REKODI alizoacha John Bocco pale Azam FC, zimemfanya Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’, kumtaja kuwa ndiye mchezaji bora wa muda wote ndani ya kikosi hicho.
Bocco ambaye aliichezea Azam kwa kipindi cha miaka 10 kuanzia 2007 ilipokuwa Ligi Daraja la Kwanza kisha kuipandisha Ligi Kuu Bara 2008 na kuondoka 2017, kwa sasa anaitumikia JKT Tanzania.
Kabla ya kutua JKT Tanzania, John Bocco mwenye umri wa miaka 35, alikuwa Simba aliyojiunga nayo 2017 wakati anatoka Azam.
Akizungumza na Mwanaspoti, Zaka Zakazi alisema hadi sasa Bocco ndiye mchezaji wake bora kwani rekodi na historia aliyoiacha kwenye klabu hiyo ni kubwa sana huku akibainisha kwamba mshambuliaji huyo ni mfano wa kuigwa kwa wazawa.
“Yeye ndiye aliyefunga mabao yaliyoipandisha timu daraja. Pia tulipocheza mechi ya kwanza Kombe la Mapinduzi aliyesababisha hilo ni Bocco.
“Wakati Azam FC inashinda ubingwa wa Ligi Kuu, Kombe la Kagame mfungaji alikuwa Bocco,” alisema Zaka Zakazi na kuongeza.
“Kwa sasa Azam haina ukaribu naye kwa sababu bado ni mchezaji wa timu nyingine, labda baadae huko akimaliza majukumu yake ingawa tunaheshimu mchango wake mkubwa kwa klabu yetu.”
Rekodi zinaonesha kuwa, wakati Azam ikishinda 2-0 dhidi ya Majimaji ya Songea katika mchezo uliowapandisha kushiriki Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza kutokea Kituo cha Dodoma, Bocco alifunga mabao yote.
Msimu wa 2013-2014, Bocco alikuwa sehemu ya kikosi cha Azam kilichobeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara chini ya Kocha Joseph Omog raia wa Cameroon bila ya kupoteza mechi.
Mwaka 2015, Azam ilibeba ubingwa wa Kombe la Kagame ikiichapa Gor Mahia mabao 2-0, bao la kwanza lilifungwa na Bocco, lingine Kipre Tchetche.
Kwa upande wa Kombe la Mapinduzi, Azam ndiyo timu kinara wa kubeba taji hilo ikilichukua mara tano 2012, 2013, 2016, 2017, 2018 huku kukiwa na mchango wa Bocco mara nne. Pia msimu wa 2011-2012 akiwa Azam, aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara akifunga mabao 19.