Kupitia ziara hiyo, wajumbe wa Bodi walioshiriki akiwemo Mwenyekiti, Bw. Halfani Halfani walitembelea miundombinu ya kuzalisha na kuchakata gesi asilia inayoendeshwa na Kampuni ya PanAfrican Energy Tanzania Ltd (PAET) na mitambo ya kuchakata gesi asilia inayoendeshwa na GASCO ambayo ni kampuni tanzu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Akizungumza katika ziara hiyo, Bw. Halfani ameeleza kuwa kwa sasa kuna ongezeko la jitihada zinazowekwa na TPDC na PAET katika kutekeleza miradi ya CSR tofauti na hali ilivyokuwa awali. Katika hili, Bw. Halfani aliishukuru Serikali kwa kuhimiza suala la CSR kupitia ufuatiliaji thabiti na miongozo iliyoandaliwa kwa mujibu wa Sheria ya Petroli ya mwaka 2015.
“Mimi ni mmoja wa watu ambao tulikuja Songo Songo enzi hizo. Tunafarijika kuona wamejenga shule ya msingi, shule ya sekondari na wamejenga bweni la wasichana, shule ya awali, na leo tumeona wamejenga kituo cha afya kikubwa tu, na walikuwa wakilipia ada wanafunzi wa kike waliokwenda kusoma Kilwa, tunafarijika kwamba miaka 20 baadae wanafunzi wa Songo Songo wanaweza kupata elimu hizi zote kama faida mojawapo ya kuwepo kwa mradi huu wa gesi asilia hapa” alisema Halfani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa PURA Mhandisi Charles Sangweni amesema ziara imelenga kuongeza uelewa kwa Wajumbe wa Bodi kwani kwa kufanya hivyo kutawawezesha kufahamu mambo kwa uhalisia wake na kuyatolea maamuzi.
“Sisi kama PURA, moja ya shughuli zetu ni kusimamia shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi nchini, na kusimamia uzalishaji, na ili kujenga ufahamu kwa watendaji pamoja na Wakurugenzi wa Bodi, huwa tunafanya ziara hizi mara kwa mara, ziara hii ni muhimu kwa sababu imehusisha Wajumbe wa Bodi lengo ni kuwawezesha kuona uhalisia wa shughuli zinazoendelea ambazo huwa wanazijadili na kuzitolea maamuzi na ushauri mara kwa mara” amesema Mhandisi Sangweni.
Akitoa neno katika ziara hiyo, Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya PURA Mhandisi Hamdun Mansur amesema ziara hiyo imewafundisha mambo mengi ya uchakataji wa gesi asilia, na kuwataka PURA kuendelea kusimamia majukumu yao ipasavyo.
Mwenyekiti na baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya PURA wakikagua miradi ya Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR) inayotekelezwa kisiwani Songo Songo na kampuni zinazofanya shughuli za utafutaji na uzalishaji wa gesi asilia katika eneo hilo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya PURA, Bw. Halfani Halfani (katikati) na baadhi ya wajumbe wa Bodi wakisikiliza maelezo toka kwa mtaalamu wakati wa ziara ya Bodi hiyo katika mitambo ya kuzalisha na kuchakata gesi asilia iliyopo Songo Songo Mkoani Lindi.