Askofu Rweyongeza atema nyongo kwenye jubilei

Mwanza. Kanisa Katoliki limeitaka Serikali kuheshimu fani  ya ualimu na kurejesha hadhi yake ikiwamo walimu kulipwa mshahara unaolingana na wabunge na mawaziri au zaidi pamoja na kuwaondolea kikokotoo.

Akizungumza leo Jumatano Machi 19, 2025 kwenye Jubilei ya miaka 25 ya Uaskofu wa Askofu Methodius Kilaini na miaka 53 ya upadri iliyofanyika Bukoba mkoani Kagera, Askofu  wa Jimbo Katoliki Kayanga, Almachius Rweyongeza, pia ameitaka Serikali kutonyanyapaa kada hiyo kwa kuwa ikichezewa taifa litaangamia.

Askofu Rweyongeza amesema hata Mungu alionya watu wake kupitia kinywa cha Nabii Oseah akisema watu wake wameangamia kwa kukosa maarifa.

 “Juzi nilikutana na vijana wawili nikaweza kudaka mazungumzo yao mmoja akawa anamuuliza mwenzake je umepata ajira, mwenzake alijibu sijapata sasa huu ni mwaka wa nane, huyo rafiki yake akadakia kwa mshangao wewe umekosa ajira kabisa kabisa hata ajira ya ualimu?

“Ajira ya ualimu umekosa? Akamcheka sana akiwa na maana kwamba, ualimu ni ajira ya walioshinda siyo wito. Fani ya ualimu iheshimiwe na Serikali isinyanyapaliwe irudishiwe hadhi yake,” amesema Askofu Rweyongeza.

Ameieleza Serikali ikumbuke mwalimu ndiye komandoo wa adui mjinga, asipoangaliwa vizuri, atashindwa vita ya kumshinda adui huyo na nchi itaendelea kuliwa na mataifa mengi, akieleza hata wahenga wamesema wajinga ndiyo waliwao.

Askofu Rweyongeza  amesema mwalimu  hasa wa shule za awali na msingi akiwa amepata ushindi wa alama za juu kabisa, alipwe mshahara unaolingana au kuzidi wa wabunge na mawaziri.

Askofu huyo ameomba walimu na watumishi wa chini kuondolewa  kikokotoo ili wachape kazi kwa amani, lakini pia wakati Serikali ikiendelea na utekelezaji wa sera ya ualimu, iruhusu shule binafsi ziwe na mitalaa ya kimataifa kupanua wigo.

Pia, ameomba shule ziingie ubia na shule binafsi za nje ya nchi au za kimataifa ili kurahisisha Watanzania kusaka ajira nje ya nchi.

“Mimi naunga mkono mia kwa mia sera mpya ya elimu ya kusoma hadi darasa la kumi pamoja na amali, lakini naomba sera hii isimbane tu mtoto wa mkulima na mpigakura wakati mtoto wa mheshimiwa mbunge aliyepitisha sera hiyo akaenda kusomea nje ya nchi huko Marekani, Ulaya,  Uchina akisomea mshahara wake mnene, malupulupu na kiinua mgongo ambavyo hakina kikokotoo,”amesema Askofu Rweyongeza.

Kuhusu, umaskini Askofu Rweyongeza amesema hayati Mwalimu Julius  Nyerere alifundisha fedha sio msingi wa maendeleo na ili nchi iendelee inahitaji  watu, ardhi safi na uongozi bora lakini Tanzania ya leo mikopo na misaada imekuwa ni msingi wa maendeleo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na Maaskofu Katoliki baada ya Ibada ya Jubilei ya  Miaka 25 ya Uaskofu wa Askofu Msaidizi Mstaafu Method Kilaini kwenye Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki la Bukoba, Machi 19, 2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

“Siku moja niliota ndoto, raia fulani mwenye cheo cha ukatibu kata, alikuwa na uchungu mkubwa, akakemea na kusema acheni mikopo, Taifa linauzwa baada ya kusema hayo akanyang’anywa ofisi, baiskeli yake na kutishiwa; ukiendelea na kidomo domo tutakuja kufyeka shamba lako la mahindi na mchicha,”amesema.

Askofu Rweyongeza amesema wananchi kunyang’anywa ardhi na kupewa wawekezaji akitolea mfano kwa ajili ya kilimo, huku akiuliza je wananchi wa eneo hilo wananufaikaje?

Ametolea mfano Mkoa wa Kagera ambao licha ya kuwa na Kiwanda cha Sukari cha Kagera, wananunua sukari bei juu ingawa kuna mashamba ya miwa na viwanda vya sukari.

Akizungumzia utawala bora amedai: “Sheria zinazopitishwa bungeni kwa wingi wa makelele ya ndiyo, badala ya kupiga  kura ya siri zinazowaingiza bungeni. Msemaji mmoja alikuwa anasema nyuma ya matendo hayo, kuna fundi mitambo ikiwa wanaosema hapana ni wengi atapunguza sauti, ikiwa wanaosema ndiyo ni wachache fundi mitambo anaongeza sauti…hiyo ni siasa safi?,”

Amedai kuwa, hata kupata viongozi ni kwa kuchanganya na kujumuisha kura halali, isiyo halali na haramu na kutangaza mshindi hata kama hapendwi na wananchi njia ambayo siyo ya kupata viongozi bora.

Amesema wanaokuwa viongozi kwa kuiba kura, kuhonga na kuwapoteza wapinzani, sio uongozi bora na Taifa haliwezi kumshinda adui kwa wananchi kushinda baa na kukesha kwenye starehe.

Kwa upande wa afya, Askofu Rweyongeza amehoji hadi lini Serikali itategemea chanjo na dawa kutoka nje, hasa katika kipindi hiki Rais wa Marekani, Donald Trump kusitisha msaada ya USAIDS, akihoji imejipangaje kukabiliana na maradhi.

Katika hatua nyingine, Askofu Rweyongeza  amewataka wananchi kuacha alama moyoni kwa watu inayogusa nyoyo za wengine na kuwaachia tabasamu, kwa kuwa watawaombea baraka badala ya kuacha mali nyingi ambazo wakifariki dunia wanakufa nazo.

Akizungumzia Askofu Kilaini, amesema ameacha alama zaidi ya moja akitaja baadhi  alikarabati Shule ya Msingi Kilaini  nyumbani kwake na kujenga nyumba za walimu, alitumia zawadi yake ya pesa aliyopewa kumnunulia kiti mwendo mtoto mlemavu na kumuasili kama mtoto wake na sasa huyo yupo kidato cha tatu.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akishiriki katika Ibada ya Jubilei ya  Miaka 25 ya Uaskofu wa Askofu Msaidizi Mstaafu Method Kilaini kwenye Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki la Bukoba, Machi 19, 2025. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatuma Mwasa. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki Mpanda, Eusebius Nzigilwa amesema maisha ya Askofu Kilaini ya kanisa yalikuwa baraka na neema kwa kuwa alikuwa baba, kaka, mwalimu, rafiki na mchungaji mwema akiwaongoza kwa imani na upendo waumini aliokabidhiwa na kugusa nyoyo za wengi.

Amemshukuru kwa huduma aliyoitoa TEC, akisema amejitolea katika baraza hilo ikiwamo kufundisha katika seminari kuu, kuwa Katibu Mkuu TEC kwa vipindi vitatu, mwenyekiti wa idara ya fedha ya baraza hilo kwa vipindi vitatu na hadi anastaafu, alikuwa mwenyekiti wa idara ya rasilimali watu akihusika kwa karibu katika mchakato wa upatikanaji wa watendaji muhimu katika baraza na taasisi zake.

Akijibu baadhi ya hoja zilizotolewa na kwenye jubilei hiyo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kupokea na kufanyia kazi ushauri wa wadau wakiwamo viongozi wa dini na ndiyo sababu imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa.

Pia, amesema itaendelea kuimarisha utoaji wa huduma za jamii kwa kusogeza karibu na wananchi na kuboresha upatikanaji wake.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika  Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu wa Askofu Msaidizi Mstaafu Method Kilaini kwenye Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki la Bukoba, Machi 19, 2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Amesema Februari na Machi, mwaka huu Serikali imeendelea na mapitio ya sera mbalimbali kwa lengo la kufanya maboresho kutokana na ushauri iliopata kwa wadau wakiwamo viongozi wa dini ili kuboresha utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Serikali vilevile inaendelea kuimarisha mkakati wa upatikanaji wa huduma mbalimbali zikiwamo za maendeleo zinazowagusa wananchi kwenye maeneo yao na Serikali itaendelea kuheshimu mikataba na makubaliano ya kimataifa kwa lengo la kukidhi matakwa ya mikataba hiyo huku tukifanya jitihada za kusimamia matakwa ya ndani ya nchi.

“Niwahakikishie Watanzania wenzangu kuwa, hakuna mwananchi atakosa huduma tunapoendelea kufanya maboresho ya huduma zetu,” amesema Waziri Mkuu.

Ibada hiyo imehudhuriwa na maaskofu wastaafu watano akiwamo  Kardinali Polycarp Pengo, Askofu Josephat Lebulu, Askofu Paulo Ruzoka, Askofu Damian Kyaruzi na Askofu Desiderius Rwoma.

Related Posts