Okwi akubali yaishe Uganda, Aucho kubeba mikoba

Baada ya kuitumikia timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’ kwa zaidi ya miaka 15, nyota wa zamani wa Simba, Emmanuel Okwi ametangaza rasmi kustaafu kuitumikia timu hiyo.

Okwi mwenye umri wa miaka 32 ambaye kwa sasa anaichezea Kiyovu SC ya Rwanda, ametangaza uamuzi huo wa kustaafu leo, Machi 18, 2025kupitia taarifa aliyoiweka katika kurasa zake za mitandao ya kijamii.

“Kuiwakilisha nchi yangu kwenye jukwaa la kimataifa imekuwa ni kutimiza ndoto ambayo imekuwa kweli.. Kuvaa jezi za Uganda Cranes kila mara kuliacha hisia maalum na unahodha wa timu yetu ilikuwa ni fursa na heshima kubwa.

 Enzi mpya ya kusisimua kwa soka la Uganda inakuja katika nyakati ambayo Afrika Mashariki itaandaa CHAN, Agosti na baadaye AFCON 2027 huku wanasoka wengi chipukizi wakiibuka. Ndio maana, baada ya kuenzi kumbukumbu zote hizo, naamini ni wakati wa mimi kujiweka kando na kuwatengenezea njia chipukizi wetu wenye vipaji.

“Siku zote nitahifadhi moyoni mwangu upendo nilioonyeshwa na mashabiki wote na shukrani zangu za pekee ziende kwa familia yangu, Kocha Bobby Williamson ambaye alinipa fursa ya kucheza kwa mara ya kwanza, makocha wote waliofuata baada ya hapo ambao tuliunda nao kumbukumbu kwa pamoja katika hali ngumu na mbaya na bila shaka uongozi wa Shirikisho la Vyama vya Soka Uganda (FUFA). Wako Mwaminifu, Emmanuel Arnold Okwi,” ameandika Okwi.

Katika kipindi chote ambacho Okwi ameichezea Uganda tangu 2009 hadi sasa anapostaafu, mchezaji huyo amefunga mabao 28 katika michezo 95 ambayo ameichezea.

Okwi alikuwa miongoni mwa wachezaji walioiwakilisha Uganda katika fainali za mataifa ya Afrika (Afc on) 2019 zilizofanyika Misri ambapo alifumania nyavu mara mbili.

Kustaafu kwa Okwi hapana shaka kunafungua mlango kwa Khalid Aucho kuwa nahodha wa kudumu wa Uganda kwani kwa sasa, kiungo huyo wa Yanga amekuwa akikaimu nafasi hiyo.

Okwi alichukua kijiti cha unahodha wa Uganda kutoka kwa Kipa Denis Onyango ambaye alistaafu mwaka 2021.

Related Posts