Dar es Salaam. Harufu mbaya, ubovu na kumwaga taka njiani ni miongoni mwa kero zilizoibuliwa na wananchi jijini Dar es Salaam kuhusu magari yanayotumika kubeba taka.
Licha ya magari hayo kufanya shughuli hiyo muhimu, yapo malalamiko kuhusu ubora wake, huku wengi wakiyanyooshea vidole kuwa ni miongoni mwa vyanzo vya kuongeza taka nayo yakiwa ‘takataka’
“Haya magari yapo katika hali mbaya, mabovu na mengi yanamwaga takataka barabarani ndiyo maana ukielekea njia ya dampo (Barabara ya Pugu) utakutana na takataka nyingi njiani,” anasema Moses Bura, mkazi wa Gongo la Mboto.

Godfrey Njau, dereva wa gari la taka katika maeneo ya Sinza na Ubungo anaeleza sababu ya taka kudondoshwa barabarani.
“Kuhusu kumwaga takataka njiani, hiyo kero ipo sana na ukiangalia barabara ya kuelekea dampo (la Pugu Kinyamwezi) njiani unazikuta kwa sababu yapo baadhi ya magari ambayo hayajazibwa kama inavyohitajika kwa hiyo unakuta katika tuta takataka zinamwagika,” anasema Njau.

Taka zikiwa zimeachwa barabarani eneo la Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam. Picha na Edwin Mjwahuzi
Rare Sapphire, mkazi wa jijini hapa anazungumzia ubovu wa magari hayo kupitia mtandao wa kijaamii wa Jamii Forum akiyafananisha na takataka.
“Hivi umeshawahi kukutana na gari la kuzoa taka lenye hali nzuri? Magari yote ambayo nimewahi kukutana nayo yanakuwa yameisha, yana hali mbaya, kutu kila pahala, yamechoka na yanajikokota kwelikweli kutoka eneo moja kwenda eneo jingine!
“Kwa nini magari haya yanaruhusiwa kufanya kazi katika hali hiyo? Yaani ni kama upo na bomu, hata ukajigonga tu bahati mbaya likakuchana ni msala! Uwajibikaji kwenye suala zima la uzoaji taka ni sifuri, utafikiri hakuna watu wanaosimamia eneo hilo.”

Sapphire anadai labda wanaopewa tenda hawapewi vigezo vya vifaa wanavyotakiwa kutumia kukamilisha kazi hiyo.
“Pia, licha ya hayo, hujaongelea mazingira na vifaa wanavyotumia wazoaji taka wenyewe, huu utakuwa mjadala wa wakati mwingine. Kwanini magari haya yanaruhusiwa kufanya kazi?” amehoji.
Juni 7, 2023 katika maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alisema zipo kampuni za kuzoa takataka zinazoshindwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo, kwa sababu ya uwezo mdogo.
Akizungumza katika Soko la Kisasa la Machinga lililopo jijini Dodoma, alisema ifike wakati mamlaka za Serikali za mitaa zitoe zabuni kwa kampuni zinazojishughulisha na kazi ya kuzoa taka zenye uwezo wa kufanya kazi hiyo kwa ufanisi.
“Kwa mfano, unakuta kampuni iliyopewa zabuni ya kuzoa taka, magari wanayotumia nayo takataka. Unakuta gari liko wazi taka zinatoa harufu kali inayosababisha kero kwa wananchi. Ninavyosema hivi, watumiaji wa Barabara ya Pugu kule Dar es Salaam nadhani wananielewa vizuri,” alisema Dk Mpango akiagiza kuwekwa miundombinu ya uhakika ya kuzoa taka katika mitaa na maeneo ya mikusanyiko ikiwemo masoko, stendi na hospitali.

Taka zikiwa zimewekwa pembeni ya barabara eneo la Magomeni kagera jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga
Njau, dereva wa gari la kubeba taka akizungumzia sababu ya magari hayo kuwa machakavu anasema ni kutokana na shughuli zake na mazingira ambayo yanafanyia kazi, ikiwamo dampo.
“Magari mengi yananunuliwa yakiwa katika hali nzuri, lakini kadri yanavyozidi kutumika ndiyo yanaharibika kutokana na shughuli za kule dampo, unakuta gari inaharibiwa na ‘operator’ ya dampo,” anasema Njau ambaye ni dereva wa magari hayo kwa miaka minane sasa.
Sababu nyingine anasema ni wamiliki wa magari hayo ambao wakiona limeharibika hawayatengenezi.
“Mmiliki akishaona vile basi anaamua kuendelea nalo kama lilivyo. Lakini pia kuna dhana ya kusema kwa kuwa linabeba uchafu acha liendelee kuwa vivyo hivyo, hii ina athari zake,” anasema.
Mmiliki wa magari ya taka ya Kampuni ya Umoja Group, Kasius Ndiyamkama anasema chanzo cha magari hayo kuwa mabovu ni kutokana na aina ya takataka wanazobeba kuwa na kemikali, hivyo wananchi wasiyabeze.
“Mwonekano siyo sababu ya kuyadharau magari ya taka kwani yapo machache sana ambayo hufanya kazi hiyo, isitoshe magari yetu yanabeba taka za aina nyingi zenye kemikali tofauti kama vile magadi na chumvi ambazo wakati mwingine zinasababisha kuozesha bodi ya gari,” anasema na kuongeza:

“Magari hayo ni imara kutokana na aina ya kazi yanayofanya na yanatakiwa kufanyiwa matengenezo mara kwa mara ili yadumu.”
Changamoto kwa makandarasi
Mwenyekiti wa makandarasi wa kuzoa taka jijini hapa, Mathew Andrew, Januari 15, 2024 akizungumza kwenye mkutano mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila na watendaji wa Serikali kuhusu tahadhari dhidi ya magonjwa ya mlipuko, alisema miongoni mwa changamoto zao wanazokutana katika uzoaji taka ni kusimamishwa mara kwa mara na askari wa usalama barabarani.
“Tunaomba magari haya yaangaliwe kama ambulensi, yasibughudhiwe kwa kuwa kazi inayofanywa ni ya kutoa huduma ya afya kwa wananchi,” alisema.

Taka zikiwa zimewekwa pembeni ya barabara eneo la Magomeni jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga
Aliomba wapewe mikataba mirefu ya kufanya kazi ili iwe rahisi kwao kukopesheka na benki, hivyo kununua magari mengi zaidi kuliko ilivyo sasa.
Kwa mujibu wa taasisi ya kimataifa ya utunzaji mazingira ya Environmental Protection Agency (EPA), magari ya kubeba takataka yanapaswa kuwa ya daraja la juu, kama la saba au nane ili kubeba uzito mkubwa, mara nyingi kati ya pauni 10,000 (tani 4.5) hadi 40,000 (tani 18.1) au zaidi.
“Magari yanapaswa kuwa na vifaa kama vile mifumo ya kubana takataka, mikono ya otomatiki, na mabomba ya kuchota ili kuboresha ufanisi,” imesema tovuti ya EPA.
Taasisi hiyo imesema magari hayo yanapaswa kuwa na alama za kurudi nyuma, kamera na mwangaza wa kutosha ili kuhakikisha usalama wa operesheni, hasa katika maeneo ya mijini.
“Yanapaswa kutii viwango vya uzalishaji wa hewa ili kupunguza athari kwa mazingira, dereva anahitaji kuwa na leseni ya kuendesha gari kubwa na mafunzo maalumu kuhusu usimamizi wa takataka.

“Magari yanahitaji kuwa na utaratibu wa ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha yanafanya kazi kwa usalama na ufanisi, yanahitajika kuwa na bima inayofaa ili kufidia matukio yoyote yanayoweza kutokea, pia yanapaswa kufuata sheria za ndani, za kitaifa na za kimataifa zinazohusu usimamizi wa takataka,” inaeleza taarifa ya EPA.
Septemba 2021 Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitoa Mwongozo wa Udhibiti wa Taka Ngumu kwa Kutumia Dhana ya Punguza, Tumia Tena na Rejeleza ambao ulieleza hali mbaya ya magari ya kuzoa taka, huku ikiyataja kuwa chanzo cha uchafuzi.
“Hali ya usafirishaji wa taka nayo imekuwa si yakuridhisha katika maeneo mengi nchini. Vifaa vinavyotumika kusafirisha taka ikiwamo magari, trekta na vyombo vingine vimekuwa katika hali mbaya, hivyo kuruhusu taka kumwagika wakati wa kusafirisha na kuendelea kuchangia katika uchafuzi wa mazingira,” unaeleza mwongozo huo.
Ili kuondokana na kadhia ya magari mabovu, mwongozo unaeleza: “Dhana ya Punguza, Tumia Tena na Rejeleza inamaanisha kupunguza kiasi cha taka kinachozalishwa katika maeneo mbalimbali katika shughuli za kila siku na hatimaye kupunguza kiasi cha taka kinachosafirishwa kwenda dampo.”
Nyongeza na Mintanga Hunda