wafanye ukaguzi angalau mara mbili.
“Lakini, pale inaposhindikana huwa tunakaa naye anatuambia ni kwa namna gani atalipa. Tunasaini naye hati ya makubaliano (MOU) ikishindikana tunakwenda mahakamani, tutapata haki yetu, hivyo ndivyo tumekuwa tukifuatilia waajiri wasiowasilisha michango,” amesema Mshomba.
Amesema kwa wale ambao hawana uwezo wa kuingia kwenye mitandao kwa ajili ya kuangalia michango yao, wafike ofisi za NSSF watawaonyesha mwenendo mzima wa michango yao.
Mshomba amesema hata mwajiri ana wajibu wa kisheria wa kumpa mwenendo wa michango mfanyakazi wake.
Pia, amesema mfuko huo hutumia Sh850 bilioni kila mwaka kwa ajili ya kuwalipa wanachama wake wanaopoteza ajira na pia imetumia Sh11 bilioni kuwalipa wanachama wake waloondolewa kwenye ajira kwa kukosa elimu ya kidato cha nne.
Mbali na hilo amesema thamani ya mfuko imeongezeka kwa asilimia 92 kutoka Sh4.8 bilioni Februari 2021 hadi kufikia Sh9.2 bilioni Februari 2025.
Amesema ongezeko hilo limechangiwa na kuongezeka kwa wanachama, mapato yatokanayo na michango na kukua kwa thamani ya vitega uchumi vya mfuko.
“Jumla ya wanachama wapya 1,052,176 wameandikishwa katika kipindi cha miaka minne kilichoanzia Machi 2021 mpaka Februari 2025, Serikali ya awamu ya sita imetekeleza mikakati mbalimbali katika kuimarisha uchumi na kufungua fursa za uwekezaji na biashara.” amesema Mshomba.
Amesema kutokana na mabadiliko ya kanuni ya ulipaji mafao ya kustaafu (kikokotoo) yaliyofanyika na kuanza kutekelezwa Julai 2022, wastaafu wa NSSF walianza kupokea mkupuo wa awali wa asilimia 33 ukilinganisha na asilimia 25 waliyokuwa wakilipwa kabla ya mabadiliko hayo.
Pia, mfuko umeendelea kuboresha tena ulipaji wa mafao kwa wanachama wote waliokuwa wanalipwa mkupuo wa awali wa asilimia 33 na kuanzia Julai 2022, waliongezewa kiwango cha mkupuo kufikia asilimia 35.
Kupunguza tozo Daraja la Kigamboni
Mkurugenzi huyo amesema mfuko uliishukuru Serikali kuwaondolea kero wananchi wa Kigamboni waliokuwa na malalamiko ya muda mrefu kuhusu viwango vya tozo walizokuwa wakilipa wanapovuka Darajani.
Amesema kupitia uamuzi huo wa Serikali, viwango vya tozo vilishushwa na kuanzisha malipo kwa utaratibu wa vifurushi (bundle) ambavyo vina unafuu mkubwa kwa watumiaji wa daraja.
Pia, katika kipindi husika, mfuko umeendelea kuboresha mifumo katika Daraja la Nyerere Kigamboni na kupunguza matumizi ya fedha taslimu, hivyo kuongeza ufanisi na kupunguza upotevu wa fedha.
Wastani wa makusanyo ya mapato kwa mwezi yameongezeka kutoka Sh1.13 bilioni Februari 2021 hadi kufikia wastani wa Sh1.89 bilioni Februari 2025, sawa na ongezeko la asilimia 66.
Mshomba amesema gharama za kutumia Daraja la Kigamboni zimepungua kwa bodaboda na bajaji kutoka kulipa Sh1,500 kwa siku hadi kufikia Sh300 kwa bodaboda na Sh500 kwa bajaji.
Mkurugenzi huyo amesema mradi wa kuzalisha sukari wa Mkulazi umekamilika na kuanza kuzalisha sukari kupitia kampuni tanzu ya Mkulazi Novemba 2023 na kuanza uzalishaji Desemba 2023.
Kiwanda hiki kilizinduliwa Agosti 7, 2024 na Rais Samia Suluhu Hassan baada ya uzalishaji wa sukari ya majumbani kuanza Julai 2024 na hadi kufikia Februari 2025, jumla ya tani 19,124 za sukari ya majumbani zilizalishwa na kupelekwa sokoni.
“Kuanza uzalishaji wa sukari katika Kiwanda cha Mkulazi, kumesaidia kupunguza tatizo la uhaba wa sukari nchini na kuchangia kuongeza ajira kwa wananchi na kupunguza umaskini.
“Vilevile, kiwanda kimeweza kutoa fursa za ajira 8,302… ajira za moja kwa moja ni 1,665 na ajira zisizo za moja kwa moja ni 6,637. Mradi huu pia unatarajiwa kuzalisha megawati 15 za umeme ambazo kati yake megawati 7.5 zitaingizwa katika Gridi ya Taifa kupitia kituo cha kupokelea na kupooza umeme cha Msamvu mkoani Morogoro.