Mwanza. Watoto 641 wamefanyiwa ukatili wa kijinsia kwa kipindi cha miezi tisa kuanzia Oktoba, 2023 hadi Juni, 2024 katika Wilaya za Nyamagana na Ilemela mkoani Mwanza.
Akifungua mafunzo ya ulinzi wa mtoto na ukatili wa kijinsia awamu ya nne yanayoratibiwa na Shirika la Plan International leo Jumanne Machi 18, 2025 kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa, Mkuu wa Polisi Jamii mkoani humo, Lwelwe Mpina amesema kati yao, watoto wa kike walikuwa 466 na wa kiume 175.
“Kesi 641 za ukatili dhidi ya mtoto ziliripotiwa vituo vya polisi vya Wilaya za Nyamagana na Ilemela kwa kipindi cha Oktoba 2013 hadi Juni, 2024,” amesema.
Mpina amesema katika kipindi hicho, pia kesi 287 za ukatili wa kijinsia ziliripotiwa katika vituo vya polisi vya wilaya hizo, ambapo wanawake waliofanyiwa ukatili walikuwa 252 na wanaume wakiwa 35.
Ameitaka jamii kuendelea kutoa taarifa za ukatili kwa watoto pamoja na kushiriki kutoa maelezo na ushahidi, utakaowezesha kukamatwa na kushtakiwa watu wote wanaokiuka au kuvunja haki za watoto.
“Kila mtu ana haki ya kulindwa na polisi dhidi ya unyanyasaji, unyonywaji, ubaguzi au matendo yoyote yanayovunja sheria za nchi, lakini ili lengo hilo litekelezwe kwa viwango vinavyotakiwa panahitajika ushirikiano wa pande mbili, yaani polisi na kila mmoja katika jamii,“ amesema.
Hata hivyo, amesema bado kuna changamoto ya uelewa mdogo kwa baadhi ya askari polisi juu ya haki za mtoto, sheria ya mtoto ya mwaka 2009 na Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Kuzuia na Kutokomeza Ukatili dhidi ya wanawake na watoto (MTAKUWWA), hivyo kujikuta wakiingia kwenye migogoro na jamii hasa katika kulinda haki za mtoto pindi anapokuwa ametendewa ukatili au ametenda kosa.
“Niwaombe nyote mliopata nafasi hii ya kushiriki katika mafunzo haya, mshiriki ipasavyo ili tukimaliza tukawatumikie wananchi kwa haki na usawa,”amesema.
Meneja wa Shirika la Plan International, Majani Rwambali amesema mafunzo hayo ya siku tatu ambayo ni utekelezaji wa mradi wa Vijana, Elimu, Malezi na Ajira (Vema) ni kwa ajili ya usimamizi wa kesi za watoto kwa maofisa ustawi wa jamii, mahakimu, madaktari pamoja na askari wa Jeshi la Polisi mkoani Mwanza.
“Haya mafunzo ni muhimu sana kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watoto na Taifa letu kwa ujumla.
“Jeshi la Polisi na Mahakama zetu ni kiungo muhimu sana katika kudumisha usalama wa raia na mali zao… suala la kupinga ukatili na kesi za watoto…hawawezi kuachwa nyuma kwa namna yoyote ile,” amesema.
Amesema mafunzo hayo yataimarisha ushirikiano kati ya makundi hayo na wananchi pamoja na kuimarisha mbinu za kutambua, kupokea na kushughulikia matukio ya vitendo vya ukatili kwa watoto.
Naye, Ofisa Ustawi Jiji la Mwanza, Edith Ngowi amesema jamii iendelee kupokea elimu ili kudhibiti ukatili wa kijinsia kwa makundi yote lakini ifanyiwe kazi.
“Tunaamini kwamba masuala mazima ya ulinzi wa watoto yanaanzia kwenye familia kwa hiyo ziendelee kumlinda mtoto na kuepuka ukatili… kila mmoja atimize wajibu wake,” ameongeza.