Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetangaza kuanza kampeni yake ya No Reform No Election’ kwa kufanya mikutano ya nchi nzima, ikiwa ni siku moja baada kueleza dhana hiyo kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
Lengo la kampeni hiyo ni kupeleka elimu kwa wananchi ya kuishinikiza Serikali kufanya mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi, vinginevyo uchaguzi usifanyike.
Uamuzi huo ulipitishwa Desemba 2024 na Kamati Kuu ya chama hicho, kabla ya msimamo huo kuthibitishwa na Mkutano Mkuu Januari 21, 2025.
Wakiwa katika maandalizi ya ziara hiyo, viongozi wakuu wa Chadema jana Jumanne Machi 18, 2025 waliitikia wito wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, iliyowataka kufafanua ajenda hiyo, kwa muktadha wa Sheria ya Vyama vya Siasa.
Baada ya mkutano, John Mnyika, katibu mkuu wa Chadema aliyeongoza ujumbe huo, licha ya kusema bado kuna mambo mengine zaidi yanahitaji kuzungumzwa baina ya chama hicho na Ofisi ya Msajili, wao wanaendelea na ratiba zao kama kawaida kuhakikisha ‘no reform no election’ inatekelezeka.
“Hivi karibuni tutawatangazia ziara ya kuanza kwa mikutano ya hadhara katika maeneo mbalimbali ya nchi ili kuzungumza na Watanzania kuhusu no reform no election na mustakabali wa nchi,” alisema Mnyika jana Machi 18, 2024.
Siku moja baada ya kauli hiyo, leo Jumatano, Machi 19, 2025, Naibu Katibu Mkuu wa cha chama hicho Bara, Aman Golugwa amewaeleza waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa ziara hiyo itaanza Machi 23, ikiwa safari ya siku 48 ya kunadi kampeni hiyo kuanzia Kanda ya Nyasa yenye mikoa ya Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe na Rukwa.
Kwa mujibu wa Golugwa, ziara hiyo itaongozwa na Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu akiambatana na Makamu Mwenyekiti (Bara) John Heche, manaibu makatibu wakuu na wajumbe wa kamati kuu.
Amesema viongozi hao watakuwa na jukumu la kuelimisha umma kuhusu ajenda ya ‘hakuna mabadiliko, hakuna uchaguzi’.
“Hakuna mabadiliko, hakuna uchaguzi’ sasa inapelekwa kwa wananchi kupitia mikutano ya hadhara ya siku 48 itakayofanyika kwenye Kanda 10 za Chadema kuanzia Machi 23 hadi Mei 10, 2025,” amesema Golugwa.
Amesema kwenye ziara hiyo wataelimisha Watanzania kuhusu mabadiliko yanayohitajika kuanzia kwenye Katiba hadi kwenye muundo na utendaji kazi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Golugwa amesema baada ya Kanda ya Nyasa wataelekea Kanda ya Kusini yenye mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi.
“Baada ya mkutano wa Mbeya mjini tutakuwa na timu mbili, ya kwanza itakayongozwa na Lissu, nyingine Heche katika mikoa na majimbo ya Kanda ya Nyasa. Tukimaliza timu zote zitakutana Iringa mjini Machi 29, kuhitimisha ziara ya Kanda ya Nyasa,” amesema Golugwa.
Kwa mujibu wa Gulugwa Aprili 4 hadi 10 watakwenda Kanda ya Kusini kisha Kanda ya Kati (Dodoma, Singida na Morogoro) kuanzia Aprili 12 hadi 13 na kumalizia Kanda ya Magharibi (Tabora, Katavi na Kigoma) kuanzia Aprili 14 hadi 17.
Baada ya mapumziko ya Pasaka, ziara hiyo itaanza upya Kanda ya Victoria (Geita, Mwanza na Kagera) kuanzia Aprili 22 hadi 24. Kanda ya Serengeti (Mara, Shinyanga na Simiyu) Aprili 26 hadi 28; wakati Kanda ya Kaskazini (Tanga Kilimanjaro, Arusha na Manyara) itakuwa Aprili 29 hadi Mei 3.
Golugwa amesema baada ya mapumziko hayo, msafara huo wa viongozi wa Chadema utahamia kisiwani Pemba (Mei 4), Unguja (Mei 5) na kumalizia katika Kanda ya Pwani, (Dar es Salaam na Pwani) kati ya Mei 7 hadi 10.
Golugwa amesema wameamua kuanzia ziara hiyo katika kanda hizo kutokana na mwamko wa wananchi katika maeneo hayo na kuwa ndiyo maana watakaa muda mrefu katika kanda hizo.
“Katika ajenda hii, ni muhimu Serikali ikasikia mabadiliko tunayoyataka kwa kuwa ni sauti ya wengi na si Chadema pekee. Katika kuendeleza ajenda hii Chadema ipo tayari kuungana na vyama na marafiki watakaoamini katika vuguvugu la mabadiliko,” amesema Golugwa.
Golugwa amesema watahakikisha wanaratibu mikutano hiyo kwa hali ya amani kama ambavyo wanafanya siku zote, huku wakiwakaribisha Watanzania wote wakiwemo watumishi wa umma kusikiliza ajenda ya hakuna mabadiliko, hakuna uchaguzi.
Mchambuzi wa siasa, Rainery Songea amesema ni haki ya Chadema kufanya mikutano ya hadhara kwa lengo kuwajengea uelewa wananchi kuhusu ajenda yoyote ikiwemo hii ya hakuna mabadiliko, hakuna uchaguzi.
“Kwa mujibu wa Chadema, ajenda hiyo imetokana na chaguzi zilizofanyika na mapendekezo ya Tume mbalimbali kuanzia ya Jaji Francis Nyalali hadi Jaji Joseph Warioba, hoja kubwa ni mifumo ya uchaguzi ambayo haina usawa, ndio maana chaguzi zinaonekana na kuwa na changamoto.
“Ni hoja ambayo Chadema ilipaswa kuichukua tangu mwaka 2020, ili kushinikiza waliopo madarakani na Bunge kuchukua hatua mapema. Changamoto inayokuja hivi sasa ni muda, hoja yao ni ya msingi lakini changamoto ya muda, je utatosha au walioko madarakani watakubali kuihirisha uchaguzi,”amesema Songea.
Songea amesema hoja kubwa ya Chadema uchaguzi uahirishwe ili mabadiliko ya msingi ya uchaguzi yafanyike, jambo ambalo analiona ni ngumu kufanikiwa kwa mazingira ya sasa.
Mchambuzi mwingine wa siasa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Conrad Masabo amesema Chadema ni chama cha siasa, na kwamba kinachokwenda kufanyika ni kuuza sera zake kwa wananchi ili kuungwa mkono.
“Chama wana sera yao kwa nini wanataka mabadiliko, hivyo kama wananchi watashawishika maana ni ishara kwamba sera yao imeeleweka,” amesema Dk Masabo.
Amesema ajenda ya Chadema ya No Reform No Election ni shughuli ya kisiasa ikiwa haijavunja Katiba. “Chadema ina uhuru wa kufanya shughuli zake za kisiasa bila kuvunja sheria za nchi,” amesema Masabo.
Alichokisema Jaji Mutungi
Jana Jumanne, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika mara baada ya kutoka kwa msajili alisema:“Tumeieleza ofisi ya Msajili kuhusu msimamo huu, baada ya kilichotokea katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji wa mwaka 2024 na historia ya chaguzi kuanzia mwaka 2019 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.”
Mwananchi limemtafuta Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Mutungi leo Jumatano, Machi 19, 2025 amesema ni mapema mno kueleza kilichojiri katika mazungumzo baina ya ofisi yao na Chadema.
Jaji Mutungi amesema hata Chadema kinafanya makosa kuongea na vyombo vya habari, ilhali bado mazungumzo baina ya ofisi hiyo na chama hicho, yanaendelea na hayajafika mwisho.
Hata hivyo, Jaji Mutungi amesema wito wa ofisi hiyo kwa Chadema haukulenga kukikataza chama hicho,kuendelea na ajenda yao, badala yake waliwawaita kusikiliza dhamira ya ajenda hiyo.
“Baada ya kuwasikiliza, na kama tutaona haja ya kuwashauri tutawashauri, lakini hatukuwaita kuwakataza kuhusu ajenda hiyo,” amesema.
Jaji Mutungi amesisitiza mazungumzo bado hayajafika mwisho kama ambavyo Mnyika alidokeza jana katika mazungumzo na wanahabari, kwamba wataitwa wakati mwingine.
Waliondoka Chadema, kurejea tena
Kwenye mkutano huo, Golugwa alidokeza kuwa, katika ziara hiyo, wanachama waliokimbia Chadema kwa nyakati tofauti, kutokana na pilikapilika ikiwemo vipigo na kukosa haki ya uchaguzi watarejea kutokana na ajenda ya mabadiliko.
Licha ya Chadema kushikilia msimamo wa ajenda ya hakuna mabadiliko, hakuna uchaguzi, wamekuwa wakikosolewa hasa na CCM kilichodai kuwa haina maana yoyote kwa sasa, kikisisitiza kuwa muda wa kufanya mabadiliko ya kisheria umekwisha kutokana na Uchaguzi Mkuu kukaribia.
Chama hicho tawala kilikwenda mbali zaidi, kupitia majukwaa mbalimbali ya kisiasa kikisema mabadiliko ya uchaguzi yameshafika kupitia 4R (ustahimilivu, mageuzi, kujenga upya na maridhiano), hivyo no reform no election haina maana kwa sasa.