Nukuu 10 za Samia zilizobamba ndani ya miaka minne

Dar es Salaam. Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake, Rais Samia Suluhu Hassan ametoa hotuba kadhaa zilizoacha alama kwenye siasa, uchumi, na maendeleo ya Tanzania.

Kauli zake zimeonyesha mtazamo wake wa uongozi, dhamira ya kusukuma maendeleo, na msimamo wake katika masuala nyeti. Hizi ni baadhi ya nukuu zake 10 muhimu kuanzia mwaka 2021 hadi 2025:

Mwanzoni kabisa mwa utawala wake, katika hotuba ya Machi 22, 2021 katika mazishi ya Hayati Dk John Magufuli mkoani Dodoma, alisema:

“Tunapokwenda kumpumzisha (Hayati John Magufuli), tunaweza kusema bila kigugumizi kuwa tuko tayari kuendeleza kazi yake nzuri kwa nguvu, kasi na ari ileile.”

Hotuba ya Machi 22, 2021 katika hafla ya kitaifa ya kumuaga Hayati Dk John Magufuli mkoani Dodoma, Rais Samia alisema.

“Kwa wale ambao wana mashaka mwanamke huyu ataweza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nataka niwaambie aliyesimama hapa ni Rais. Aliyesimama hapa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye maumbile yake ni mwanamke.”

Hotuba ya Aprili 6, 2021 alipokuwa akiwaapisha viongozi alio wateuwa Ikulu, Dar es Salaam.

“Wewe (Mkurugenzi Mkuu Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania-Tasac, Kaimu Mkeyenge) ni kijana mimi ni mama ukinizingua tutazinguana. Nataka ukafanye kazi pale.”

Hotuba ya Septemba 27, 2021 katika Mkutano Mkuu Maalumu wa viongozi wakuu wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT).

“Msitegemee nitakuiteni fulani na fulani njooni hapa, kwa nini hivi na hivi! Hapana… wote watu wazima mnayajua mazuri na mabaya, mkifanya mnafanya makusudi nitaongea kwa kalamu narudia tena.”

Hotuba ya Februari 15, 2024 katika Mkutano wa Mapitio ya Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19, jijini Dar es Salaam.

“Sasa kama huwezi kazi, acha wengine waifanye! Mimi siwezi kubeba mizigo ya watu wazembe. Nimewapa dhamana ili muwatumikie wananchi, sio kukaa ofisini na kusubiri mshahara. Miradi inachelewa, fedha zipo, lakini utekelezaji hauonekani. Hili haliwezekani! Kama unajiona huwezi, ni bora uondoke mwenyewe kabla sijaondoa.”

Hotuba ya Januari 31, 2023, akizindua Tume ya Kuangalia Jinsi ya Kuimarisha Taasisi za Haki Jinai, Ikulu Chamwino, Dodoma.

“Tumepoteza uadilifu katika mifumo yetu ya haki jinai, na matokeo yake ni wananchi kupoteza imani na taasisi hizi muhimu lazima turekebishe hali hii.”

Hotuba ya Septemba 28, 2024, alipozungumza na Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) mkoani Ruvuma.

“Msimame tu mjibu ndugu zangu mnahofia nini… msimame tu mjibu hakuna cha kuhofia hapa. Mkiambiwa Mwenyekiti wenu Rais wenu muuaji, waambieni kweli ameua nguvu hasi ya upinzani, mkiambiwa Rais wenu muuaji, waambieni kweli ameua giza lililokuwa limegubika Tanzania na sasa katika kiwango cha kimataifa inang’ara. Hayo ndiyo niliyoua Mwenyekiti wenu na rais wenu, sijawahi kuua mtu labda sisimizi nimeua lakini sio mtu.”

Hotuba ya Februari 28, 2025, alipohutubia wananchi wa Muheza katika ziara yake mkoani Tanga.

“Tulisema asilimia 80 ya watu wetu ikifika 2030 wawe na nishati safi ya kupikia na kwa sasa tupo chini ya asilimia 10, lakini kwa kasi tunayoendelea nayo nina hakika kabla ya kufika 2030 tutakuwa tumefikia lengo tulilojiwekea kwenye mkakati wetu… hilo nina hakika.”

Hotuba ya Februari 4, 2022 akiwa Magu kuelekea mkoani Mara, katika maadhimisho ya miaka 45 ya CCM.

“Nimemuelekeza Waziri Mkuu, aunde kamati nyingine iende ikafanye uchunguzi wa mauaji yaliyofanywa na Jeshi la Polisi halafu watuletee taarifa, lakini wakati huo huo, nataka Jeshi lako lijitafakari waone kinachotokea ni misingi ya jeshi la polisi.”

Hotuba ya Aprili 18, 2021 katika kongamano la kitaifa lililoandaliwa na viongozi wa dini jijini Dodoma.

“Inasikitisha sana kuona kwamba watu wanapiga ngoma mitandaoni, lakini ngoma ile inachezwa bungeni na inachezwa kwa kudemka vizuri sana, mnademka vizuri sana… kulinganisha watu na sio kulinganisha ajenda za kitaifa. Ajenda ya kitaifa ni moja, mnalinganisha Magufuli na Samia, hawa watu ni kitu hiki… kimoja.”

Related Posts