Dar es Salaam. Mjadala wa wahitimu wa vyuo vikuu kwenda kupata ujuzi vyuo vya ufundi stadi (Veta) bado haujapoa. Wadau mbalimbali wameuendelea wakichambua kwa mitazamo tofauti.
Msingi wa mjadala huo ni ushauri alioutoa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akionesha umuhimu wa wahitimu wa vyuo vikuu wakiwamo wenye shahada kwenda kujiunga Veta kusoma ujuzi.
Mwanzoni mwa wiki iliyopita, Majaliwa akiwa ziarani Wilaya ya Nzega mkoani Tabora alisema:
“Veta ile si tu kwa kijana wa darasa la saba, hata wewe uliyemaliza digrii, mtaalamu wa kompyuta, nenda kajifunze kushona nguo uwe fundi cherehani, nenda kajifunze ufundi umeme uwe fundi umeme,” alisema Majaliwa na kuongeza:
“Kwa hiyo, mwanafunzi wa chuo kikuu anaweza kwenda kusoma Veta kwa sababu pale anasomea ufundi na ndiyo malengo ya Serikali ya kutoa fursa ya watu kusomea ujuzi na ufundi, ili uwasaidie kujianzishia shughuli za kiufundi ambazo zitakuletea kipato na kuendesha maisha yako.”
Kauli hiyo, iliibua mjadala na wapo walioipokea kwa mtazamo hasi. Jana Jumanne, Machi 18, 2025, jijini Dar es Salaam, alipokuwa anafungua maadhimisho ya miaka 30 tangu kuanzishiwa kwa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta), Majaliwa alisema mjadala huo una tija.
“Mjadala unaoendelea mtaani, Serikali ichukue yale yote bora yatakayoboresha mfumo wetu wa ufundi stadi. Mimi ninaufuatilia, hakika una tija kwa sababu kuna watu wanapinga na wengine wanashauri namna ya kwenda vizuri, kwa hiyo tutumie maadhimisho haya ambayo yamekuja wakati mzuri kukiwa na mjadala huu,” amesema.
Leo Jumatano, Machi 19, 2025, Mwananchi Communications Limited (MCL) limeendeleza mjadala huo kupitia X Space ukiwa na mada inayouliza: Je, ni muhimu wahitimu wa vyuo vikuu kujiunga na vyuo vya ufundi? Ambapo wadau mbalimbali wameshiriki.
Mwandishi wa habari za elimu wa The Citizen, Jacob Mosenda akichokoza mada hiyo amesema wazazi, wanafunzi na jamii kwa ujumla wanapaswa kubadilisha fikra ya kuona mafunzo kutoka Veta ni ya watu wenye elimu ndogo, bali wanapaswa kujifunza ujuzi.
Sambamba na hilo amesema na vyuo vikuu vinapaswa kubadilika ili kuwatengeneza wahitimu wanaohitajika kwenye sekta ya ajira.
Amesema elimu inayotolewa inakinzana na kile kinachohitajika kwenye soko la ajira, akifafanua kuwa kuna changamoto ya ajira na hali ilivyo wanaotoka vyuo vikuu wanakosa ujuzi kitu ambacho kinahitajika zaidi na waajiri.
“Kuna vitu vingi vinahitajika kwenye soko la ajira ambavyo havipatikani vyuo vikuu, hapa ndipo umuhimu wa mafunzo ya Veta unapoonekana,” amesema Mosenda na kuongeza: “tunapaswa kuiga taifa la China ambalo wanasoma kwa vitendo.
Mlay: Jamii ibadili mtazamo
Msomi mwenye shahada ya uzamili ambaye alisema Veta na sasa ni mjasiriamali, Gregory Mlay amesema nchi ya China na Japan wana mitazamo tofauti kuhusu ufundi na hawadharau vitu vidogo kutokana na kiwango cha elimu walionayo, bali wanatumia ujuzi kujisaidia katika shughuli zao.
“Elimu ulionayo haitakusaidia katika kazi unayoifanya bali inakufundisha na kukuweka kwenye nafasi ya kusimamia shughuli za uendeshaji katika kiwanda fulani,” amesema Mlay.
Amesema inawezekana kusoma ufundi na kuanza na kiwanda cha mabegi na kufikia mbali, kwani hata wanaotengeneza magari walianza kwenye ufundi gereji.
Amesema kuna umuhimu wa kuchukulia mtazamo tofauti wa elimu ya ufundi, kwani wapo watoto wanapomaliza kidato cha nne wamekuwa wakiulizwa kama wanaweza kwenda kidato cha tano na sita au apelekwe katika elimu ya ufundi.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Conrad Masabo amesema suala la wahitimu kuambiwa kwenda kusoma Veta ni kama zima moto ya kutatua changamoto ya ajira iliyopo sasa.
“Tujiulize nchi gani duniani imetatua changamoto ya ajira kwa watu kujifunza ufundi? Kila mmoja anaweza kuwa fundi? Je, ufundi ndiyo kimbilio? Duniani hakuna nchi iliyotatua matatizo kwa kufundisha watu ufundi, bado elimu ya nadharia inabaki kuwa na umuhimu wake.”
Dk Masabo amesema changamoto iliyopo hakuna vipaumbele na hatujui nani akasome nini na kwa wakati gani. “Tujiulize watu wote waliopita Veta wamejiajiri?
“Si jambo la kujivunia kwamba mtu unaweza ukakaa chuoni miaka mitatu halafu ukaja kuokolewa kwa kozi ya miezi sita ambayo haikuhitaji wewe kukaa mwaka mzima chuoni,” amesema.
“Siamini kama Veta itakuwa suluhisho bali suluhisho ni kuongeza sekta za uzalishaji. Mfano tujiulize Veta zetu ipi inaandaa wanafunzi kwa ajili ya kilimo? Kwa sababu kilimo ndio kama uti wa mgongo Tanzania.”
“Tusikimbilie kuona Veta itatatua changamoto iliyopo. Kuna mabadiliko ya sayansi na teknolojia ambayo vyuo vyetu vya Veta haviwezi kuhimili bali kinachotakiwa ni kufumuliwa kwa mfumo wa elimu yetu,” amesema Dk Masabo
‘Mjadala wa wahitimu kusoma Veta, ina sura mbili’
Rais mstaafu serikali ya wanafunzi Chuo Kikuu cha Ardhi, Innocent Alex amesema kauli ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuhusu wahitimu wa vyuo vikuu kwenda kusoma Veta ina sura mbili.
Amesema upande wa kwanza hoja hiyo ina mashiko kwa sababu ina lengo la kuwazalisha watu wenye ujuzi wa ufundi kutokana na soko la ajira la sasa, hivyo wahitimu watashindana kwenye soko wenye ujuzi wakiwa na nafasi ukilinganisha na wengine.
Upande wa pili amesema hoja hiyo inatengeneza mazingira kwa wanafunzi waliopo vyuo kwa sasa, waone kwamba wanasoma tu kwa sababu mfumo wa elimu uliopo unawataka wasome bila ya kujua hatima ya ajira.
“Kutokana na mfumo wa elimu wa sasa unaomtaka mwanafunzi asome kisha aje apate ajira inaonesha kuwa haijitoshelezi. Tubadilishe mifumo ili wanafunzi wanapokuwa vyuoni wanasoma wajue wanahitajika kuwa na ujuzi, ingawa nafahamu kwa sasa kuna sera mpya ya elimu ina mafunzo ya amali,” amesema Alex.
Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya (ACT Wazalendo), Abdul Nondo amesema mafunzo ya ufundi stadi (Veta) ni nyenzo nzuri kwa vijana kwa ajili ya kupata maarifa na kujiajiri lakini haitakiwi kusemwa kitu fulani hakifai na kingine kinafaa zaidi.
Hoja ya Nondo inajengwa na kile alichokieleza kwa sasa kuna mjadala unaendelea kuwa kwenda kusoma kidato cha tano na sita hakufai bali kwenda Veta ndiyo bora.
Amesema takwimu za Baraza la Taifa la Elimu ya ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Nactvet) ya mwaka 2022 na mwaka 2023 inaonyesha idadi ya vyuo vya ufundi stadi Tanzania vinavyomilikiwa na Serikali ni 63.
Amesema vyuo vinavyomilikiwa na Serikali kupitia Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) kwa mwaka 2022 vilikuwa 34 na kufikia 2023 vilikuwa 50 huku vyuo binafsi 2022 vilikuwa 273 na mwaka 2023 vilikua 282.
Nondo amesema hadi kufikia Januari 2025 vyuo vya umma vya Veta vilikuwa 91 na binafsi ni 814.
“Msukumo ukoje kwa wanaokwenda katika hivyo vyuo na fursa zipo namna gani na baada ya kumaliza taarifa zao zinabaki wapi kwa maana ya kufuatiliwa na kusaidiwa mitaji, kwani wapo watu wanaohitaji kujiajiri,”amesema Nondo.
Amesema kauli ya Waziri Mkuu: “Ni nzuri sana watu kwenda kupata ujuzi.” Hata hivyo amesema isitumike kama kigezo cha kukwepa wajibu wa kuajiri. Pia, uwepo utaratibu kuwawezesha hata baada ya kuhitimu mafunzo yao Veta.
Naye Shaban Shaban akichangia mjadala huo amesema kauli ya Waziri Mkuu, Majaliwa imechukuliwa tofauti kwani Veta imewekwa kwa ajili ya kumtengeneza mtu na kwenda kujiajiri mwenyewe.
“Kauli ya Waziri ichukuliwe tofauti kuliko ilivyo kwa sasa na kutengenezwa vipande,” amesema Shaban.
Sekta binafsi iangaliwe vyema
Mwanahabari mkongwe, Peter Saramba amesema njia rahisi ya kutatua changamoto ya ajira nchini ni kuwezesha sekta binafsi ili iajiri, kwani ndiyo mwajiri mkuu si tu Tanzania bali duniani kote.
“Kwa bahati mbaya hapa kwetu sekta binafsi zinachukuliwa kama washindani wa Serikali kwani hatuweki mazingira mazuri ya kuwezesha watu wenye mitaji kuwekeza, vikwazo kuanzia kodi, ushuru, taasisi za udhibiti zinazomfanya mtu ashindwe kumudu,’ amesema.
Amesema njia sahihi ya kukabiliana na changamoto ya ajira, Serikali inapaswa kuangalia sekta binafsi kama mdau muhimu wa fursa za ajira kwa vijana kwa kuweka mazingira bora kwa kila mwenye mtaji aweze kuwekeza, na mwenye mtaji aweze kujiajiri.
“Tutoe motisha kwa watu wanaotoa ajira kwa wengine, tusiweke vikwazo kwani tatizo la ajira ni bomu linalosubiri kulipuka,” amesema Saramba.