Wakazi Dar waeleza walivyohenyeka kusaka maji

Dar es Salaam. Wakazi wa eneo la Dar es Salaam ya Kusini ikiwemo Bangulo, Kifuru wamesimulia namna walivyosumbuka kupata maji safi kwa muda mrefu, huku ikiwalazimu kujihimu kutafuta huduma hiyo maeneo ya jirani.

Wameyaanika hayo walipozungumza na Mwananchi kwenye ziara ya Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, iliyofanyika leo Jumanne Machi 18, 2025 kwenye mradi wa maji wa Bangulo uliopo Kata ya Pugu Station wilayani Ilala.

“Tumekuwa tukinunua maji yanayokuja kuuzwa na wafanyabiashara kwa bei ya maumivu,” amesema Hairat Bakari, mkazi wa Bangulo Mlimani.

Hairat ambaye ameanza kuishi mtaa huo mwaka 2016 amesema wameteseka kwani huduma ya maji ni muhimu na pale inapokosekana inaleta changamoto.

Said Msangi amesema hana kisima hivyo inamlazimu kutumia maji ya kununua kwa bei ya juu.

“Kama huna vyombo vya kutosha basi utakiona cha moto, maana ukishayakosa basi yanakaa muda hadi kuyapata tena,” amesema.

Mariam Msemwa aliyeanza kuishi mtaa wa Bangulo Mlimani mwaka 2008, amesema amekuwa akidamka na mume pamoja na familia yake kutafuta maji ambayo hata hivyo ni ya chumvi.

“Tunanunua dumu moja la lita 1,000 kwa Sh17, 000 wakati mwingine hatuna hela basi ni matatizo, lakini mradi huu tunatumaini umeanza majaribio tutapata maji,” ameeleza.

Maneno yake yanashabihiana na Halima Muddy ambaye ana miaka miwili akiishi eneo hilo ambaye amedai wamekuwa wakitumia maji ya chumvi yanayotoka kwenye visima kwa kuwa hawana budi.

Baadhi ya wakati wa Kifuru, wakiwamo Jonia Peter, Rafael Isdol, Nuru Msidala na Leonard Nyika wamesema kwa sasa maji yanatoka ukilinganisha na kuanzia Novemba 2024, ambapo yalikuwa hayatoki kwa uhakika.

Matumaini ya wakazi hayo yanabebwa na mradi huo wa Bangulo uliogharimu Sh36.8 bilioni utakaohudumia wakazi zaidi ya 450,000 ambapo kuna tenki kubwa la kuhifadhi maji lenye ujazi wa lita milioni tisa na ulazaji wa mtandao wa mabomba wenye Kilomita 108.

Akizungumza katika ziara hiyo, Aweso amesisitiza umuhimu wa kutunza miundombinu katika kipindi hiki ambacho mamlaka inaendelea na mchakato wa kuwaunganishia wananchi huduma hiyo.

Katika kusisitiza hilo ameonya watendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), kutowabambikia wananchi bili za maji sambamba na kuwaomba rushwa kuwaunganishia huduma hiyo muhimu.

Akitolea mfamo amesema ankara ikiwa Sh15,000 alipe hiyohiyo sio unamwambia alipe Sh150,000. Aidha amerejea suala la kubadili uelekeo wa mita za maji akisema sasa zinakuja mita za malipo ya kabla kama za luku,  kama ilivyoagizwa na Rais Samia Suluhu Hassan alipokuwa ziarani mkoani Tanga.

Katika ziara hiyo Aweso ameambatana na Katibu Mkuu Wizara hiyo, Mwajuma Waziri watendaji wa Dawasa pamoja na waandishi wa habari. Mradi huo  kwa sasa upo kwenye majaribio ingawa wananchi wanaendelea kupata maji wakati wakisubiri kuanza rasmi hapo Aprili 2025.

“Pia, mwananchi akiomba kuunganishiwa maji akilipa aunganishiwe ndani ya siku saba. Sitarajii na sitegemei watu kuunganishiwa maji.

“Sio mtu anaomba kuunganishiwa maji anaambiwa aje kesho sijui keshokutwa hadi atoe kitu kidogo, mara amuone fulani sitaki kusikia. Pia, marufuku kwa msoma mita au mtu mwingine kukata maji mwisho wa juma au siku ya sikukuu kwa sababu ni muda wa mapumziko.”

Awali, Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Mkama Bwire amesema mradi utahudumia maeneo  ya Ukonga, Kisarawe, Ubungo, Temeke na Segerea.

Akitaja baadhi ya maeneo amesema utafika katika eneo la Kinyerezi, Bonyokwa, Kipawa, Kipunguni, Kitunda, Saranga, Misigani, Buza na Yombo.

“Kwa sasa tupo kwenye majaribio ingawa maji tayari yanatoka lakini utaanza rasmi Aprili. Mradi umeenda kwa wakati tunashukuru. Wananchi wanapata maji safi ya Dawasa,” amesema.

Amesema kuna takriban kilomita 10.8 kutoka Kibamba ambapo maji hayo yanasukumwa kwa pampu kutoka Ruvu. Kwa sasa wanaendelea kubadilisha mtandao wa zamani.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri amesema katika kipindi hiki cha maadhimisho ya wiki ya maji amesisitiza watu kutunza miundombinu ili wapate huduma iliyo bora.

Related Posts