Dar es Salaam. Unaweza kuiita ajali kazini ili ueleweke kwa haraka, baada ya mvuvi Maximo Castro kutoka nchini Peru kupotea baharini kwa takriban siku 95 wakati alipokwenda kuvua samaki.
Cha kushangaza zaidi ni jinsi alivyoishi muda wote huo akila mende, ndege na kunywa damu ya kasa kwa sababu ya kiu.
Kwa mujibu wa The New York Times Castro mwenye umri wa miaka 61, alipotea tangu Desemba 7, 2024 katika Bahari ya Pasifiki akiwa na boti yake.
Katika maisha yake ya upweke anasimulia alitumaini Mungu atamsaidia na siku moja angeiona familia yake.
“Mungu nisaidie nitapata nini hapa, nitaokolewa na nani,” ameeleza alivyozungumza na Mungu akiwa mwenye huzuni.
Ilikuwa Machi 12, 2025 alipoonekana na wafanyakazi wa boti ya kuvua ya Ekuado ikiwa ni mamia ya maili kutoka pwani ya Peru, chanzo cha habari cha Peru RPP News kiliripoti.
Alikuwa baharini tangu Desemba 7, alipoondoka bandari ya Marcona ya Peru, vyombo vya habari vya Peru vimesema.
Castro alikuwa ameenda kuvua mayai ya samaki, akipakia chakula cha kutosha kwa mwezi mmoja lakini mambo yakawa tofauti bada ya kupotea.
Lakini Desemba 20, ikiwa ni karibu wiki mbili baharini, injini ya boti yake iliharibika. Alipunguza akiba yake ya chakula, ikiwa ni pamoja na mchele na biskuti alizokuwa nazo ndani akaanza kukinga maji ya mvua.
Lakini kulikuwa na siku ambapo Castro hakula kabisa na hakukuwa na mvua ya kukinga ingawa bado, aliamini angeokoka. “Nilijiambia, sitakufa, kwa sababu nina watoto wangu na mama.”
Lakini baadaye alikamata kobe huku akisema hakupenda kulazimika kumuua lakini hakuwa na namna.
Binti yake Ines Napa Torres, aliiambia RPP News kwamba wavuvi wa ndani walikuwa wamemtafuta baba yake, bila mafanikio.
Alisema familia pia ilikuwa imezihimiza mamlaka kufanya utafutaji wa angani. Boti yake haikuwa na beacon ya redio, ambayo ingefanya iwe rahisi kuipata, RPP News iliripoti.
Anasema kama familia haikupoteza imani na ilikuwa na tumaini ya kumpata baba yao huyo. Baada ya kuonekana alipelekwa kwa helikopta hadi kwenye chombo cha walinzi wa Pwani wa Peru, ambako alipewa matibabu, kulingana na Jeshi la Wanamaji la Peru.
Bintiye anasema baba yake alikuwa amechomwa na jua na amepungukiwa na maji mwilini. Aliita tukio la kupatikana tena ilikuwa ni kama muujiza kwamba alikuwa ameokoka.
Baada ya kurudi alikaribishwa nyumbani kwa sherehe, ambapo marafiki, jamaa na majirani wenye shangwe walimzawadia keki iliyopambwa na ndege wa mapambo, mende na kasa.