Sabilo aitamani tena Ligi Kuu

KIUNGO mshambuliaji wa TMA, Sixtus Sabilo amesema licha ya ugumu anaokumbana nao kucheza Ligi ya Championship anaiona nafasi yake ya kurejea Ligi Kuu Bara baada ya kushuka kiwango kwa muda.

Sabilo amejiunga na TMA mwanzoni mwa msimu huu akitokea Polisi Tanzania ameliambia Mwanaspoti kuwa aliamua kushuka katika Ligi ya Championship kwa lengo la kuinua kiwango chake ambacho ameweka wazi kuwa kiliporomoka.

“Championship ni kugumu kuna ushindani mkubwa niliamua kuja kucheza huku baada ya kuona kiwango changu kiuchezaji kimeporomoka sasa ni suala la muda kurejea Ligi Kuu kuendeleza ushindani,” alisema Sabilo aliyewahi kuzitumikia Mbeya City, Namungo, JKT Tanzania katika Ligi Kuu kabla ya kushuka daraja akiwa na Polisi Tanzania.

“Uamuzi nilioufanya ulikuwa sahihi kwani sasa najiona nimerudi kwenye ubora, unajua kuna muda unapambana na unafika levo ya juu huelewi uelekee wapi zaidi unatakiwa kujilinda usishuke ukishuka ndio unajikuta unapotea, hicho ndio kilichonitokea,” aliongeza.

Alisema ili kulinda kipaji chake licha ya kupata ofa kadhaa kutoka timu za Ligi Kuu, aliamua kuelekea Ligi ya Championship ili kujipanga upya akijitafuta kurudi katika ubora wake uliozoeleka.

“Kulikuwa na ofa kadhaa kutoka timu mbalimbali zinazocheza Ligi Kuu lakini sikutaka kwenda huko kwasababu nilihitaji utulivu kipindi narejesha makali yangu, lakini pia nilitaka timu ambayo nitacheza muda wote kikosi cha kwanza na ndio maana nilichagua TMA.”

Akizungumzia TMA alisema wapo katika nafasi nzuri wao wanakimbiza mwizi kimya kimya wakiwaangalia wanaowakimbiza huku akiweka wazi kuwa waliojuu yao wanaenda kupambana wao kwa wao.

‘’Tupo nafasi ya tano kwa pointi 44. Tunazifukuzia timu nne zilizo juu yetu ambazo zina michezo ya kukutana wao kwa wao huku sisi tukikutana na timu ambazo zipo chini kwenye msimamo, hatuzidharau ila tunaamini kwa mwendo tulionao tukipambana tukashinda na waliojuu mmoja kati yao akadondosha pointi tunapanda ngazi,” alisema Sabilo aliyewahi pia kuitumikia Stand United enzi ikiwa Ligi Kuu kabla ya kushuka daraja.

Related Posts