UONGOZI wa Mashujaa, upo hatua za mwisho za kumtangaza aliyekuwa kocha wa Mbeya City, Salum Mayanga ili kurithi mikoba ya Abdallah Mohamed ‘Baresi’, aliyetimuliwa Februari 26 mwaka huu kutokana na mwenendo mbaya timu hiyo katika Ligi Kuu Bara.
Mayanga anakuwa kocha wa tatu msimu huu kutoka Ligi ya Championship kuhamia Ligi Kuu, baada ya awali Melis Medo kuondoka Mtibwa Sugar na kujiunga na Kagera Sugar, na Amani Josiah kuondoka Geita Gold na kutua Tanzania Prisons.
Medo alijiunga na Kagera Sugar Oktoba 17, 2024 akichukua nafasi ya Mganda Paul Nkata aliyetimuliwa rasmi Oktoba 10, 2024 ambapo raia huyo wa Marekani aliiongoza Mtibwa katika michezo minne ya mwanzoni ya Ligi ya Championship na kushinda yote.
Hata hivyo, baada ya kutambulishwa huko, uongozi wa Kagera Sugar ulitangaza kuachana na Medo Februari 25, 2025, kutokana na mwenendo mbaya tangu ajiunge nayo, akishinda michezo miwili tu, sare mitano na kupoteza saba kati ya 14 aliyoiongoza. Kwa sasa Medo yupo Singida BS.
Katika michezo hiyo, kikosi hicho kilifunga jumla ya mabao 13 na kuruhusu 22, japo kiujumla kilicheza michezo 21, ambapo kilishinda mitatu tu, sare sita na kupoteza 12, huku Medo akikiacha kikishika nafasi ya 15, kwenye msimamo kwa kuwa na pointi 15.
Kwa upande wa Josiah alijiunga na Tanzania Prisons Januari 2, 2025, akichukua nafasi ya Mbwana Makatta aliyetimuliwa pia kutokana na mwenendo mbaya Desemba 28, 2024, baada ya kukiongoza kikosi hicho katika jumla ya michezo 14 tu ya Ligi Kuu.
Hadi anaondoka Geita, Josiah aliiongoza timu hiyo katika michezo 14 ya Ligi ya Championship ambapo alishinda tisa, sare mitatu na kupoteza miwili, akiiacha nafasi ya pili kwa pointi 30, nyuma ya vinara Mtibwa Sugar iliyokuwa na 35 kwa wakati huo.
Makatta alikiongoza kikosi hicho katika jumla ya michezo 14 ya Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2024-2025, ambapo kati ya hiyo alishinda miwili, sare mitano na kupoteza saba, ambapo alikiacha kikiwa nafasi ya 15, kwenye msimamo na pointi zake 11.
Josiah aliyepo katika presha ya kuinasua timu hiyo na janga la kushuka daraja, hadi sasa ameiongoza kwenye michezo saba ya Ligi Kuu Bara ambapo kati yake ameshinda mmoja tu na kutoka pia sare mmoja, huku mingine mitano akichezea vichapo.
Katika michezo hiyo ambayo Josiah ameiongoza Prisons, amefunga mabao matano tu na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 14, ikiwa ni wastani wa kuruhusu mabao mawili kwa kila mchezo, ikiwa nafasi ya 15 kwa pointi 18, baada ya mechi 23.
Mayanga anaondoka Mbeya City akiiacha katika nafasi ya pili katika Ligi ya Championship ikiwa na pointi 49, sawa na ilizonazo Stand United iliyo ya tatu, nyuma ya Mtibwa Sugar inayoongoza kwa pointi 54, baada ya michezo 23.
Kwa msimu wa 2024-25, Baresi aliiongoza Mashujaa katika mechi 22, akishinda tano tu, sare nane na kupoteza tisa, akifunga mabao 17 na kuruhusu 26, akiiacha katika nafasi ya 11 kwa pointi 23.
Wakati uongozi wa Mashujaa ukiwa hatua za mwisho za kumalizana na Mayanga, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mbeya City, Ally Nnunduma alisema hana taarifa zozote juu ya hilo
“Kama ni mazungumzo yanayoendelea kati ya Mashujaa na Mayanga juu ya hilo sawa, ingawa tunachosubiria ni kupewa taarifa rasmi na kuanzia hapo ndipo tutakuwa na wigo mpana wa kuelezea hatua ambazo sisi tumezichukua kama klabu,” alisema Ally.