Unguja. Licha ya Serikali kuweka mazingira mazuri kwa wafanyabiashara ikiwemo kujenga masoko ya kisasa katika maeneo mbalimbali, bado mwitikio wa wafanyabiashara ni mdogo wa kufanya biashara katika masoko hayo.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Machi 19, 2025, Mkuu wa Soko la Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja, Abdalla Silima Makame amesema tangu lilipofunguliwa soko hilo bado mwitikio wa wafanyabiashara ni mdogo na wengine kufanya biashara zao pembezoni mwa soko hilo.
Amesema kuwa ni jambo la kusikitisha kuona Serikali inatumia fedha nyingi kujenga masoko katika maeneo mbalimbali ili kuweka mazingira bora ya wafanyabiashara, lakini wao bado wanaendeleza kufanya biashara katika maeneo yasiyo rasmi.
“Bado muitikio wa wafanyabiashara sokoni hapa ni mdogo licha ya kuwa ni la kisasa na lenye huduma zote za kijamii, na wanaendelea kufanya biashara katika maeneo yasio rasmi,” amesema Silima
Mkuu huyo wa soko amesema, lengo la Serikali kujenga masoko mengi ni kwa sababu ya kufanya biashara pembezoni mwa barabara ambapo siyo maeneo salama katika harakati zao.
Silima, amesema soko hilo lina jumla ya vibaraza 144 na milango kumi ya maduka,” hadi kufikia sasa watu 27 pekee ndio wanaouza biashara zao humu na wengi kuendelea kuuza sehemu hatarishi,” amesema.
Amesema kuwa, zipo hatua mbalimbali zilizochukuliwa ili kuhakikisha wafanyabiashara wanajaa katika soko hilo ikiwemo kuwapunguza wafanyabiashara wa soko la Kinyasini na kuwaleta hapo bila kuathiri soko hilo.
Vilevile, amesema wamefanya hivyo kwa sababu soko la Kinyasini lina wafanyabiashara wengi wanaouza pembezoni mwa barabara, hivyo watatumia fursa hiyo kutatua changamoto hizo.
Naye, Mtendaji wa Baraza la Manispaa Kaskazini A, Salha Rashid Sleyum amesema wamezungumza na wafanyabiashara walio pembezoni mwa barabara kuingia katika soko hilo, lakini bado wamekuwa wazito kutokana na sababu zisizo kuwa za msingi.
Amesema, licha ya wafanyabiasha hao kujaza fomu za kumiliki vizimba na milango ya maduka katika soko hilo, bado hawajaanza kupanga bidhaa zozote bila kutoa sababu maalumu.
“Baraza la Manispaa limetoa muda kwa wafanyabiashara hao kuanza kazi katika soko hilo na endapo utafika muda waliokubaliana bila kufanya shughuli yoyote maeneo hayo, watapewa wafanyabiashara wengine waliokuwa tayari,” amesema Salha.
Baadhi ya wafanyabiashara walioanza kuwekeza katika soko hilo, akiwemo Ismail Hashim amesema hali ya biashara bado haijachangamka katika soko hilo, kwani watu wengi wamezoea Soko la Kinyasini ambalo lipo karibu na soko hilo.
Ametoa wito kwa wafanyabiashara wenzao kuungana nao kwani uwepo wa wafanyabiashara wengi wa bidhaa tofauti kutachangamsha sokoni hapo na kuvutia wateja.