Sababu wanaume kuwa kinara wa mapishi hotelini

Mwanza. Yawezekana mara kadhaa umetembelea hoteli kubwa ndani na hata nje ya nchi na kukutana na wapishi wanaume.

Je, ulishawahi kujiuliza kwa nini wapishi wakuu kwenye hoteli kubwa wengi wao ni wanaume? Hata kwenye makundi ya kijamii ya wanawake wanaofanya kazi ya kupika kwenye shughuli mbalimbali ni lazima utakuta wamo wanaume miongoni mwao.

Tovuti maarufu kwa ajili ya kuchapisha na kushirikisha tafiti, makala za kisayansi, na matokeo ya utafiti ya ‘ResearchGate’ ilichapisha utafiti uliofanywa mwaka 2021 ulioangalia sababu za wapishi wakuu kwenye mahoteli kuwa wanaume (Why are the cook chefs always male).

Katika utafiti huo, ilibainika asilimia 98.5 ya wapishi wanaofanya kazi katika hoteli za nyota nne au tano ni wanaume huku wanawake wakiwa asilimia 1.5 pekee.

Utafiti huo uliojumuisha baadhi ya nchi za bara la Asia, Ulaya na Afrika kati ya hoteli 400 zilizofanyiwa utafiti, 394 zilikuwa na wapishi wanaume huku sita pekee zikiwa na wapishi wanawake.

Hata hivyo, wadau wa mapishi maeneo mbalimbali nchini wamesema sababu wanaume kuwa wapishi wakuu na wasimamizi wa jiko katika hoteli kubwa na hata vikundi vinavyopika na kusambaza vyakula, licha ya ukweli kwamba mwanamke ndiye mpishi na msimamizi wa jiko katika familia.

Mkazi wa jijini Mwanza, Neema Stanslaus amesema wanaume wengi wanakuwa wapishi hoteli kubwa kwa kuwa wanazingatia usafi ukiwemo wa nywele na kucha, hivyo kuhakikisha usalama wa chakula cha mteja.

“Nywele hawana hawajabandika kucha wala kope. Kucha siku zote zinabeba bakteria..hata rangi za kucha zikibanduka na kuingia kwenye chakula inakuwa hatari. Na hata nywele hasa kwa wanawake wanaoweka dawa zinaweza kutoka na kuingia kwenye chakula,” amesema Neema

Amesema hata kwenye kutunza muda wanaume wanaopika mahotelini au kusimamia majiko wapo vizuri, akieleza wakisema chakula hiki kitakuwa tayari ndani ya dakika tano na kweli ndani ya muda huo kitakuwa mezani.

“Kingine ni wabunifu….vyakula vingi duniani na hata viungo vya chakula wamebuni wanaume. Mfano wa vyakula maarufu ni ‘burger’ inasemekana ilibuniwa na Louis Lassen, licha wanawake wanaboresha lakini wanaume ni wabunifu.”

“Kwa ujumla, wanasimamia ubora wa chakula kilichotayarishwa ili kuhakikisha kinakidhi viwango kuanzia kwenye ladha, mwonekano na usafi ili mteja afurahie na kuridhika,”

Mkazi wa Ilemela, Daunson Martin amesema wanaume wengi ni wapishi  kwenye hoteli kubwa kwa sababu wamegeuza upishi kuwa taaluma na wanakwenda kusomea na kupata ujuzi, lakini wanawake wengi wanachukulia mazoea ya kujua kupika hata wasipoenda kuongeza ujuzi.

“Wanajua kupika wanaona kwenda tena kusomea ni kupoteza muda na kwamba hakuna ambacho hawakijui”amesema Martin

Naye, Cesilia Kasebele amesema ufanisi wa kazi ya kupika hotelini inahitaji mtu makini ambaye yupo tayari kutoa yote kwa ajili ya kazi yake na wanaume ni  rahisi sababu wenyewe hawapigii masuala ya uzazi ikiwemo kushika mimba, hivyo kwao ni rahisi kuwa makini tofauti ya wanawake.

“Sababu ya umakini inafanya wenye hoteli kupendelea kuwekeza kwa wapishi wa kiume badala ya wa kike sababu mwanamke ataolewa na kuzaa na kuacha kazi na mwenye hoteli ataona kapoteza muda wake wa kuwekeza,” amesema.

Mkazi wa Kaloleni jijini Arusha, Glory Lukumay amesema wanawake wengi ni wapishi wazuri ila wanaonekana kama wana majukumu mengi, hasa ya kifamilia na kuwafanya wengi kushindwa kupatikana au kushindwa kufanya kazi kwa wakati wote.

Mpishi na msambazaji wa chakula jijini Mwanza, Elizabeth Jackson alisema wanaume wanaaminika sana kwenye masuala yanayohusu kujenga afya ya mwili likiwemo la kusimamia na kupika chakula kizuri.

“Mwanamke anaweza kuwa anaandaa hapo chakula..mara kashika simu hatmaye chakula kinaungua na yeye yupo hapo hapo. Lakini, wanaume wapo makini. Huwezi kula hata wali alioupika yeye ukakutana hata na pumba au mchanga japo kwa hoteli kubwakubwa wanatumia mchele wenye viwango,” amesema.

Amesema kuwa, sababu nyingine ni uongozi wa jikoni au upishi unahitaji nguvu ya kimwili hasa kwenye mahoteli makubwa, uvumilivu wa kazi ngumu ambayo wenye sifa ya kufanya kazi ngumu ni wanaume.

“Kwa mfano, kwenye vikundi vya wapishi wa kwenye shughuli, kama kinachopikwa ni wali au ugali, basi utakuta chakula hicho kinapikwa kwenye chombo/sufuria yenye ujazo wa zaidi ya kilo 100 kwa wakati mmoja, kazi inayohitaji watu wenye nguvu/misuli ambao kiuhalisia ni wanaume,” amesema.

Mtaalamu wa mapishi jijini Arusha, Julius Athanas amesema asilimia kubwa ya wapishi duniani ni wanaume licha ya kuwa wanawake wengi ni wapishi wazuri, lakini ni wachache wanaoamua kwenda kusomea upishi akieleza mapishi na hasa ujuzi wake wanarithishana wao kwa wao bila kusoma.

Meneja wa hotel ya Goldcrest iliyopo jijini Mwanza, Dickson Ngereza amesema miongoni mwa sababu zinazowafanya wanaume wapishi kuwa wengi kwenye hoteli kubwa kubwa ni kumudu kufanya kazi ngumu.

“Huku kuna mikiki mikiki…kukimbizana sana. Unakuta kwa siku kuna conference (mkutano) yenye watu kati ya 400 hadi 500, wapishi wanaume wanaweza kumudu, lakini wanawake kusimamia jiko kinakuwa kipengele,” amesema

Ameongeza kuwa, baadhi ya waajiri wa mahoteli pia wanakwepa wapishi wanawake kutokana na likizo ya uzazi ambayo kikawaida mwanamke huichukua kwa kipindi cha miezi mitatu baada ya kujifungua.

Amesema ikitokea hivyo inawalazimu wamiliki au wasimamizi wa hoteli kutafuta mtu wa kushika nafasi ya mwanamke aliyeenda likizo ya uzazi na hivyo kuwa usumbufu kwa baadhi ya wamiliki.

Meneja wa Hoteli ya BBB jijini Mbeya, John Mwamilili amesema hakuna sababu kubwa zaidi ya mwanamume kuhimili mikikimikiki ya jikoni na kuzingatia usafi.

Amesema mara kadhaa akiwa mwanamke jikoni anapaswa kuwa imara, lakini inakuwa ngumu muda mwingi kukabiliwa na changamoto za hapa na pale.

Meneja wa moja ya hoteli ya kitalii ya nyota tano jijini Arusha (jina limehifadhiwa) amesema hoteli nyingi wapishi wakuu ni wanaume kwa sababu wanaamini utendaji kazi wao ni mkubwa na wapo makini.

Mkurugenzi wa Dodoma Hoteli iliyopo Jijini Dodoma, Wellington Malea amesema kuna sababu nyingi zinazosababisha kuwaajiri wapishi wanaume dhidi ya wanawake ikiwemo suala zima la afya.

Amesema wanaume wana uwezo mkubwa wa kuhimili moto na moshi wa jikoni kuliko wanawake ambao wana uwezo wa kuhimili kwa muda mfupi tu.

Malea amesema pia wanaume wana uwezo wa kufanya kazi nyingi  kwa haraka na kwa ufanisi kuliko wanawake ,hivyo wapishi wanaume ni chaguo la kwanza kuliko wanawake.

Mkurugenzi huyo amesema pia maumbile ya wanaume hayabadiliki kama ilivyo kwa wanawake kwa sababu mwanamke akifikisha umri wa miaka 30 hafanani tena na alivyokuwa na umri wa miaka 25, lakini wanaume wana uwezo wa kuwa na umbo lilelile mpaka anazeeka hata kama atakuwa na umri mkubwa.

“Kwa hiyo suala la kuwaajiri wapishi wanaume badala ya wanawake ni la uwekezaji ukiwekeza kwa wanaume wanafanya kazi muda mrefu kuliko mwanamke kwa sababu ya kiafya, kimaumbile na nguvu za kufanya kazi hiyo, kwa sababu mwanaume anaweza kupika akiwa amesimama kwa muda wa saa nane mfululizo kitu ambacho mwanamke hawezi.

Imeandikwa na Saada Amir (Mwanza), Janeth Mushi (Arusha) na Sadam Sadick (Mbeya), Rachel Chibwete (Dodoma).

Related Posts