BENCHI la ufundi la Simba linazidi kukuna kichwa juu ya jereha linalomsumbua beki wa kati, Fondoh Che Malone aliyepelekwa Morocco kwa ajili ya kufanyiwa matibabu kwa lengo la kuwahi mapema kabla ya timu kukabiliana na ratiba ngumu kuanzia mwezi ujao hadi Mei.
Simba iliyopo nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Bara na hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, imemkosa Che Malone katika mechi tatu zilizopita zikiwamo mbili za Ligi Kuu na moja ya Kombe la Shirikisho (FA) kutokana na kuumia siku ya mechi dhidi ya Azam.
Mechi hiyo ya Dabi ya Mzizima ilipigwa Februari 26 na beki huyo alitumika kwa dakika 20 kabla ya kutolewa kumpisha Chamou Karabou baada ya kuumia na kulikosa pambano lililofuata dhidi ya Coastal Union na Dodoma Jiji pamoja na lile la 32 Bora ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya TMA Stars.
Kwa sasa Simba imesaliwa na wiki mbili kabla ya kurejea katika jukumu la mechi za Kombe la Shirikisho Afrika itakapokutana na Al Masry ya Misri Aprili 2 kabla ya kurudiana Aprili 9, huku ikiwa na uwezekano mkubwa wa kumkosa Malone aliyepo Morocco kwa matibabu.

Hesabu za mabosi wa Simba ni kwamba kama Malone atakosa mechi za CAF, basi awepo katika zile nane za kumalizia msimu wa Ligi Kuu Bara kikiwamo kiporo cha Dabi ya Kariakoo iliyoshindwa kuchezwa Machi 8 baada ya Bodi ya Ligi kuiahirisha.
Mabosi wa klabu hiyo wameamua kumsafirisha Che Malone hadi Morocco kwa ajili ya kupata matibabu ya uhakika ili apone haraka, huku wataalamu wakifichua ili kurejea kwa upasuaji alioenda kufanyiwa itachukua kati ya wiki tatu hadi nne kabla ya kurejea tena uwanjani.
Hapo awali Mwanaspoti liliandika kwamba baada ya beki huyo kupata majeraha, Simba iliamua kumtafutia daktari maalumu, huku tatizo lake likiwa halijawekwa wazi. Hata hivyo baada ya mambo kuwa makubwa sasa imefahamika klabu inapambana kumwezesha arudi mapema uwanjani.
Mwanaspoti linafahamu, beki huyo anayeichezea Simba msimu wa pili anasumbuliwa na majeraha ya kuchanika kwa nyama za paja. Taarifa za ndani zinasema kuwa, beki huyo amepelekwa Morocco kwa matibabu zaidi na akiwa huko atafanyiwa upasuaji wa kutobolewa (Laparoscopic Surgery) ambao ni wa kisasa zaidi.
Jeraha hilo kitaalamu linaweza kupona ndani ya wiki tatu hadi nne na hasa kama mchezaji anajitunza vyema, kitu ambacho Simba inapambana kutokana na umuhimu wa beki huyo aliyewezesha timu hiyo kuwa yenye ukuta mgumu kwani imeruhusu mabao manane tu kupitia mechi 22 za ligi.

Simba inafanya juhudi zote hizo ili staa huyo asikosekane katika michuano ya CAF itakayoanza Aprili 2 ikianzia ugenini dhidi ya Al Masry ambayo ni wazi hataweza kuiwahi kabla ya kurudiana nayo Aprili 9 jijini Dar es Salaam na mshindi wa jumla atapenya kwenda nusu fainali ya michuano hiyo.
Hesabu za mabosi wa Simba ni kwamba kama itashindikana Malone kurudi mapema, kwa mechi hizo basi kama itafuzu awepo katika nusu fainali na mechi nyingine za Ligi Kuu zilizoshikilia hatma ya ubingwa kwa msimu huu ikichuana na Yanga ambayo bado hawajamalizana nayo.
Kutokana na umuhimu wa beki huyo anayecheza sambamba na Abdulrazaq Hamza na Chamou Karabou, mabosi ndio maana wameamua kumsafirisha hadi Morocco ambako inaelezwa kuanzia muda wowote atafanyiwa upasuaji huo wa kisasa utakaomrejesha mapema uwanjani.
Mbali na mabeki hao watatu, pia nafasi hiyo ina Hussein Kazi ambaye hajaonekana uwanjani kwa muda mrefu, lakini kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids akiwatumia zaidi Malone na Hamza na muda mwingine Malone na Chamou.
WASIKIE MADAKTARI
Daktari Samwel Shita, alisema inategemea na ukubwa wa jeraha, huwa kuna daraja la kwanza, pili na tatu la jeraha la misuli na la mwisho ndilo linahitaji upasuaji na linachukua kupona ndani ya muda wa miezi 3-6.
“Kupona na kufanyiwa Laparoscopic Surgery (upasuaji wa matundu) ni wa kisasa, kwani wanatoboa matundu wanapenyeza vifaa vya upasuaji ni tofauti na ule wa zamani,” alisema Dk Shita ambaye ni mchambuzi wa Mwanaspoti akiandika uchambuzi kila Alhamisi, aliyeongeza:
“Wanapasua mkato mrefu, msaada wake ni kuwa kuna damu chache inapotea, jeraha la upasuaji ni dogo mgonjwa anaweza kutoka mapema hospitali kwa sababu vijeraha vya upasuaji ni vidogo vitundu tu.”
Daktari wa Taifa Stars, Gilbert Kigadye alisema jeraha la kuchanika kwa nyama za paja kwa mchezaji uponaji wake unategemea na mhusika mwenyewe.

“Huwa hawafanyi upasuaji ila inaweza kuwa njia rahisi ya kumfanya mchezaji apone haraka au kuna kitu kingine kinamsumbua, lakini akipewa matibabu mazuri hawezi kuchukua muda mrefu,” alisema Dk Kigadye na kuongeza:
“Mchezaji akipata jeraha hilo anaweza kukaa nje kwa muda wa wiki tatu mpaka nne, lakini kama ataamua kutulia bila kuutonesha kwa kucheza au kufanya mazoezi.”
Daktari mwingine wa klabu ya Ligi Kuu (jina limehifadhiwa) alisema inategemea na aina ya jeraha kuna kuchanika kwa nyama za paja kwa upande wa mbele na nyuma.
“Tukizungumzia mbele, mara nyingi kupona kwake huwa ni kwa haraka zaidi kuliko nyuma, kwa sababu kunategemea kumechanika kwa ukubwa gani, ambako ndiko kunaamua akae nje kwa muda mrefu kiasi gani,” alisema.
“Hatua ya awali anaweza kukaa siku 10-14 ya pili wiki nne hadi sita na ya tatu ni miezi miwili hadi mitatu, kama atapata matibabu mazuri ambayo ndio jambo la muhimu sana, basi mchezaji anaweza kuwahi kupona.”