Mbeya. Wananchi wa Jiji la Mbeya na Mkoa wa Songwe bado wana miezi 19 mingine ya kufunga mkanda na kuendelea kupambana na foleni ya malori, wakisubiri ahadi ya ukamilishwaji wa upanuzi wa barabara ya njia nne kutoka Nsalaga hadi eneo la Ifisi mkoani Mbeya.
Barabara hiyo, inayosababisha msongamano mkubwa wa magari, ilianza kujengwa Machi 2023 na Kampuni ya Kichina ya Henan International Cooperation Group Co. Ltd (CHICO) na ilitakiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi 24 hadi Aprili mwaka huu kwa gharama ya Sh138.78 bilioni.
Hata hivyo, baada ya Serikali kuona kuwa mkandarasi hatoweza kukamilisha ujenzi kwa sababu mbalimbali, ikiwemo upatikanaji wa fedha, imelazimika kumuongezea muda hadi Oktoba 2026. Kuanzia leo Machi 19, 2025, hadi Oktoba 2026 ni sawa na miezi 19.
Hadi Serikali inamuongezea muda mkandarasi huyo kabla ya ule wa kwanza haujafikia ukomo, mradi huo ulifikia asilimia 23.5.
Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mkoa wa Mbeya, Matari Masige, akizungumzia juzi amesema kuwa pamoja na mambo mengine, changamoto ya fedha ni sababu ya mradi huo kusuasua.
Wakati Masige akieleza hayo, tayari wananchi wa Mji wa Tunduma wameshawasilisha ombi lao kwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wasira, wakimtaka aishauri Serikali kutafuta mkandarasi mwingine aanze kujenga upande wa Tunduma ili wakutane katikati na mkandarasi aliyeanzia Uyole.
Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Mjini Tunduma Machi 15, 2025, wakati wa ziara ya Wasira ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya chama hicho, wananchi wamesema wamechoka kusubiri, lakini pia hawaridhishwi na kasi ya utekelezaji wake.
Wananchi hao wamesema kuwa foleni ya malori inayojitokeza katika barabara hiyo huathiri shughuli zao za kiuchumi, kwani kuna wakati wanalazimika kusimama kwa zaidi ya saa matano kusubiri magari yapungue.
Wanachama wa CCM, mkoa wa Mbeya walifanya kikao cha ndani ambacho mgeni rasmi alikuwa Wasira, Masige alitakiwa kwenda kutoa taarifa yake mbele ya kiongozi huyo.
Masige, katika majibu yake, amesema kuwa kwa sasa mradi huo unatekelezwa kwa kasi, ingawa hapo awali ulikuwa unasuasua kutokana na upatikanaji wa fedha.
“Lakini sasa Serikali imetoa fedha na mkandarasi anafanya kazi mchana na usiku. Ingawa mkandarasi ameomba muda hadi ifikapo Oktoba mwakani awe amemaliza,” amesema Masige.
Amesema kuwa baada ya kufanya tathmini, wameona kuwa ili mradi huo uwe wa manufaa zaidi kwa jamii, inapendekezwa uongezwe hadi kufika maeneo ya Uwanja wa Ndege wa Mbeya badala ya Ifisi.
“Tunaomba mwenyekiti uchukue ombi letu ili mradi huu uwe na manufaa zaidi. Ni muhimu ufike hadi maeneo ya Airport ili uwanufaishe zaidi wananchi wa Mbeya na mikoa mingine inayozunguka Kanda ya Kusini,” amesema.
Ameongeza kuwa Mbeya ni lango la uchumi kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na kuwa kujengwa kwa barabara hiyo ya njia nne kutarahisisha shughuli za kiuchumi kwa wakazi.
“Kutaongeza na kukuza uchumi kwa kuwa katika mradi huu tutaweka taa katika kilomita zote 29, zinazotekelezwa na mkandarasi,” amesema Masige.
Kwa upande wake, Wasira amesema kuwa tayari amewasilisha maombi ya wananchi wa Tunduma kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Geodfrey Kasekenya, ya kuomba kupata mkandarasi mwingine wa kuanza kupanua barabara hiyo kuanzia Tunduma.
“Wakianza kujenga kutoka Tunduma kuja Mbeya hata kwa kilomita 15, itasaidia kupunguza msongamano wa magari. Hata kama haitakamilika haraka, lakini changamoto itakuwa imepungua,” amesema.
Katika mkutano wa ndani uliofanyika Machi 17, 2025, jijini Mbeya, Masige amesema kuwa wakala huo unahudumia kilomita 1,403, kati ya hizo, kilomita 169 zimejengwa kwa kiwango cha lami, huku kilomita 934 zikiwa za changarawe.
“Ukiachana na mradi wa upanuzi wa barabara ya njia nne tunayo miradi mingine ikiwemo ya barabara ya Katumba hadi Tukuyu, Makongorosi Rukwa, na barabara ya Rujewa Madibila,” amesema.
Masige amefafanua kuwa barabara ya Katumba hadi Tukuyu inahusisha njia nne kutoka Katumba kwenda Rupaso kwa kilomita 75.4 na kipande kingine cha kilomita saba.
“Mradi huu tayari tumeshasaini mkataba na tumeshalipa fedha za awali (advance payment). Mkandarasi yupo eneo la mradi na thamani yake ni Sh85 bilioni kwa loti zote mbili,” amesema.
Kwa upande wa barabara ya Makongorosi-Rungwa, Masige amesema kuwa mradi huo ulianzishwa mwaka 2012 na unatarajiwa kuunganisha Mkoa wa Mbeya na Kanda ya Ziwa.
“Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya mradi huu. Kwa upande wa Singida, ujenzi umeshaanza kutoka Itigi kuja maeneo ya Mbeya, hivyo tunatarajia upatikanaji wa fedha ili kuanza ujenzi kwa upande wetu,” amesema.
Amesema matarajio yao mradi wa barabara hiyo uanze na ujengwe walau kwa kilomita 50 kuanzia Makongorosi kwenda Rukwa kwa sababu eneo hilo lina watu wengi na uzalishaji ni mkubwa.
“Tuna mradi mwingine wa Ibanga, Kajujumele, Itungi Port na Kiwila Port. Mradi huu, Serikali ilishasaini mkataba na mkandarasi, lakini hakufanya vizuri, na hivyo Serikali ilisitisha mkataba tangu Mei 2024.
“Hata hivyo, kutokana na kuona umuhimu wa mradi huu, tayari Serikali imeshatafuta mkandarasi mwingine na wapo kwenye mazungumzo ili wasaini mkataba,” amesema.
Ameeleza kuwa mradi wa barabara ya Rujewa hadi Madibila umekuwa ukitengewa fedha kidogo kidogo tangu 2012 na kwamba Serikali inapanga kupata fedha kwa pamoja ili kuutekeleza kwa ukamilifu.
“Serikali imekuwa ikitenga fedha kidogo kidogo kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu. Kwa watu wa Madibila, nafikiri wanajua, lakini nia yetu ni kupata fedha kwa pamoja ili tutekeleza kwa pamoja,” amesema.
Amesema licha ya mkandarasi kufikia asilimia 23.5 za ujenzi, changamoto ya utekelezaji wa mradi huo ni kwamba kwanza unapita katikati ya mji, pia kuna mitandao ya maji, umeme, na mtandao wa TTCL.
“Changamoto nyingi zinalazimu kuja na ramani mpya, kwani iliyokuwepo ilibuniwa miaka mingi iliyopita, na wamekuja na vitu vipya katika kuuboresha ili kukidhi kiwango cha barabara ya njia nne,” amesema na kuongeza:
“Moja ya eneo tuliloongeza ni njia ya watembea kwa miguu na kuwepo kwa sehemu ya kupaki magari pembeni ili wanaotaka kupaki wapate nafasi.”