Serikali yaongezwa muda kujitetea kesi ya kura ya maoni

Tabora: Mahakama Kuu Masjala Ndogo Tabora imesogeza mbele tarehe ya usikilizwaji wa awali wa shauri la kura ya maoni kuhusu upatikanaji wa Katiba mpya.

Shauri hilo la maombi mchanganyiko namba 3965/2025 limefunguliwa na mwanasheria, Alexander Barunguza dhidi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC, zamani Tume ya Taifa ya Uchaguzi – NEC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG). Lilipangwa kusikilizwa leo Jumatano, Machi 19, 2025 na Jaji Dk Zainabu Mango.

Hata hivyo, wadaiwa kupitia jopo la mawakili likiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Mark Mulwambo wameiomba mahakama iwaongezee muda wa kuwasilisha majibu ya utetezi wa maandishi nje ya muda, kujibu madai ya Barunguza, kabla ya usikilizwaji.

Wakili Mulwambo amesema wamechelewa kuwasilisha majibu kwenye mfumo kutokana na changamoto ya mtandao.

“Kwa hiyo tunaomba shauri hili liahirishwe ili tupate muda wa kuwasilisha majibu katika mfumo,” ameiomba mahakama.

Barunguza amepinga maombi na sababu hizo, akidai ameshangazwa na kitendo cha mawakili wa Serikali kuomba kuongezwa muda akisema walikuwa nao wa kutosha kwa kuwa walitakiwa kutekeleza hilo mpaka ifikapo Machi 10, 2025.

Ameiomba mahakama isikubaliane kuongeza muda, akidai kilichofanyika ni uzembe, badala yake iamuru kuendelea na usikilizwaji wa shauri hilo.

Jaji Mango baada ya kusikiliza hoja za pande zote katika uamuzi amekubali ombi la mawakili wa Serikali na kuongeza siku mbili leo na kesho Machi 20, akipanga kuendelea na usikilizwaji Machi 21.

Baada ya uamuzi huo,  Wakili Mulwambo amesema Machi 21 hawatakuwepo kwa kuwa kuna dharura watakuwa Dodoma na Machi 26 na 27 watakuwa Arusha.

Barunguza ameieleza mahakama Machi 25 na 28 hatakuwepo.

Baada ya majadiliano ya pande zote, Jaji Mango amepanga kuendelea na usikilizwaji wa shauri hilo Aprili 10, 2025.

Barunguza katika shauri hilo, pamoja na mambo mengine anaiomba mahakama iamuru wadaiwa wafanye marekebisho ya Sheria ya Kura ya Maoni na iamuru upigaji wa kura ya maoni ufanyike wakati wowote kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Mchakato wa Katiba mpya ulianza mwaka 2011 kwa utungwaji wa sheria za kuratibu na kusimamia utekelezaji wa upatikanaji Katiba mpya.

Hizi ni Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Namba 83/2011 iliyoelekeza kuundwa vyombo vya kuratibu mchakato wa Katiba, yaani Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Mabaraza ya Katiba na Bunge Maalumu la Katiba (BMK) na Sheria ya Kura ya Maoni Namba 11/2013.

Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba iliratibu mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi na kuandaa Rasimu ya Kwanza ya Katiba iliyohaririwa na Mabaraza ya Katiba na kupata Rasimu ya Pili ya Katiba iliyowasilishwa kwenye BMK.

Katika Bunge hilo ambalo licha ya mvutano wa kiitikadi wa wajumbe uliosababisha baadhi ya wajumbe kususia majadiliano na kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), lilijadili na Oktoba 2, 2014 lilipitisha Katiba pendekezwa.

Oktoba 8, 2014, aliyekuwa mwenyekiti wa BMK, Samwel Sitta aliikabidhi Katiba pendekezwa kwa Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete, ambayo ilizinduliwa siku hiyo kwa ajili ya kuendelea na hatua nyingine.

Kwa mujibu wa Sheria ya Kura ya Maoni, kama alivyoirejea Barunguza, ndani ya siku 14 baada ya kupokea Katiba pendekezwa, Rais alipaswa kuchapisha katika Gazeti la Serikali amri kuielekeza NEC kuanzisha mchakato wa kura ya maoni.

Oktoba 17, 2014 Rais wa wakati huo, Kikwete kupitia Tangazo la Serikali (GN) namba 383 la mwaka 2014 alitangaza kampeni za kura ya maoni zingeanza Machi 30 mpaka Aprili 29, 2015, (siku 31) na tarehe ya kupiga kura ya maoni Aprili 30, 2015.

Tarehe hiyohiyo, Oktoba 17, 2014, NEC kupitia GN namba 414A ilichapisha swali la kura ya maoni lililouliza; “Unaikubali Katiba inayopendekezwa?”

Hata hivyo, Aprili 2, 2015 Tume, ilitangaza kuahirisha kura ya maoni ya Katiba pendekezwa kutoka Aprili 30, 2014 hadi itakapotangazwa tena. Mpaka leo haijatangazwa.

Barunguza anayedai alishiriki kikamilifu katika mchakato wa mabadiliko ya Katiba kuanzia ukusanyaji wa maoni mpaka utungwaji wa Katiba pendekezwa, anadai NEC haikutekeleza wajibu wake wa kikatiba kutekeleza masharti ya Sheria ya Kura ya Maoni ndani ya muda ulioelezwa.

Anadai wadaiwa wamezuia utekelezaji wa mchakato huo bila kuueleza umma sababu au kwa sababu zisizo wazi na halali, bila kushauriana na kuhusisha ushiriki wa wananchi, wala bila kujali muda, fedha na rasilimali zilizotumika katika mchakato wote.

Barunguza anadai huo ni ukiukwaji wa Ibara ya 18(d) ya Katiba, inayotoa haki ya kupewa taarifa muda wote kuhusu matukio muhimu ya maisha na shughuli za watu na masuala yenye umuhimu kwa jamii.

Pia, anadai kusitishwa mchakato huo kumemnyima fursa ya kikatiba ya kunufaika na haki zake za kikatiba, kushiriki katika mambo ya nchi na haki yake ya kufahamishwa sababu za kusitishwa kwa zaidi ya miaka tisa sasa.

Anadai amenyimwa haki ya kuwa na nchi ya kidemokrasia inayozingatia utawala wa sheria na mgawanyo wa madaraka, kwa kuwa Katiba ya mwaka 1977 haikutokana na mchakato shirikishi.

Mwanasheria huyo anadai si yeye pekee aliyeathirika na mkwamo huo, bali hata Watanzania walio wengi waliotoa maoni kwa upana yaliyowezesha Katiba pendekezwa kupatikana.

Anaiomba mahakama itamke kuwa NEC sasa INEC ilikuwa na wajibu kikatiba kutekeleza masharti ya Sheria ya Kura ya Maoni ndani ya muda ulioelezwa na kutokutekeleza masharti hayo ilikiuka Katiba Ibara ya 26(1), inayotoa wajibu kila mtu kufuata na kutii Katiba na sheria.

Ameiomba mahakama itamke kuwa wadaiwa kuzuia mchakato wa Katiba kwa zaidi ya miaka tisa ni kinyume cha ibara ya 21(1) na (2) ya Katiba ya nchi, kuhusu haki ya raia wote kushiriki katika masuala ya umma na Mkataba wa Kimataifa kuhusu Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR).

Anaiomba iamuru hadi Aprili 2025 wadaiwa wafanye marekebisho yote muhimu ya Sheria ya Kura ya Maoni kuwezesha upigaji kura ya maoni, muda wowote kabla ya Julai 30, 2025 au kabla ya kuanza kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba au Novemba 2025.

Related Posts