TBS yabaini matumizi holela ya bidhaa za vilevi

Dodoma. Shirika la Viwango Tanzania (TBS), limefanya tathimini ya vileo sokoni na kubaini changamoto kubwa ipo katika matumizi holela bidhaa.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk Ashura Katunzi leo Machi 18,2025 alipokuwa akizungumzia mafanikio ya miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita na mwelekeo wa shirika hilo.

Amesema shirika hilo limechukua hatua nyingi mahususi katika kukabiliana na bidhaa za vinywaji vya vilevi ambapo mwaka 2023/24 walinunua kutoka sokoni bidhaa mbalimbali na kuzipima ubora.

“Katika zile bidhaa nyingi zilikuwa na ubora unaostahili lakini chache tu zilikuwa na changamoto, unakuta kwa mfano kinywaji kinatakiwa kiwe na asilimia 45 unakuta kina asilimia 40. Ina maana mlaji amepunjwa kile kiwango cha kilevi,”amesema.

Dk Katunzi amesema kinywaji kilicho na chini ya kilevi kinachotakiwa kinakuwa hakina ubora na hivyo waliviondoa sokoni.

Amesema kwa tathimini hiyo imeonyesha kuwa bidhaa hizo zilikuwa na ubora unaostahili, lakini mapungufu yalikuwa katika kiwango cha ulevi na taarifa chache za kifungashio hazikuwa zinafikiwa.

Dk Katunzi amesema kwa kushirikiana na kitengo ambacho kinakagua vihatarishi sokoni katika mwaka 2025 walienda sokoni ambapo watu karibu 400 walihojiwa, kuangalia vinywaji vilivyoko sokoni na kuangalia changamoto ni nini.

“Kitu kikubwa ambacho tumekiona sokoni kuna kiwango kikubwa cha matumizi holela ya vilevi, si kwamba bidhaa hazina ubora, ni chache tu hazina ubora lakini changamoto kubwa ni matumizi yasiyo salama ya vilevi.”

“Unakuta mtu anakunywa isivyostahili, unakuta kilevi kile kinatakiwa kuchanganywa na kingine, yeye anakunywa kikavu kavu. Lakini pia zinanywewa nyingi,”amesema.

Amesema wamechukua hatua kwa kuwashirikisha Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kuangalia ni namna gani watawezesha vilevi kupatikana katika mazingira salama na unywaji salama zaidi.

Dk Katunzi ametaka kuendelea kutolewa kwa elimu kwa umma kuhusu matumizi salama ya vinywaji kwa kuwa watu wanatumia kupitiliza na vinapatikana kwa urahisi (bei ndogo).

Machi mwaka 2017, Serikali ilipiga marufuku matumizi ya pakiti za plastiki kufungashia pombe kali, maarufu viroba, kuzuia matumizi holela ambayo ilisababisha hata vijana wadogo kumudu bei.

Hata hivyo, wauzaji wamekuja kwa namna nyingine ambapo hupima na kuuza vinywaji hivyo kwa kupima kiasi kidogo ambapo kuna kinachouzwa  kuanzia Sh500, Sh1,000 na Sh2,000.

Mkazi wa Dodoma Mjini, Janeth Mazengo amesema changamoto hiyo imekuwa ni kubwa kwani vinywaji, hivyo vimekuwa vikiuzwa hata katika maduka ya vyakula mtaani ambayo hayana leseni za kuuza vilevi.

“Siku hizi vijana hata hawapati tabu ya kuvifuata baa, wakizunguka mtaani katika maduka ya vyakula wanavikuta tena kwa bei rahisi, mapema unakuta mtu ameshalewa, unashangaa anafanya kazi muda gani,”amesema.

Dk Katunzi amesema katika kipindi cha kati ya Julai hadi Desemba mwaka jana, walibaini bidhaa zenye thamani ya Sh1.5 bilioni zilizokuwa hazina ubora na hivyo kuziondoa sokoni.

Kuhusu bidhaa zilizothibitishwa, amesema jumla ya bidhaa 2,402 zilithibitishwa ubora na hivyo ziko sokoni katika miaka minne, huku 1,066 sawa na asilimia 44 zikiwa ni zinazozalishwa na wajasiriamali wadogo.

Aidha, Dk Katunzi amesema Sh350 milioni zinatengwa kila mwaka kwa ajili ya kuwahudumia wajasiriamali wadogo ili kuthibitisha bidhaa zao.

Pia, amesema wameweza kupima sampuli ya bidhaa 118,059 katika kipindi cha miaka minne.

Related Posts