MVTTC YAISAIDIA SHULE KONGWE YA UFUNDI MSAMVU

 

 CHUO cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro,MVTTC, wameamua kuisaidia shule kongwe ya Ufundi ya Msamvu yenye wanafunzi wenye mahitaji maalum kukarabati karakana ya fani ya chuma na uchomeleaji ambayo Kwa muda mrefu ilikuwa chakavu sana sambamba na kurekebisha mfumo wa Umeme katika karakana hiyo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 ya Mamlaka ya Elimu ya Ufundi stadi VETA na miaka Hamsini ya mfumo wa kitaasisi wa elimu na mafunzo ya Ufundi stadi nchini Tanzania.

Katika maadhimisho hayo chuo hicho pia kimeweka mkakati wa kuongeza kiwango cha udahili wa wanafunzi walimu kutoka 500 wa mwaka huu kufikia wanafunzi 3100 ifikapo mwaka 2026 ili kwenda sambamba na mahitaji ya sasa ya walimu  wa amali nchini hasa baada ya Serikali kufanya maboresho ya mtaala ya kufundishia na kujifunzia kwa shule za msingi na sekondari.

Maboresho hayo yamewafanya wanafunzi wa msingi na Sekondari  sasa kujifunza mkondo wa Amali kwa kulenga kuwapatia zaidi ujuzi kwenye stadi mbalimbali za ufundi hivyo  mahitaji ya Walimu kwaajili ya kufundishia kuwa ni kipaumbele mashuleni.

Akizungumza wakati wa maadhimisho yaliyofanywa na MVTTC, Mkuu wa chuo hicho Samwel Kaali alisema baada ya upanuzi wa miundo mbinu ya chuo hicho cha ualimu wa ufundi ikiwemo mabweni na karakana wameongeza mtaala mipya 18 ili kwenda sambamba na mahitaji ya Soko.

Aidha akasema wameguswa kukarabati karakana Katika shule ya Ufundi ya Msamvu sambamba na kurekebisha mfumo wa Umeme baada ya kubaini mahitaji makubwa ambayo shule hiyo kongwe yenye wanafunzi 155 inakabiliwa nayo.

“Maadhimisho haya yanalenga kutambua mchango wa elimu na mafunzo ya ualimu wa ufundi Katika kuendeleza elimu na mafunzo ya Ufundi stadi nchini, Tunakarabati karakana hii kama sehemu ya shughuli za kujitolea Katika kusaidia kuboresha huduma za jamii,ukarabati utahusisha kuboresha mfumo wa umeme, kuezua paa la zamani na kuweka jipya, pamoja na kuweka sakafu ya zege”Alisema Mkuu huyo wa chuo cha MVTTC  kilicho chini ya VETA 

Aidha wamekabidhi vifaa na nyenzo za kujifunzia na kufundishia masomo ya Ufundi kwa Uongozi wa shule hiyo ili kusaidia masomo ya Ufundi stadi..

Baadhi ya wanafunzi waliosoma Katika shule hiyo mwaka 2022 akiwemo Husein Msagati walisema licha ya masomo waliyopata shuleni hapo kuwaonesha njia ya maisha hata kama bado hawajafanikiwa Sana,bado shule waliyowahi kusoma ina changamoto nyingi zinazohitaji kutatuliwa.

Msagati akasema Choo kilichopo wanalazimika kukifuata mbali na wanachangia na wanafunzi wa shule ya Msingi huku karakana moja iliyopo wakitumia kwa zamu kwa kusubiriana kwasababu haitoshelezi kwa fani zote za ufundi.

Kaimu Afisa Elimu ya Msingi Manispaa ya Morogoro, Amina Kova, Alisema shule hiyo inayotoa elimu Katika fani za chuma na uchomeleaji, sayansi kimu ikiwemo ushonaji na mapishi, Uashi na Umeme wa majumbani imekuwa na msaada mkubwa kwa vijana waliokosa elimu Katika mfumo Rasmi ambao kama wasingesaidika wangekuwa wamejiingiza kwenye vitendo viovu mtaani 

Akasema ujuzi wanaoupata wanafunzi hao watautumia kupata kipato kwani sekta ya Ufundi kwa sasa ina Ajira za kutosha zinazoonekana ikiwemo Ujenzi wa nyumba mpya, ununuzi wa magari,  sherehe zinazohitaji vyakula na mapambo, nguo zinashonwa hasa na kina mama kila siku nk.

MVTTC, Odiface Tarimo akizungumzia Sana zilizokabidhiwa Alisema zimebuniwa na wanafunzi wenyewe lengo likiwa kutengeneza uhalisia wa Kile wanafunzi watakachokwenda kufanyia kazi na kwamba Sana hizo zinaondoa changamoto ya gharama kubwa kununua vifaa halisia kwaajili ya kufundishia.

Mapema Mwalimu Mkuu wa shule ya Ufundi Msamvu Bi Lydia Molel licha ya kushukuru kwa msaada huo akasema umekuja kuwavisha nguo kwani mahitaji waliyo nayo kwenye miundo mbinu na vifaa bado ni makubwa sana.

Aidha akasema masomo ya Ufundi uashi yamewasaidia kupata kipato cha kuboresha baadhi ya Majengo ambayo ni chakavu hususani eneo ambalo sasa wanatumia kama ofisi ingawa bado Wana changamoto nyingi ikiwemo mahitaji ya vyoo na uchakavu wa Majengo mengine na uhaba wa karakana, jiko na Majengo mengine

Mwisho.

Related Posts