Morogoro. Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linamtafuta Abubakari Mwichangwe, dereva wa lori la kusafirisha mafuta, mkazi wa Dar es Salaam anayetuhumiwa kula njama ya kuiba mafuta na kuchoma moto lori hilo ili kupoteza ushahidi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama akizungumza na Mwananchi amesema tukio hilo lilitokea usiku wa Machi 16, 2025.
Amesema dereva huyo akiwa anaendesha lori aina ya FAW, mali ya Kampuni ya Meru likiwa na shehena ya mafuta akitokea Dar es Salaam kwenda Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) alikula njama na wenzake watatu na kuiba mafuta.
“Dereva huyo alikula njama na wenzake watatu ambao ni mameneja wa vituo vya mafuta vya Kampuni ya Simba Oil ya mkoani hapa (Morogoro) na baada ya kuiba mafuta hayo aliendelea na safari, huku gari hilo likiwa tupu. Alipofika eneo la Msufini, Kijiji cha Msimba barabara ya Mikumi – Iringa kwa makusudi aliliingiza gari hilo kwenye korongo kwa lengo la kutaka kumuaminisha bosi wake kuwa limepata ajali,” amesema.

Lori la mafuta la kampuni ya Meru ya Dar es Salaam likiwa limeegeshwa nje ya kituo cha Polisi Morogoro. Picha Hamida Shariff
Kamanda Mkama amesema baadaye dereva huyo aliwasha moto akijaribu kuliteketeza gari hilo, lakini kabla moto haujashika walitokea wasamaria wema waliouzima na kutoa taarifa polisi.
Amewaja watuhumiwa waliokula njama na dereva huyo kufanya wizi ni Hamidu Sudi (50), mkazi wa Dar es Salaam, Abiner Shalon (25) na Abdallah Nihed (30) wakazi wa Morogoro, ambao wote ni mameneja wa vituo vitatu vya mafuta vya Kampuni ya Simba Oil vilivyopo mkoani Morogoro.
Amesema kwa kushirikiana na dereva, watuhumiwa waliiba lita 35,700 za dizeli yenye thamani ya Sh77.1 milioni iliyoshushwa kwenye vituo vya Simba Oil.
“Pamoja na kumsaka (dereva) ambaye tunaamini muda si mrefu tutampata, pia, tunaendelea na uchunguzi wa tukio hili kwa kushirikiana na vyombo vingine, ikiwamo Ewura na TRA,” amesema.
Kamanda ametoa onyo na karipio kwa madereva akiwataka kuacha tamaa ya kupata mali kwa njia ambazo si halali.
Amewapongeza wananchi wa Kijiji cha Msimba kwa kutoa taarifa mapema kuhusu tukio hilo.
Katika vituo hivyo vya mafuta, Mwananchi imezungumza na wananchi wanaofanya shughuli jirani ambao wamesema vimefungwa tangu Mei 16, 2025.

Mfanyabiashara Said Abdallah, ambaye pia hujishughulisha na uzibaji pancha jirani na kituo kimojawapo amesema Mei 16 akiwa kwenye shughuli zake aliona askari polisi wakiwa na watu wengine walifika kwenye kituo hicho na kuamuru kifungwe mpaka uchunguzi utakapokamilika.
“Nikiwa hapa kwenye shughuli zangu niliona gari la polisi likiwa na askari, walikuja na watu wengine baada ya kuondoka tukaona kituo hiki kimefungwa na hakifanyi kazi mpaka leo Machi 18,” amesema.
Alif Mbaraka, mmoja wa wasimamizi wa Kampuni ya Simba Oil, ambaye ni mwanafamilia ya wamiliki wa kampuni hiyo amekiri vituo kufungwa tangu mchana wa Machi 16 na pia kukamatwa kwa mameneja, akiwamo wa kituo kilichopo Mkambarani.
Akizungumza na Mwananchi amesema siku ya tukio akiwa ofisi jirani na kituo kilichopo katikati ya mji wa Morogoro alishuhudia maofisa wa polisi na Ewura wakifunga utepe kuzunguka mashine za kuuzia mafuta, wakati huo hakuwa akijua nini kimetokea.
Amesema alipokwenda eneo hilo alikuta meneja ameshakamatwa.
“Ilibidi niende polisi kufuatilia nilipofika niliwakuta mameneja wetu wawili wa hapa mjini na Mkambarani,” amesema.
Amesema akiwa polisi alizungumza na meneja mmoja akasema mafuta hayo aliyapokea kutoka kwa meneja wa Simba Oil Dar es Salaam.
Mbaraka amesema meneja huyo aliyapokea kwa maelekezo kuwa ni ya kampuni moja ya mafuta ambayo inaingia mkataba na Simba Oil kuyahifadhi kwenye visima vya Simba Oil.
“Mimi binafsi silijui hili,” amesema Mbaraka akieleza wamepata hasara wao binafsi na kampuni za minara ya simu ambazo huchukua mafuta kwenye vituo vya Simba Oil.
Hata hivyo, Mbaraka amesema hawezi kuzungumzia tukio hilo zaidi kwa kuwa husimamia biashara anapokuwa Morogoro lakini makazi yake ni Bagamoyo.