Wananchi wa Idete wapanda juu ya miti, vichuguu kutafuta mawasiliano

Morogoro. Zaidi ya wananchi 7,000 wa kijiji cha Idete, kata ya Chanzulu, Wilaya ya Kilosa, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikosa mawasiliano ya simu na kulazimika kupanda miti mirefu na vichuguu kutafuta mtandao, sasa wamepata matumaini ya kuondokana na changamoto hiyo.

Matumaini hayo ni baada ya Serikali kwa kushirikiana na kampuni ya mawasiliano ya Airtel kuanza ujenzi wa mnara wa simu katika kijiji hicho, ambapo mnara huo unatarajiwa kuwashwa rasmi Aprili Mosi mwaka huu.

Akizungumza mbele ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, ambaye alifika kijijini hapo juzi Machi 15, 2025 kukagua maendeleo ya ujenzi wa mnara, mwenyekiti wa kijiji hicho, Adrian Aron, amesema kuwa Kijiji cha Idete hakikuwa na mnara wa mawasiliano ya simu ya aina yoyote, na siku zote wamekuwa wakipanda juu ya miti mirefu, miinuko na kwenye vichuguu kutafuta mtandao, hivyo ujenzi wa mnara huo utawasaidia kupata mawasiliano ya uhakika.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, hali hiyo imewafanya wakose mawasiliano ya kifedha, taarifa za masoko ya bidhaa, na hata taarifa za kimataifa.

Aron alieleza kuwa, kutokana na kukosekana kwa mtandao wa simu, wananchi walilazimika kutembea umbali mrefu wa zaidi ya kilometa 18 kutafuta maeneo yenye mawakala wa simu ili kufanikisha miamala ya kifedha.

Mwenyekiti huyo amesema kukosekana kwa mawasiliano ya simu kunawafanya wananchi wakose taarifa muhimu za duniani zikiwemo taarifa ya masoko ya bidhaa wanazozalisha yakiwemo mazao ya biashara wanayolima ambayo ni ufuta, tangawizi na maharage kutokana na kukosekana kwa mtandao wa simu kijijini hapo.

“Watapata huduma bora za simu, huku shughuli za kifedha na biashara zikiboreshwa kwa urahisi zaidi. Taarifa muhimu kutoka kwa Serikali, taasisi za kifedha na masoko zitakuwa na manufaa kwa wananchi wa Idete, na hivyo kuboresha hali yao ya maisha kwa ujumla,” amesema.

Mwalimu Jumanne Machela ambaye ni mkazi wa kijiji hicho cha Idete, amesema hata anapoingiziwa mshahara mwisho wa mwezi bado ilimlazimu kusafiri kwenda wilayani Kilosa au makao makuu ya kata hiyo ya Chanzulu kutafuta huduma za kifedha kwa mawakala ili aweze kutoa fedha kwa ajili ya matumizi yake.

“Ikitokea msiba hapa kijijini ama mtu mzima au mwanafunzi kaugua ghafla njia ya kuwapa taarifa ndugu ama wazazi wake ni kwenda nyumbani kumpa taarifa ama kumfuata shamba hakuna namna nyingine yoyote ya kupashana habari, yani huku tulipo tunapeana taarifa kwa mdomo,” amesema Machela.

Jenista Sekwao amesema kukosekana kwa mawasiliano katika kijiji hicho kulikuwa kuhatarisha usalama wa wananchi wa kijiji hicho kwa kuwa ni vigumu hata kuwasiliana na polisi.

“Akiingia jambazi hapa kijijini na usiku akavamia nyumba moja hadi nyingine na tunaweza kupata madhara makubwa, kwa sababu hakuna atakayeweza kuwapiga simu polisi kwa sababu mawasiliano hakuna, amesema Sekwao.

Kwa upande wake Waziri Jerry Silaa ameziagiza kampuni za simu pamoja na wakandarasi waliopewa kazi ya kujenga minara ya mawasiliano kuhakikisha wanakamilisha kazi hiyo kwa haraka na itakapofika Mei 12 saa sita kamili usiku minara yote 758 iwe imeshawashwa Ili wananchi waweze kutumia mawasiliano ya simu.

“Ikifika Mei 12 mwaka huu tunataka minara yote 758 iwe imeshawashwa nchi nzima na hatutaongeza hata sekunde moja niwatake makampuni ya simu ya Halotel, Airtel, Voda, Yas na TTCL kushirikiana na wakandarasi waliopewa hii kazi ya kujenga minara kuhakikisha wanamaliza kazi kabla ya mkataba kuisha,” amesisitiza Silaa.

Amesema Serikali imetenga jumla ya Sh126 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa minara 758 itakayojemgwa nchi nzima na katika ujenzi huo ipo minara itakayojengwa upya na mingine itakayoongezewa nguvu ambapo mpaka sasa minara 420 nchini nzima tayari imeshashawashwa.

Waziri Silaa amesema mbali ya kupata mawasiliano lakini pia uwepo wa minara hiyo itasaidia wananchi hasa wakulima kupata taarifa za masomo ya bidhaa zao na hivyo kuongeza kipato.

Akitoa taarifa ya ujenzi wa  minara hiyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa  Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Mhandisi Peter Mwasalyanda amesema mradi wa ujenzi wa minara 758 inayojengwa nchi nzima  ulianza kutekelezwa Mei 13, 2023 na kwamba ujenzi huo uliofanywa kwa kujenga minara mipya na kuongeza nguvu minara iliyopo na kufikia 3G na 4G.

“Katika minara 758 inayojengwa nchi nzima mkoa wa Morogoro umekuwa ni mkoa unaoongoza kwa kuwa na minara mingi ipatayo 69 na kati ya minara hiyo 34 ipo inajengwa katika Wilaya ya Kilosa, mkoa wa pili unaoongoza kuwa na minara mingi ni mkoa wa Tabora ambao unajumla ya minara 50,” amesema mhandisi Mwasalyanda.

Mhandisi Mwasalyanda ameongeza kuwa mpaka sasa minara 304 nchi nzima tayari imeshaongezwa nguvu na kukamilika kwa asilimia 100, na minara 420 tayari imeshawashwa na wananchi wanafurahia mawasiliano.

Kwa upande wake Mkuu wa Mawasiliano wa Kampuni ya Airtel, Jackson Mmbando ameishukuru Serikali kupitia UCSAF kwa kuwaamini kuwa sehemu ya utekelezaji huo wa minara ukiwemo mnara uliojengwa kwenye Kijiji cha Idete kata ya Chanzulu wilaya ya Kilosa.

Mmbando amesema hadi kufikia Aprili Mosi mwaka huu mnara wa Idete utakuwa imeshawashwa ambapo amesema kuwashwa huko licha ya wananchi kupata mawasiliano lakini pia kutawezeaha upatikanaji wa ajira za uwakala wa kampuni hiyo ya simu.

Awali akitoa taarifa ya wilaya, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa ambaye pia ni kaimu Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Shaka Hamdu Shaka amesema ujenzi wa minara katika wilaya hiyo  umeleta matumaini kwa wananchi ambao wengi ni wakulima wanaotegemea mawasiliano kupata taarifa za masoko na mwenendo wa hali ya hewa.

Related Posts