Dar es Salaam. Vyama mbalimbali vya siasa vimesema vinatumia kila mbinu inayowezekana kuhamasisha wanachama wao wajiandikishe katika daftari la kudumu la mpiga kura, huku Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikiwa na msimamo tofauti.
Msimamo wa Chadema, kwa mujibu wa Katibu Mkuu wake, John Mnyika, ni ajenda ya ‘No Reform, No Election’ (hakuna mageuzi, hakuna uchaguzi), inayolenga kuzuia kufanyika uchaguzi iwapo hakutafanyika mageuzi ya kisheria.
Mnyika alitoa kauli hiyo alipoulizwa na Mwananchi jana Jumanne, Machi 18, 2025, dakika chache baada ya kutoka kwenye kikao na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, aliyewaita kujua dhima ya ajenda hiyo.
Mpaka sasa, chama hicho hakijaweka wazi maandalizi yake kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu, zaidi ya kusema mwelekeo wake ni ajenda hiyo.
Mbali na msimamo huo wa Chadema, wadau wengine, wamesema wanaendelea kuhamasisha wanachama na wananchi wajiandikishe katika daftari hilo, ingawa kishindo chao pengine kisilingane na kile cha Chama cha Mapinduzi (CCM).
CCM ilishaanza mapema harakati za uelimishaji wananchi kujiandikisha katika daftari hilo, imekuwa ikizungumzwa na Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wake Bara, Stephen Wasira na hata Katibu Mkuu, Dk Emmanuel Nchimbi na mwenezi, Amos Makalla.
Rais Samia akiwa ziarani mkoani Tanga hivi karibuni, pamoja na mambo mengine aliwahamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.
Leo Jumatano, Machi 19, 2025, ikiwa ni siku ya pili ya uandikishaji jijini Dar es Salaam, Mwananchi imezungumza na wadau mbalimbali akiwemo Katibu Mkuu chama cha UDP, Saumu Rashid, aliyesema chama hicho kinaendelea na uhamasisha wa wapigakura, ingawa kishindo chake hakiwezi kushindana na CCM.
Amesema kwa sababu CCM ina rasilimali za kutosha na mtandao mkubwa wa viongozi, kila mkoa, wilaya, kata na mitaa, ikifanya jambo hata dogo ni rahisi kuonekana kwa ukubwa, tofauti na wao.
“Sisi tunahamasisha kwa uwezo wa rasilimali tulizonazo, mara nyingi tunahamasisha kwa kutoa vipeperushi, kuzungumza na watu mitaa, pia tunakwenda kwenye vyombo vya habari kutoa elimu ya kujiandikisha,” amesema.
Hata hivyo, amesema katika siku za karibuni chama hicho kinatarajia kufanya tukio jijini Dar es Salaam linalolenga kutoa elimu ya kuhamasisha wanachama na wananchi kujiandikisha.
Kwa upande wa chama cha NCCR-Mageuzi, kimesema kinatumia vyombo vya habari kuhamasisha wananchi wakajiandikishe kwa sababu kupita mitaani kuna gharama zake.
Makamu Mwenyekiti wa chama hicho-Bara, Joseph Selasini, amesema uhamasishaji wa watu kujiandikisha unahusisha wadau wengi, ingawa vyama vya siasa ni namba moja.
“Suala la kuhamasisha wapigakura lina wadau wengi, sisi vyama vya siasa ni mdau namba moja, lakini tume ndiyo inayohusika na aina ya bajeti kabisa,” amesema.
Amesisitiza chama hicho hakitaacha kushiriki uchaguzi, ndiyo maana hakijaacha kuhamasisha wananchi wakajiandikishe kwenye daftari la kudumu la wapigakura.
“Kila chama kina mikakati yake, sisi tumesema chama chochote cha siasa, kimesajiliwa kwa ajili ya kuchukua dola na dola sio urais tu, kuanzia mwenyekiti wa kijiji, mtaa, diwani, mbunge na hatimaye Rais,” amesema.
Amesema chama kinasajiliwa kwa ajili ya kupata nafasi hizo, ili wakipata waonyeshe uwezo wao wa kuongoza na kisichotaka kushiriki uchaguzi kinagomea kuchaguliwa.
“Chama kinaonyesha kukubalika kwenye uchaguzi, kama tuna nguvu ya kuzuia uchaguzi, kwanini tusiitumie kuhakikisha watu wetu wanaopigiwa kura wametangazwa?” amehoji.
Amesema chama hicho hakiamini katika fujo kuelekea kupata viongozi wao, kwa sababu kuzuia uchaguzi bila kuweka mbinu hadharani ni tatizo.
Amesema wanawahamasisha Watanzania wenye nia ya kushiriki uchaguzi na kugombea nafasi mbalimbali waende NCCR-Mageuzi kwa sababu watashiriki uchaguzi na watafanya kila namna kulinda kura zao.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa chama cha Ada Tadea, Ali Juma Khatibu, amesema wameshapita mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Geita kuhamasisha wananchi wakajiandikishe.
Amesema hilo linakwenda sambamba na kuwahamasisha wanachama wao wakachukue fomu za kugombea nafasi mbalimbali, hasa wanawake na makundi maalumu.
“Tunaendelea na hamasa ya kuhakikisha wananchi wanakwenda kujiandikisha ili wapige kura, sisi tulishasema tutashiriki uchaguzi na kujiandikisha ndio nyenzo ya ushiriki, kwa hiyo tunawahamasisha,” amesema.
Amesisitiza chama hicho kinatoa fomu bure za kugombea kwa wanawake na makundi mengine maalumu yatakayotaka kugombea nafasi mbalimbali ili kuhamasisha ushiriki wao katika siasa.