YANGA Princess imemaliza ubabe wa Simba Queens baada ya kuichapa bao 1-0 kwenye mchezo mkali wa Ligi Kuu ya Wanawake uliopigwa leo Machi 19, 2025 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar.
Kabla mchezo huu, Simba Queens ambao wanaendelea kuwa kileleni kwenye msimamo wa ligi hiyo, walikuwa hawajapoteza mchezo wowote msimu huu kati ya 12 waliyocheza.
Lakini pia hii ni kama Yanga Princess imeanza kuamka kutokana na kunyanyaswa na wapinzani wao hao kuanzia zilipoanza kukutana kwenye ligi mwaka 2019, zikicheza mechi 12, Simba Queens ikishinda tisa, sare moja na kupoteza moja.
Katika mchezo wa leo ambao Yanga Princess ilionekana kumiliki mpira kwa asilimia kubwa na kupoteza nafasi kadhaa za wazi, Jeannine Mukandayisenga ndiye alifanikiwa kuifungia timu hiyo bao pekee dakika ya 48 baada ya kutumia vyema makosa ya mabeki wa Simba.

Kutokana na ushindi huu, Yanga imefikisha pointi 27 ikiwa imefufua matumaini ya ubingwa kwani ipo nyuma ya vinara Simba Queens kwa tofauti ya pointi saba zikiwa zimebaki mechi tano ligi hiyo imalizike.
Hata hivyo presha sasa ni kubwa kwa Simba Queens kwani endapo JKT Queens itaibuka na ushindi kesho dhidi ya Mashujaa Queens itakaa kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya pointi moja kwani itafikisha 35.

Kocha wa Yanga Princess, Edna Lema ‘Mourinho’ amewapongeza wachezaji kwa matokeo hayo huku akifichua kwamba walijiandaa vizuri ndiyo maana wameshinda hivyo sifa zote ziende kwa wachezaji.
Naye Kocha wa Simba Queens, Yussif Basigi, amesema licha ya kupoteza mchezo huo, lakini bado wana matumaini ya kubeba ubingwa wa ligi hiyo msimu huu.