Arusha. Haya ndiyo madhara ya kujichukulia sheria mikononi. Ndicho kilichowakuta wakazi wawili wa Musoma, ambao wamekwaa kisiki Mahakama ya Rufani iliyobariki adhabu ya kunyongwa hadi kufa kwa kumuua mtu mmoja waliyemtuhumu kuiba mihogo.
Waliohukumiwa adhabu hiyo ni Kisika Omary na Juma Mweya ambao walimuua Shida Peter kwa kumkata na panga kichwani na kifuani kisha kuchoma mwili wake moto kwa kutumia nyasi na godoro.
Tukio hilo lilitokea Oktoba 16, 2019 katika Kijiji cha Buturu wilayani Butiama mkoani Mara saa 8 mchana, marehemua kiwa shambani kwake karibu na nyumbani kwake, warufani pamoja na Bahati na Juma Dinga walienda katika nyumba hiyo wakidai mihogo ya Bahati imeibwa.
Ilidaiwa marehemu aliwaruhusu kupekua eneo lake, lakini hawakupata chochote na Bahati alipendekeza wamuue kwani wakimpeleka mahakamani ataachiwa.
Marehemu alikimbia nyumbani kwake kujificha ila mrufani wa pili alivunja mlango wa nyumba hiyo na kuingia pamoja na wenzake, wakamkata marehemu kifuani na kichwani kwa kutumia panga kisha kuuteketeza mwili wake kwa kuuchoma moto.
Warufani hao walishtakiwa kwa kosa la mauaji kinyume na kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu.
Jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufani walioketi Musoma, wakiongozwa na Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma, Dk Mary Caroline Levira na Dk Benhajj Shaban Masoud, wametoa hukumu hiyo Machi 14, 2025 katika rufaa hiyo ya jinai namba 154 ya mwaka 2022.
Jaji Levira amesema baada ya kusikiliza hoja za pande zote, kuzingatia misingi ya kukata rufaa na kupitia kumbukumbu nzima ya rufaa hiyo, uamuzi wao utajikita katika masuala mawili ambayo ni iwapo ushahidi wa shahidi wa kwanza na nne walikuwa mashahidi wa kuaminika, kama shitaka dhidi ya warufani ililithibitishwa bila kuacha shaka.
Amesema kwa kuwa hii ni Mahakama ya Rufani ya kwanza katika kesi hiyo, wana haki kwa mujibu wa Kanuni za Mahakama ya Rufani Tanzania, kutathmini uya ushahidi huo na kufikia uamuzi wao.
Jaji Levira amesema warufani walishtakiwa kwa mauaji na kuwa mahakama ilijiuliza ikiwa warufani walihusika na kifo chake na kama walikuwa na nia mbaya ya kumuua marehemu,swali ambalo lilijibiwa na ushahidi wa shahidi wa kwanza na wa nne.
Hivyo,akasema wanatupilia mbali rufaa hiyo kwa sababu haina mashiko na hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Musoma ilikuwa sahihi.
Rufaa hiyo inatokana na hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, Februari 28, 2022.
Shahidi wa kwanza wa Jamhuri, Tumaini Peter Sambaganye na shahidi wa nne Peter Shida (mtoto wa marehemu), walidai kuwaona warufani hao na watu wengine wakidai mihogo ya Bahati imeibwa.
Walidai kuwa baada ya kuingia ndani, walimtoa marehemu nyumbani kwake na mrufani wa pili akamkata kifuani kwa kutumia panga, Sadick akamkata kichwani na Mabula akampiga na mchi nyuma ya kichwa chake,marehemu alianguka chini na kumpeleka nyuma ya nyumba yake, wakakusanya nyasi zilizokauka na kumfunika.
Shahidi wa kwanza alidai mrufani wa kwanza alimchoma moto na wakati akiungua, Juma Dinga alichukua godoro kutoka nyumba ya marehemu na kuiweka juu ya nyasi zinazoungua zilizokuwa zikiwateketeza marehemu.
Shahidi wa tatu, Sajenti Asukile akiwa na askari wenzake walidai kufika eneo hilo na kukuta umati mkubwa wa watu huku mwili wa marehemu ukiteketea.
Shahidi huyo alidai kuona kuona jeraha kwenye kifua cha marehemu na katika uchunguzi wake, alipata taarifa kuwa marehemu alipigwa na kundi la watu na kwa kuwa Kisika alikuwa bado eneo la tukio alikamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi Butiama na shahidi wa pili, Koplo Lawrence alimkamata mrufani wa pili.
Katika utetezi wake Kisika, alikiri kukamatwa katika eneo la tukio, ambapo inadaiwa alikuwa akilinda mihogo yake ya wizi iliyokutwa nyumbani kwa marehemu na kuwa walipekua nyumba ya marehemu ambapo walikuta mihogo na mali nyingine za wizi kutoka kwa watu wengine.
Alidai wanakijiji walimvamia marehemu hadi akafa hivyo kukana kuhusika kumshambulia marehemu.
Ushahidi wake ulithibitishwa na ushahidi wa mkewe Bahati Fwelefwele, ambaye alidai kuwa mtu wa kwanza kugundua mihogo yao iliibwa shambani na hivyo kumjulisha mumewe na kudai wanakijiji ndiyo walimshambulia marehemu.
Mrufani wa pili (Juma) alidai kuwa miongoni mwa watu waliokusanyika nyumbani kwa marehemu na kudai alipofika eneo la uhalifu, alikuta tayari marehemu ameshauawa.
Mahakama Kuu ilipima ushahidi wa pande zote mbili na kuja na matokeo kwamba, upande wa mashtaka umethibitisha kesi yake dhidi ya warufani bila shaka yoyote na kuwatia hatiani na kuwahukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.
Warufani hao hawakuridhika na adhabu hiyo na kukata rufaa ambapo walikuwa na sababu tatu ikiwemo Jaji aliyesikiliza kesi hiyo kukosea kuwatia hatiani kwa ushahidi wa shahidi wa kwanza na wanne ambao hawakuwa mashahidi waaminifu hivyo ushahidi wa mashtaka haukuthibitishwa.
Nyingine ni kutokueleweka kwa ushahidi kwenye kumbukumbu na Mahakama Kuu na kusababisha hatia ya makosa ya warufani.