Dar es Salaam. Mchungaji Daud Nkuba, maarufu Komando Mashimo, amehukumiwa kifungo cha miaka miwili jela baada ya kupatikana na hatia katika makosa mawili, kuingia kijinai katika ardhi isiyo yake na kuharibu mali.
Katika hukumu hiyo Komando Mashimo pia ameamriwa kulipa fidia ya Sh5 milioni.
Komando Mashimo amehukumiwa kutumikia adhabu hiyo na Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, leo Jumanne, Machi 18, 2025, kutokana na kesi ya jinai iliyokuwa ikimkabili mahakamani hapo.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Ramadhani Rugemalira, aliyesikiliza kesi hiyo, baada ya kuridhika na ushahidi wa upande wa mashitaka umethibitisha mashitaka hayo bila kuacha mashaka yoyote.
Katika kesi hiyo Komando Mashimo alikuwa anakabiliwa na mashitaka matatu yakiwamo hayo mawili yaani kuingia kijinai na kuharibu mali pamoja na kutishia kufanya vurugu.
Katika shitaka la kwanza, Komando Mashimo Novemba 22, 2023, maeneo ya Mbezi Luis Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam, aliingia kwa jinai katika ardhi inayomilikiwa na Frola Mwashaa.
Katika shitaka la pili katika kipindi hicho kwa makusudi na kinyume cha sheria aliharibu ujenzi wa nyumba iliyoko maeneo ya Mbezi Luis ambayo ni mali ya Frola Mwashaa.
Katika shitaka la tatu Komando Mashimo alimtishia Ramson Vicent kwa vurugu.
Katika kesi hiyo upande wa mashitaka uliwaita mashahidi watano waliotoa ushahidi mahakamani hapo na kuwasilisha vielelezo viwili, huku Komando Mashimo akijitetea yeye mwenyewe na kuita mashahidi kadhaa.
Hata hivyo, Hakimu Rugemalira katika hukumu hiyo amesema kuwa upande wa mashitaka umethibitisha mashitaka hayo mawili, yaani ya kuingia kijinai na kuharibu mali na shitaka la tatu la kutishia kufanya vurugu halikuthibitishwa.
“Baada ya kupitia ushahidi wa upande wa mashitaka na wa utetezi, Mahakama hii imeridhika kuwa upande wa mashitaka umethibitisha, shitaka la kwanza la kuingia kijinai na la pili la kuharibu mali.
“Hivyo Mahakama hii inamtia hatiani mshtakiwa katika mashitaka hayo, kama alivyoshtakiwa,” amesema Hakimu Rugemalira.
Baada ya kumtia hatiani kabla ya kusomewa adhabu, mwendesha mashitaka, Wakili wa Serikali, Rhoda Kamungu, ameieleza Mahakama kuwa upande wa mashitaka hauna kumbukumbu za nyuma za jinai za mshtakiwa, lakini akaomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshtakiwa kama sheria inavyoelekeza.
Hata hivyo, kwa upande wake Komando Mashiko alipopewa nafasi ya kuomba shufaa (nafuu ya adhabu) ameiomba mahakama kumpunguzia adhabu akieleza ana familia inayomtegemea.
Hakimu Rugemalira baada ya kusikiliza pande zote katika hukumu hiyo amesema amezingatia maelezo ya shufaa ya mshtakiwa na upande wa mashitaka pamoja na msimamo wa sheria.
“Hivyo mshitakiwa kwa kosa la kuingia kwa jinai Mahakama inamuhukumu adhabu ya kwenda jela miezi sita, na kwa kosa la kuharibu mali mahakama hii inamuhukumu mshtakiwa adhabu ya kwenda jela miaka miwili na adhabu zote zinakwenda kwa pamoja.
“Pia utatakiwa kulipa fidia ya Sh5 milioni,” amesema Hakimu Rugemalira na kuongeza:
“Pia mahakama hii inakuachia huru kwa kosa la kutishia kwa vurugu kwa sababu upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha shitaka dhidi yako, hivyo utatumikia kifungo cha miaka miwili gerezani.”