Mitazamo tofauti sera mpya ya ardhi

Dar es Salaam.  Wakati Serikali ikizindua Sera ya Ardhi ya mwaka 1995 toleo la 2023, wadau wamesema angalau inaonesha matumaini katika kutatua migogoro ya ardhi, huku wakisisitiza Bunge kuharakisha marekebisho ya sheria ili ziendane na sera hiyo.

Mbali na matumaini hayo, wametilia shaka baadhi ya vipengele, kikiwamo kwenye sekta ya milki wakisema biashara ya kujenga nyumba za kupangisha na kuuzia wananchi ifanywe na Serikali badala ya wawekezaji kutoka nje.

Maoni hayo ya wadau yanakuja siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan, jana Jumatatu, Machi 17, 2025 jijini Dodoma kuzindua sera hiyo ikiwa na vipengele sita vinavyoitofautisha na ile ya awali.

Miongoni mwa vipengele hivyo ni kuimarishwa kwa mfuko wa fidia ili kurahisisha ulipaji kwa haki, wakati na thamani halisi, pamoja na kutoa ruhusa kwa wawekezaji kutoka nje kujenga nyumba na kupangishia au kuuzia Watanzania.

Pia, sera hiyo inaweka msisitizo wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kama nyenzo ya kupungua changamoto katika sekta ya ardhi.

Akizungumzia sera hiyo leo Jumanne, Machi 18, 2025, Mkurugenzi Mtendaji wa HakiArdhi, Cathbert Tomitho amesema miongoni mwa mambo yaliyokonga nyoyo za wadau ni sera hiyo kuweka ulinzi wa haki za ardhi za kimila ili kuwalinda wazalishaji wadogo kama wakulima na wafugaji.

Kwa kuwa sera hiyo inaelekeza mfumo wa utatuzi wa migogoro ya ardhi, alisema matarajio yake ni kuliona Bunge likirekebisha sheria za ardhi zitakazoweka msisitizo na mwongozo wa utekelezaji wa hilo.

“Kwenye hili natarajia Bunge litarekebisha sheria za ardhi ili alichokisema Rais Samia kuhusu usuluhishaji wa migogoro ndani ya sera kionekane,” amesema.

Sambamba na hilo, amesema anaona migogoro ya ardhi itapata suluhu kwa wakati na haki kutokana na sera hiyo kutambua umuhimu wa maboresho ya mabaraza ya ardhi kuanzia ngazi ya chini hadi juu.

“Mapitio ya mabaraza hayo ya ardhi, yatadhibiti utatuzi wa migogoro kwa njia ya matamko ya viongozi, badala yake kutakuwa na mfumo utakaoifanya kazi hiyo,” amesisitiza.

Katika hoja hiyo, Tomitho amesema ni imani yake, mfumo utakaowekwa utaruhusu pande zote zilizopo kwenye mgogoro husika kusikilizwa na uamuzi utatolewa kwa haki na usahihi.

Jambo lingine lililokidhi matarajio yake katika sera hiyo kwa mujibu wa Tomitho, ni kuonekana umuhimu wa kuanzishwa kwa Kamisheni ya Ardhi, itakayodhibiti biashara ya rasilimali hiyo na kuondoa uholela.

“Kubwa tunalolitarajia, hata kwenye uuzaji wa ardhi, sasa kuna watu wanakwenda kulindwa, kwa sababu unakuta baba ameuza ardhi, mama anasema sikushirikishwa, hili tunaamini linakwenda kusimamiwa kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa,” amesema.

Amesema sera hiyo pia, inaweka msisitizo wa kuwepo kwa vifaa na wataalamu wa kutosha, jambo litakaloondoa kisingizio kwa maofisa wa umma katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Sekta ya ardhi ikiwa na vifaa vya kutosha na hata wataalamu, kwanza unaondoa tabia ya maofisa au wataalamu kubabaika au kubabaishwa na rushwa zinazotolewa na mtu mmoja au kikundi cha watu wanaotaka kununua ardhi bila utaratibu.

“Katika halmashauri huko, mtu anapotaka kununua ardhi kwanza ataambiwa ofisa hana usafiri na hana nauli, kwa hiyo unapotaka huduma inabidi uinunue huduma unayoitaka ndiyo uhudumiwe,” amesema.

Pamoja na hayo, Tomitho alitilia shaka kipengele kinachotoa haki ya kumiliki ardhi kwa diaspora, akisema kwa kuwa walishaukana uraia, ni muhimu wapewe kwa masharti.

Kwa mtazamo wake, amesema diaspora anaweza kutumika na wageni kununua vipande vikubwa vya ardhi.

“Lazima tuweke vipengele vya kumdhibiti asije akawa dalali wa ardhi ya Tanzania kwa sababu yeye ni diaspora. Diaspora naye awekeze na hilo lifanywe wakati wa marekebisho ya sheria,” amesema.

Lingine alilotilia shaka ni katika sekta ya milki, akisema kwa kawaida sio watu wenye kipato duni watakaomudu kununua nyumba zitakazojengwa na hakuna mwekezaji atakayewekeza kwenye eneo lisilo na wateja wenye uwezo.

“Tunaweza kutengeneza soko ambalo wanunuzi ni watu matajiri tu, je, hawa wanaochukuliwa maeneo yao wanauza kwa bei rahisi watakuja kujenga lini. Biashara hii ingefanywa na Serikali ni sawa,” amesema.

Mratibu wa Jukwaa la Haki Ardhi Tanzania (TALA), Bernard Baha amesema kitendo cha kuzinduliwa kwa sera hiyo ni hatua moja mbele kwa wadau wa ardhi.

Hata hivyo, amesema tathmini kuhusu kiwango gani mapendekezo yao yamezingatiwa ndani ya sera husika itajulikana baada ya kikao cha wadau kinachotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Baha amesema, kuna namna sera hiyo itakuwa muarobaini wa migogoro ya ardhi kutokana na matumizi ya Teknolojia ya Habari ya Mawasiliano (Tehama) yaliyotajwa ndani yake.

“Sera haikulenga kutatua migogoro ya ardhi pekee, lakini hilo ni moja ya malengo yake na naona itafanikiwa hasa kupitia matumizi ya Tehama,” amesema.

Kuhusu maeneo mengine, amesema yatabainika baada ya wadau kukaa kufanya ulinganifu wa mapendekezo yao na kilichomo ndani ya sera husika.

Pamoja na hayo, amesema jambo lingine muhimu la kuangalia ni iwapo ndani ya sera hiyo kuna mpango mkakati wa kutenga bajeti ya utekelezaji.

“Kwa sababu sera ya zamani haikuwa na mpango mkakati wa utekelezaji na nafikiri ndio sababu ilikwama,” amesema.

Baha pia, amegusia changamoto ya suala la haki za wanawake katika usawa wa kumiliki ardhi, akidokeza kipengele kinachoipa nafasi mila bado hakijafutwa ndani ya sera hiyo.

“Kama hakijafutwa maana yake kuna kazi kubwa ya kufanya, kwa sababu kinatoa nafasi ya mambo hayo kuendelea kufanyika. Mtu akionewa atalazimika kwenda mahakamani ni wachache wenye uthubutu huo, wengi wataonewa,” amesema.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu Chuo Kikuu cha Ardhi, Profesa Evaristo Liwa amesema sera hiyo imehusisha mambo mengi aliyoyataja kuwa suluhu ya changamoto zilizopo katika sekta ya ardhi.

“Ndio naisoma sijamaliza, lakini nikirejea yaliyozungumzwa na Rais Samia kuna namna ndani ya sera kuna suluhu ya migogoro katika sekta ya ardhi,” amesema.

Kwa mujibu wa Profesa Liwa, jambo muhimu ni kuzingatiwa maelekezo yote ya sera kwa maofisa wa ardhi wanaoitekeleza, ili kila kilichomo ndani kiwe na matokeo.

“Rais anaonyesha ana matumaini na sera husika ndio maana ametoa maelekezo mbalimbali ikiwamo kwa maofisa ardhi, kama yatazingatiwa mambo yatakwenda vema,” amesema.

Related Posts