Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, amezitaka mamlaka za maji nchini kuweka mikakati thabiti ya kupunguza kiwango cha upotevu wa maji ili kuepuka hasara inayopatikana.
Ametoa kauli hiyo wakati ambapo ripoti ya utendaji wa mamlaka za maji nchini ikieleza kiwango cha upotevu wa maji nchini katika mwaka wa fedha 2023/2024 kilikuwa asilimia 36.8, sawa na Sh114.12 bilioni.
Kiwango hicho cha upotevu wa maji ni juu ya kiwango cha huduma kinachokubalika cha asilimia 30.
Dk Biteko ametoa kauli hiyo leo Jumatano, Macji 19, 2025 wakati akizindua ripoti ya 16 ya utendaji wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa mwaka wa fedha 2023/24 uliofanyikajijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyoandaliwa na Mamlaka ya Nishati na Maji (Ewura), kiwango cha maji kilichokuwapo katika kipindi husika ni pungufu ikilinganishwa na asilimia 37.2 katika mwaka wa fedha 2022/23.
Dk Biteko amesema thamani ya fedha inayopotea kwa sababu ya maji kutofika kwa wateja inatosha kujenga mradi mwingine mkubwa wa maji.
“Sababu zinazotajwa si tu miundombinu, lakini pia wizi, yaani mwizi anaturudisha nyuma. Mtaona kuwa tuna kazi ya kufanya,” amesema Dk Biteko.
Ametaja miongoni mwa mamlaka zinazoongoza katika upotevu wa maji ni Rombo kwa asilimia 79, Handeni asilimia 69, Mugango Kiabakari asilimia 68, Ifakara asilimia 56, na Kilindoni asilimia 55.
Waliofanya vizuri ni Maganzo wakiwa na asilimia nne pekee ya upotevu wa maji, Nzega asilimia sita, Kashwasa asilimia 11, Biharamulo asilimia 12, na Monduli asilimia 13.
“Kwa hali tuliyonayo ya upotevu wa asilimia 70, maana yake ni kwamba maji yanayowafikia wananchi ni kidogo sana kwenye hayo maeneo. Mheshimiwa waziri (wa Maji, Jumaa Aweso), hilo ni eneo la kuangalia.
“Huenda kuna sababu za msingi zinazosababisha hali hii, lakini kwa kweli tumesoma ili tufanyeje kama hatuwezi kuondoa tatizo hilo, ni lazima tuliondoe,” amesema Dk Biteko.
Amesema kuwapo kwa upotevu wa maji kwa kiasi kikubwa kunaongeza gharama za uendeshaji: “Kama unawekeza katika maji na mengi yanapotea kwa asilimia 70, maana yake ni kuwa kile unachokusanya na kile unachokiweka hakikutani. Jambo hili litaendelea kuwafanya kulalamika kuwa gharama ni kubwa kuliko hela inayopatikana.”
Amesema changamoto hizo zinahitaji mipango madhubuti na ushirikiano wa wadau wote wa sekta ya maji, kwani Serikali haiwezi kufanya kila kitu na sekta binafsi inahitajika kusaidia kuondoa changamoto hizo.
Pia ametaka mamlaka hizo kuongeza juhudi kwenye uwekezaji wa uzalishaji maji na miundombinu ili kusaidia kuziba pengo la uzalishaji maji, kwa sababu wastani wa uzalishaji dhidi ya mahitaji kwenye taarifa hii ni asilimia 45.
Kwa mujibu wake, licha ya uzalishaji maji kuongezeka hadi kufikia lita milioni 685 mwaka 2023/2024 kutoka lita milioni 593 mwaka uliotangulia, kiwango cha maji kilichozalishwa kilikuwa ni asilimia 45 pekee ya mahitaji ya maji katika maeneo yanayohudumiwa na mamlaka hizo.
Ongezeko la mahitaji ya maji katika maeneo yanayohudumiwa na mamlaka za maji linahusishwa na ongezeko la watu kutokana na ongezeko la maeneo ya huduma ya mamlaka za maji na ongezeko la kawaida la idadi ya watu.
“Ukilinganisha na miaka ya nyuma, uwiano wa uzalishaji dhidi ya mahitaji ya maji uliopo umeongezeka kutoka asilimia 47 katika mwaka wa fedha 2022/23 hadi a asilimia 48 katika mwaka wa fedha 2021/22,” amesema.
Kupungua kidogo kwa uwiano huo kunamaanisha ongezeko la uzalishaji maji halikuendana na kasi ya ongezeko la mahitaji ya maji.
Kuhusu uwiano wa uzalishaji maji dhidi ya uwezo wa mitambo, ulipungua kufikia asilimia 53 katika mwaka wa fedha 2023/24 kutoka asilimia 56 katika mwaka wa fedha 2022/23, ikimaanisha kutotumika ipasavyo kwa miundombinu ya uzalishaji maji iliyopo katika kuboresha upatikanaji wa huduma za maji.
Katika upande wa ukosefu wa huduma bora za usafi wa mazingira na miundombinu ya kutibu maji safi na maji taka, ripoti inaonesha kuwa ni mamlaka 11 ndiyo zina mtandao huo. Dk Biteko amesema suala hili linahitaji kuwekewa mkazo ili miundombinu hiyo iwepo.
“Suala hili ni mtambuka, liendelee kuwa kipaumbele cha sekta ya maji. Wizara imeandaa mwongozo wa usimamizi wa huduma ya maji safi na tope kinyesi. Mwongozo utoe maelekezo ya kitaalamu na hatua zinazolenga kuboresha hali ya usafi wa mazingira na upatikanaji wa maji. Mamlaka zisome na kutekelezwa kwa vitendo,” amesema Dk Biteko.
Katika hafla hiyo, Waziri wa Maji, Aweso amesema pamoja na changamoto zote, kazi kubwa imefanyika na nzuri ambayo imeleta mageuzi kwenye maeneo mbalimbali.
“Tuliomba nafasi kuwa taarifa za utendaji wa mamlaka zisiwe za kawaida. Sio tunawapongeza watendaji waliofanya vizuri pekee na wale wasiofanya vizuri tuwabainishe ili tuchukue hatua, kwa sababu kuwa mkurugenzi si suti bali utendaji, umefanya nini,” amesema Aweso.
Kuhusu upotevu wa maji, amesema walipendekeza kuanza kubainisha kiasi badala ya kutaja asilimia pekee, watumishi waone maumivu ya fedha hizo kupotea.
Hata hivyo, katika kushughulikia upotevu wa maji baadhi ya maeneo, ikiwemo Dar es Salaam, walianza kufanya ushirikishwaji wa wenyeviti wa Serikali za mitaa, jambo lililoweka urahisi kutambua tatizo linapotekea katika maeneo yao.
“Pia tumetumia chuo chetu cha maji, kwani kina teknolojia inayosaidia kuona maeneo yenye changamoto za maji ili wizara na taasisi zake zichukua hatua,” amesema Aweso.
Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Dk James Mwainyekule amesema licha ya kuongezeka kwa ufanisi kwa mamlaka za maji, bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo mamlaka kuwa tegemezi katika masuala ya kifedha kutoka serikalini.
“Ili kutatua tatizo hili, wizara kwa kushirikiana na Ewura tumekuwa tukitoa mafunzo ili kutafuta namna za kuwekeza kupitia njia mbadala kama ilivyo Tanga wanapotumia hatifungani,” amesema.
Changamoto nyingine ni baadhi ya mamlaka kutokuwa na bei zinazoakisi gharama za utoaji huduma, ambapo Ewura imekuwa ikiwashauri kuwasilisha maombi ya kurekebishiwa bei kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.
“Pia uchakavu wa miundombinu unaosababisha upotevu mkubwa wa maji. Tumekuwa na mikakati ya kuimarisha ukarabati ili maji yanayozalishwa yawafikie wananchi inavyotakiwa,” amesema.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Ewura, Profesa Mark Mwandosya amesema sekta ya maji ni anuai inayogusa sekta zote, na kuongeza uwepo wa huduma bora za maji kunapunguza magonjwa yanayoenezwa kwa njia ya maji.
“Pia ripoti ya NBS inaonyesha kuwa kwa sasa zaidi ya asilimia 70 ya taasisi ya elimu zinapata maji. Hii imesaidia kuongeza muda wa wanafunzi kukaa shuleni na kuleta matokeo chanya,” amesema.