100 wanaswa wizi wa miundombinu ya maji, wananchi wawekewa dau

Mbeya. Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Mbeya (Mbeya UWSA) imesema imewakamata zaidi ya watu 100, kwa wizi wa maji na uhujumu wa miundombinu ya huduma hiyo.

Miongoni mwa watuhumiwa hao wamo waliofikishwa mahakamani na kuhukumiwa vifungo vya mwaka mmoja jela, huku wengine wakilipa faini hadi kufikia zaidi ya Sh300 milioni, huku ikitangazwa dau la Sh1 milioni kwa wananchi watakaofichua wahalifu wengine.

Akizungumza leo Machi 19, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo, Gilbert Kayange amesema ukamataji huo umefanyika kwa kipindi cha miezi miwili kuanzia Januari na Februali, mwaka huu.

Kayange amesema wataendelea kuchukua hatua kali kwa wanaohujumu miundombinu ya maji na mali nyingine za Serikali.

Pia, amesema baadhi ya wananchi wamekatiwa huduma ya maji kutokana na kushindwa kutimiza wajibu wao wa kulipa bili za maji, akieleza kuwa hadi sasa mamlaka hiyo inadai takribani Sh900 milioni.

“Suala la maji halina mbadala kwa kuwa linamgusa maisha ya kila mmoja, huduma kama hii yenye thamani ingepewa nafasi kuwa ya kwanza kwa kila mmoja kulipa kipaumbele, wananchi walinde miundombinu yake,” amesema Kayange.

Kayange amesema Mbeya UWSA itaendelea kufanya operesheni za mara kwa mara, kila eneo kuhakikisha wezi na wahujumu wa miundombinu ya maji wanakamatwa na kwamba watahakikisha, huku akieleza changamoto nyingine ya wizi wa chemba za majitaka na wizi wa maji kwenye dira.

Mmoja wa wananchi, Fusta Suleman amesema mamlaka hiyo imeonesha utendaji kazi, akieleza kuwa wananchi wanapaswa kuonesha uzalendo katika kulinda na kutunza miundombinu.

“Maji ndio huduma pekee inayomfanya mtu kuishi, tuwe wazalendo wa nchi yetu, hii idadi ya waliokamatwa inashtua sana, muda mwingine badala ya kulaumu Serikali tujitathimini wenyewe” amesema Fausta.

Naye George Mwasa amesema wananchi wanapaswa kupewa elimu kuhusu umuhimu wa utunzaji wa miundombinu, lakini akishauri kila mwananchi kutanguliza uzalendo katika miradi ya serikali.

“Tumeona mamlaka inavyojitahidi kubuni vyanzo vya maji hadi kufikia 29, hii yote ni katika kumsaidia mwananchi kuondokana na kero ya maji, hivyo inapotokea hujuma kama hizi inafifisha nguvu na ufanisi,” amesema Mwasa.

Related Posts