KENGOLD bado inapasua kichwa ikitaka kubaki Ligi Kuu Bara, lakini imezitaja mechi mbili zinazoweza kuwa kikazo kwao ambazo ni dhidi ya ni Simba na Azam FC.
Kikosi hicho kimesalia na mechi saba, ambazo ni dhidi ya Azam (nyumbani), Dodoma Jiji (ugenini), Tanzania Prisons (nyumbani), Coastal Union (ugenini), Pamba Jiji (nyumbani), Simba (nyumbani) na Namungo (ugenini).
Kocha Mkuu wa KenGold, Vladislav Heric ameliambia Mwanaspoti kuwa, kwenye mechi zao saba zilizosalia kuna michezo miwili dhidi ya Azam na Simba ndio inawaumiza kichwa.
Heric ambaye tangu atambulishwe kikosini hapo Januari mwaka huu ameshindwa kukaa benchi kutokana na kutokidhi vigezo vya kuwa kocha mkuu, alisema kikosi chake kinajipanga kutafuta alama nne au tatu kwenye mechi hizo mbili ili kuhakikisha wanasalia ligi kuu.
Kocha huyo amesema kikosi chake kitazicheza michezo hiyo kama fainali ili kuchukua pointi zote tatu endapo tu maamuzi yatakuwa ya haki.
“Mechi ambazo zinatuumiza kichwa ni dhidi ya Simba na Azam, unajua hizi ni timu mbili bora kati ya tatu au nne, unaona na wao wana hesabu zao kule juu, lakini tuna malengo yetu, hapo kuna pointi tutazitaka kama sio zote basi angalau tatu au nne.
“Hizi mechi zingine tano zilizosalia kwa kikosi tulichonacho, naona tuna nafasi ya kushinda, kitu muhimu ni kuzicheza kama fainali kwetu, nitawaambia wachezaji wangu tutakuwa na kazi ngumu, hatutakiwi kuruhusu kushuka daraja.
“Tunaamini maamuzi pia yatakuwa sawa, kuna mambo yalitokea kwenye mchezo dhidi ya JKT Tanzania yalituumiza sana, ile ni mechi ambayo tulitakiwa kushinda,” alisema kocha huyo.
KenGold iko kwenye hatari ya kushuka daraja ambapo sasa ipo nafasi ya mwisho katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, ikiwa na alama 16 katika mechi 23, huku ikishinda michezo mitatu, sare saba na kupoteza 13.