Kesi mauaji ya polisi wanne, raia watatu Sitakishari kusikilizwa faragha

Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imetoa amri kuzuia kutajwa majina ya mashahidi katika kesi ya mauaji ya askari wanne na raia watatu, tukio lililohusisha kundi la watu wenye silaha za kivita.

Kwa mujibu wa kiapo cha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Faustine Mafwele, washirika wa washtakiwa bado hawajakamatwa na kwamba, wamemuua mmoja wa mashahidi wa Jamhuri, mgambo MG 472454 Mussa Koti.

Amedai kundi hilo la watu wenye silaha lililovamia Kituo cha Polisi Stakishari kilichopo Ilala, Dar es Salaam, pia liliiba bunduki 11 aina ya Sub Machine Gun (SMG), bunduki tisa aina ya Semi-Automatic Rifles (SAR) na risasi 90.

Uamuzi wa Mahakama Kuu kuzuia kutajwa majina ya mashahidi na kesi kuendeshwa faragha, umetolewa Machi 17, 2025 na Jaji Hussein Mtembwa. Hukumu hiyo imewekwa kwenye mtandao wa Mahakama leo Machi 19, 2025.

Ombi lililotolewa uamuzi huo, liliwasilishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kupitia maombi ya jinai namba 5569 ya mwaka 2025 dhidi ya wajibu maombi 13 ambao ni washtakiwa katika kesi ya mauaji. Maombi hayo yalisikilizwa upande mmoja.

Wajibu maombi ni Omari Makota, Rajabu Mohamed, Ramadhani Hamis, Fadhil Lukwembe, Ally Salum, Khamis Salum, Nassoro Abdala, Seleman Salum, Said Chambeta, Hamis Masamba, Mohamed Ungando, Abdalla Kalupula na Mnemo Mwatumbo.

Maombi hayo yaliwasilishwa mahakamani kupitia kifungu cha 34(3) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi namba 21 ya mwaka 2002, ikisomwa pamoja na vifungu namba 188(1)(a)(b)(c) na (d) na kifungu cha (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

DPP aliomba amri ya kutotajwa majina na anuani au mahali walipo mashahidi kwa sababu za kiusalama wakati wa usikilizwaji wa uhamishaji wa shauri la mauaji kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwenda Mahakama Kuu.

Aliomba hilo lifanyike pia wakati wa usikilizaji wa shauri la msingi la mauaji na mahakama itoe amri ya kutoweka wazi maelezo ya mashahidi na nyaraka yoyote inayoweza kuwatambulisha na mahali walipo.

Katika kiapo cha ACP Mafwele kilichoambatanishwa na maombi hayo, ameeleza Julai 12, 2015 Kituo cha Polisi cha Stakishari kilivamiwa na kundi la watu wenye silaha. Katika uvamizi huo polisi wanne na raia watatu waliuawa.

ACP Mafwele ambaye ni Mkuu wa Upelelezi (ZCO) wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam amesema askari waliofariki dunia ni D.6252 Sajini Adam Ryoba, E.1279 Koplo Peter Sabuni, E.3962 Koplo Gaudin na G.3010 Konstebo Anthony Komu. Wengine wawili ingawa walikuwa na majeraha makubwa walinusurika kifo.

Amewataja raia waliofariki dunia kwa kupigwa risasi katika uvamizi huo kuwa ni Jackline Duma, Erick Swai na Salehe Simkoko.

Katika kiapo hicho, amesema washambuliaji waliiba SMG 11, SAR tisa na risasi 90. Baada ya upelelezi ilibainika waliofanya tukio hilo walikuwa wamejificha katika msikiti wa Ulatule, ulioko Mkuranga.

Amesema upelelezi zaidi ulifanyika ambao watuhumiwa 13 walikamatwa na kwamba, vitendo vyao vilikuwa na dhamira ya kuvuruga Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hali ya kisiasa, kiuchumi na mfumo mzima wa jamii.

ACP Mafwele katika kiapo amedai kuna washirika wa washtakiwa hao ambao bado hawajakamatwa na jitihada za kuwakamata na baadaye kuwafikisha mbele ya mkono wa sheria kujibu tuhuma zao zinaendelea.

Amedai wajibu maombi (washtakiwa) kwa kushirikiana na washirika wao ambao bado hawajakamatwa, wanajaribu kupata utambulisho wa mashahidi wa Jamhuri ili kuwazuia wasitoe ushahidi.

Amedai washirika hao wa washtakiwa ambao bado hawajakamatwa, tayari wamemuua shahidi mmoja wa Jamhuri, MG 472454 Mussa Koti, ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Mamdikongo, Mkuranga baada ya kutoa maelezo Polisi.

Ni kutokana na mazingira hayo, unyeti na ukubwa wa mashtaka yanayowakabili washtakiwa na ukweli kuwa wapo washirika wao ambao hawajakamatwa, DPP anaona kutoa majina ya mashahidi ni kuhatarisha usalama wao na familia zao.

Baada ya kusikiliza hoja za DPP, Jaji amesema kulingana na kiapo cha ACP Mafwele na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Ashura Mzava, washirika wa washtakiwa wanajaribu kupata majina ya mashahidi ili kuwazuia kutoa ushahidi wao.

“Imeelezwa katika viapo hivyo kuwa tayari hao walioko uraiani maeneo mbalimbali ya Tanzania ambao bado hawajakamatwa, wamemuua mmoja wa mashahidi wa Jamhuri mara tu baada ya kutoa maelezo ya ushahidi polisi,” amesema jaji na kuongeza: “Hizi sababu kwangu naziona zina msingi sana.”

Katika uamuzi huo, jaji amesema: “Mawakili na maofisa wa mahakama hawajawahi kuzingatia kutofichuliwa kwa utambulisho wa mashahidi au ushahidi wowote au jambo lingine linaloweza kusababisha utambulisho wa shahidi kama kizuizi cha usikilizwaji wa haki.

“Inachukuliwa kama njia ya kuruhusu shahidi kutoa ushahidi wake kwa uhuru kuhusu kile anachokifahamu bila kutishwa na nguvu kutoka ndani au nje. Ni jukumu la mahakama kuhakikisha inamlinda shahidi, ndugu au marafiki zake.”

Kwa msingi huo, mahakama imeamuru utambulisho wa mashahidi wote wa Jamhuri usitajwe katika hatua za usikilizwaji wa hatua za mwanzo (committal) za kuhamisha kesi kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwenda Mahakama Kuu ya Tanzania.

Pia ameamuru wakati wa usikilizwaji, shauri hilo litasikilizwa faragha na Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS) ipitie kwa makini maelezo yote ya mashahidi na nyaraka na kufuta majina na anuani zao ambazo zitaweza kuwatambulisha.

Mbali na amri hizo, ili kuhakikisha usikilizwaji wa shauri hilo unakuwa wa haki, Jaji ameitaka NPS kuandaa muhtasari wa ushahidi huo bila kutaja utambulisho wao kuwawezesha washtakiwa kujua aina ya ushahidi dhidi yao.

“Katika usikilizwaji wa ‘committal’ na usikilizwaji wa kesi hiyo, hakuna kusambaza au kuchapishwa nyaraka yoyote ya ushahidi ambayo itakuwa na utambulisho wa shahidi, pia taarifa yoyote inayoonyesha anuani zao nayo isichapishwe,” ameamuru jaji.

Related Posts