Dar es Salaam. Takriban wakazi zaidi ya 4,000 wa Kijiji cha Kwedizinga na maeneo ya jirani ya wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga wanatarajia kunufaika na mradi wa maji safi ikiwa ni baada ya kuteseka kwa muda mrefu bila ya kupata huduma hiyo.
Hivi sasa, wakazi hao wanategemea mabwawa na mito ya msimu, hali inayosababisha ongezeko la magonjwa ya mlipuko pia wanawake husafiri zaidi ya kilomita mbili kila siku kutafuta maji.
Mradi huo unaotekelezwa na Benki ya Absa Tanzania na Shirika la World Vision Tanzania kuboresha upatikanaji wa maji kwenye Kijiji hicho chenye vijiji vidogo saba na idadi ya watu takriban 4,000.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini leo Jumatano, Machi 19, 2025, Obedi Laiser, Mkurugenzi Mtendaji wa Absa Bank Tanzania, amesisitiza dhamira ya benki ya kuwa chachu ya maendeleo chanya katika jamii wanazofanya kazi.
Benki hiyo imetoa Sh50 milioni kuwezesha mradi huu, ikionyesha dhamira ya kuiwezesha jamii kunufaika na uwepo wa benki hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Obedi Laiser (wa tatu kushoto) akibadilishana hati ya makubaliano ya ushirikiano na Mkurugenzi wa Miradi wa Shirika la World Vision Tanzania, Nesserian Mollel, jijini Dar es Salaam.
Mradi unatarajiwa kunufaisha moja kwa moja wakazi wote 3,890 wa kijiji cha Kwedizinga na kuwanufaisha kwa namna tofauti watu wengine 596 kutoka vijiji jirani, hatua muhimu kuelekea kuboresha afya na elimu katika eneo hilo.
“Katika Absa, tunaamini kwamba kila stori ina umuhimu. Ushirikiano huu ni ushahidi wa lengo letu la kuiwezesha Afrika ya kesho pamoja, hatua moja baada ya nyingine,” amesema Laiser.
Mkurugenzi wa uendeshaji World Vision Tanzania, Nesserian Mollel amesema wamejitolea kufanya kazi na jamii kuleta maendeleo kwa dhamira ya kukuza mabadiliko ya kibinadamu.
Pamoja, tunahakikisha watoto na familia katika kijiji cha Kwedizinga wanapata moja ya mahitaji ya msingi ya maisha, ambayo ni maji safi.
Mradi huo unalenga kushughulikia changamoto hiyo kupitia uchunguzi wa kihidrolojia na uchimbaji wa visima, kufanya uchunguzi wa kina wa maji chini ya ardhi ili kubaini eneo linalofaa zaidi kwa ajili ya kisima chenye mavuno mengi, ikifuatiwa na uchimbaji hadi kina cha mita 180.
Aidha mfumo wa kusukuma maji kwa nguvu za jua, kufunga mfumo rafiki wa mazingira ili kusafirisha maji kutoka kisimani hadi kwenye tanki la kuhifadhia.
Amesema uhifadhi na usambazaji wa maji kwa kujenga tanki la kuhifadhi maji lenye ujazo wa lita 50,000 na kuanzisha mtandao wa usambazaji maji wenye vituo vingi vya ukusanyaji, kuhakikisha kwamba vijiji vidogo vyote saba vinapata maji safi ndani ya mita 400, sambamba na viwango vya sera ya maji ya Tanzania.

Mpango huu unalingana na Malengo kadhaa ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa, ikiwemo SDG 3 (Afya bora na ustawi), SDG 4 (Elimu Bora), na SDG 6 (Maji Safi na Usafi wa Mazingira).
Pia unaunga mkono awamu ya tatu ya Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Maji ya Tanzania (2022/2025), ambao unalenga kuwaunganisha mamilioni ya watu na vyanzo vipya na vilivyoboreshwa vya maji.