Vipaumbele vinne vya Profesa Janabi WHO

Dar es Salaam. Mgombea wa Tanzania katika nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Profesa Mohamed Janabi, ameainisha vipaumbele vinne atakavyovitekeleza iwapo atachaguliwa kushika wadhifa huo. 

Profesa Janabi ambaye ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo, amekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha sekta ya afya nchini na duniani.

Amehudumu kwa miongo kadhaa kwenye sekta hiyo, akiwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na baadaye Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Juhudi zake katika kuboresha huduma za matibabu, hususan kwa magonjwa ya moyo na mageuzi ya kitaasisi, zimemjengea heshima ndani na nje ya Bara la Afrika. 

Akizungumza leo Jumatano Machi 19, 2025 kupitia chaneli yake ya WhatsApp, Profesa Janabi ameeleza dhamira yake ya kuimarisha mifumo ya afya, kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za afya kwa wote na kuchochea ubunifu katika sekta hiyo Afrika. 

“Kuanzia kuongoza hospitali kubwa zaidi nchini Tanzania hadi kushiriki katika uundaji wa sera za afya ya umma na lishe, pamoja na ushirikiano wa kikanda, dhamira yangu imekuwa wazi kujenga Afrika yenye afya, inayojitegemea na yenye ustahimilivu. Pamoja, tunaweza kubadilisha taswira ya afya na kuhakikisha kila Mwafrika anapata huduma bora,” amesema. 

Profesa Janabi amesema kampeni yake inajengwa katika msingi wa nguzo nne ambazo ni huduma za afya kwa wote, ustahimilivu, kisasa na umiliki. 

Profesa Janabi ameeleza kipaumbele chake cha kwanza ni kuimarisha huduma za afya ya msingi ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora kwa watu wote, bila kujali hali zao za kiuchumi. 

“Kuwezesha upatikanaji wa huduma za msingi za afya kwa wote ni hatua muhimu kuelekea huduma za afya jumuishi. Huduma bora za afya hazipaswi kuwa anasa, bali haki ya kila mmoja,” amesisitiza. 

Kuhusu ustahimilivu wa mifumo ya afya, Profesa Janabi amesisitiza umuhimu wa maandalizi na mwitikio wa haraka dhidi ya milipuko ya magonjwa, hususan katika zama ambazo mabadiliko ya tabianchi yanaathiri afya kwa kiwango kikubwa. 

“Kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya mabadiliko ya tabianchi na afya. Mafuriko yanaweza kusababisha milipuko ya kipindupindu, huku joto kali likisababisha kiharusi. Tunahitaji mifumo thabiti ya afya inayoweza kukabiliana na changamoto hizi, hasa wakati wa dharura, kama tulivyojifunza wakati wa janga la Uviko-19,” amefafanua. 

Pia, amesema janga la Uviko-19 lilidhihirisha udhaifu uliopo katika mifumo ya afya duniani, hivyo kuna haja ya Afrika kujenga miundombinu thabiti itakayowezesha bara hilo kujitegemea zaidi. 

Profesa Janabi ameeleza dhamira yake ya kutumia teknolojia za kisasa katika utoaji wa huduma za afya, akisisitiza umuhimu wa kutumia suluhisho za kidijitali kupunguza ombwe la huduma katika maeneo ya mbali. 

“Afrika ni kubwa, na jamii nyingi hazina wataalamu wa kutosha wa afya. Kwa kutumia tiba mtandao na mifumo ya afya ya kidijitali, tunaweza kufikisha huduma kwa jamii zilizo pembezoni na zisizo na fursa ya huduma za afya za kawaida,” ameeleza. 

Nguzo ya mwisho katika ajenda yake ni kuhakikisha mataifa ya Afrika yanachukua jukumu muhimu katika kugharimia mifumo yao ya afya. 

“Lazima tujenge mifumo ya ndani ya ufadhili wa afya na kuanzisha mbinu bunifu za upatikanaji wa rasilimali. Njia mojawapo ni kuhakikisha bajeti za kitaifa zinatilia mkazo sekta ya afya, huku pia tukitengeneza mifumo madhubuti ya kusaidia mataifa madogo na visiwa vyenye rasilimali chache. Kwa pamoja, tunaweza kuimarisha mifumo yetu ya afya na kuwa na bara lenye uwezo wa kujitegemea,” amesema. 

Profesa Janabi amewasilisha dira yake Machi 17, 2025 katika mkutano wa pamoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika Harare, Zimbabwe, alikotambulishwa rasmi kama mgombea wa Tanzania kwa nafasi hiyo ya WHO. 

“Kwa pamoja, tunaweza kujenga Afrika yenye afya kwa kuwekeza katika misingi yetu, kuzuia majanga yajayo, kutumia rasilimali za bara letu ipasavyo, na kuhamia kwenye mfumo wa kujitegemea badala ya utegemezi,” amehitimisha. 

Serikali ya Tanzania, kwa kushirikiana na wadau wakuu wa sekta ya afya, imezindua kampeni ya kidiplomasia kwa ajili ya kumpigia debe Profesa Janabi.

Balozi za Tanzania katika nchi mbalimbali za Afrika zimepewa jukumu la kushawishi uungwaji mkono wake, huku kampeni za mitandao ya kijamii zikisambaza maono yake kwa umma. 

Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza rasmi majina ya wagombea wa nafasi hiyo baada ya kifo cha mtaalamu wa afya ya umma wa Tanzania, Dk Faustine Ndugulile, aliyechaguliwa kushika wadhifa huo mwaka 2024 lakini akafariki dunia kabla ya kuanza kazi rasmi. 

Profesa Janabi anakabiliana na ushindani kutoka kwa wagombea wanne ambao ni Dk N’da Michel Yao kutoka Ivory Coast, Dk Dramé Lamine (Guinea), Dk Boureima Sambo (Niger), na Profesa Mijiyawa Moustafa kutoka Togo.

Related Posts