Kibaha. Mbunge wa Kibaha Mjini, Mkoa wa Pwani, Selvestry Koka amekemea vitendo vya uanaharakati ambao umekuwa ukijitokeza kwa baadhi ya viongozi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) mkoani humo, kwamba huchochea uvunjifu wa amani.
Mbunge huyo amewataka viongozi wapya wa chama hicho kujiepusha na vitendo hivyo na badala yake waungane na Serikali kutatua changamoto zinazowakabili wanachama wao.
Koka amesema hayo leo Jumatano Machi 19, 2025 muda mfupi kabla ya kuanza kwa uchaguzi wa viongozi wa CWT wa Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani uliofanyika mjini Kibaha.
Mbunge huyo amesisitiza kuwa viongozi wa chama hicho wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa wanachama wao na kuwa ni vyema wakatumia njia sahihi za kushughulikia changamoto, badala ya kujihusisha na siasa za uanaharakati ambazo zinachochea mivutano.

“Kiongozi wa chama cha walimu anapaswa kuwa na dhamana ya kuleta mabadiliko kwa njia za kisheria na kwa kuzingatia maadili. Siyo vyema kuwa sehemu ya harakati za kisiasa ambazo zinaweza kuzua uhasama baina ya Serikali na taasisi nyingine. Tunahitaji mshikamano ili kujenga taifa lenye amani na maendeleo,” amesema Koka.
Koka ameongeza kuwa ingawa kuna changamoto nyingi zinazokikumba chama hicho, ni muhimu kuzifikisha kwa Serikali kupitia njia zinazozingatia taratibu na kanuni.
Amesema kuwa uvumilivu na ushirikiano kati ya walimu na Serikali ni muhimu kwa mafanikio ya kazi ya uongozi.
“Kwa kuwa kuna changamoto nyingi, inatakiwa kuwasilisha kero za walimu kwa njia sahihi ili ziweze kutatuliwa kwa wakati na kwa kuzingatia taratibu zilizopo. Uvumilivu ni jambo muhimu katika mchakato huu,” amesema.
Katibu wa CWT Mkoa wa Pwani, Susana Shesha ameleza kuridhishwa na hatua zinazochukuliwa na Serikali kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili walimu, kama vile suala la kupanda madaraja.
Amesema kuwa baada ya kliniki ya walimu iliyofanyika hivi karibuni, walimu wameona mabadiliko chanya na wana matumaini kuwa changamoto zilizobaki zitapatiwa ufumbuzi.
“Hivi sasa tunaamini kuwa Serikali inaendelea kutekeleza ahadi zake tuliwasilisha changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na suala la madaraja na tunashukuru kwamba hatua zinachukuliwa ili kutatua matatizo haya,” amesema Shesha.
Katibu wa CWT Wilaya ya Kibaha, Jenny Shoo amesema kuwa chama hicho kitaendelea kufuatilia kwa ukaribu ahadi zinazotolewa na Serikali ili kuhakikisha changamoto mbalimbali zinazowakabili wanachama wao zinapatiwa ufumbuzi.
Amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya chama, walimu na Serikali katika kutatua changamoto za elimu nchini.
“Kazi yetu ni kufuatilia changamoto zinazokikumba chama chetu, na kutumia njia sahihi ili kuhakikisha changamoto hizi zinapatiwa ufumbuzi tunahitaji ushirikiano wa dhati kati ya chama na Serikali ili kufanikisha maendeleo ya nchi yetu,” amesema Shoo.

Mwenyekiti wa CWT Wilaya ya Kibaha, Mwita Magige, ambaye anamaliza muda wake, amesema kuwa ushirikiano wa pande zote mbili, Serikali na chama cha walimu, ni muhimu katika kutatua changamoto za walimu.
Ameongeza kuwa, ili kufanikisha utatuzi wa matatizo ya walimu, ni lazima kuwe na ushirikiano mzuri na utayari wa pande zote kushirikiana kwa pamoja.
“Katika kazi yetu, ushirikiano ni muhimu. Tunasubiri kwa hamu kuona changamoto zote zikiisha kwa sababu maendeleo ya walimu ni maendeleo ya taifa,” amesema Magige.
CWT ilianzishwa mwaka 1992 ikiwa na lengo la kuwaunganisha wanachama wake na kufikisha changamoto zinazowakabili serikalini ili kutafutiwa ufumbuzi kwa ustawi wa nchi.