AKILI ZA KIJIWENI: Mnguto kaongea uhalisia wala tusishangae

WANAOSHANGAA kauli ya Mzee wangu Steven Mnguto kwamba uendeshaji wa mpira wa miguu pia unahitaji busara na hekima ndio hapa kijiweni tunapaswa kuwashangaa maana sidhani kama kuna ambacho hawakijui.

Simba na Yanga zimebebwa sana katika suala zima la uamuzi wa vyombo vyetu vinavyosimamia soka hata pale ambapo kanuni zilikuwa zinazibana timu hizo mbili, sasa leo sidhani kama kuna kitu cha kushangaza kuona Mzee Mnguto akisema hivyo.

Tatizo la hizo timu mbili ni moja ambalo ni kila upande kutazama zaidi maslahi yake ambapo ikitokea umenufaika utaimba mapambio kwa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), lakini mambo yakiwa tofauti subiria povu lake.

Mfano kanuni zinatanabaisha wazi kuwa ratiba ya ligi haiwezi kuathiriwa na ushiriki wa timu katika mashindano ya kimataifa lakini ni mara ngapi tunaona TFF na TPLB wakizifanyia uungwana Simba na Yanga kwa kusogeza mbele mechi zao kisa tu kuzipa nafasi ya kujiandaa na mechi za kimataifa.

Mara kibao hizo timu mbili zimekuwa zikitazamwa tu zinavyoacha wachezaji kihuni na kinyume cha sheria na taratibu za usajili pasipo kufungiwa na TFF hadi kusababisha zinapelekwa FIFA na wachezaji au makocha wanaozidai ndipo tunaona hatua zinachukuliwa kwa hapa nyumbani.

Maana yake kama makocha au wachezaji ambao wanakuwa wanazidai wasingekuwa wanakimbilia FIFA kufuata haki zaidi, mambo yangekuwa yanamalizwa kimyakimya hapa nyumbani, lakini upendeleo kama huu watu hawauoni na kuusema wanakuja kuhangaika na kauli ya mzee wangu Mnguto.

Kwani wao wenyewe Simba na Yanga wamekuwa wakitamba kuwa timu zao zimeshikilia soka la nchi na ndio zinapendwa na serikali kulinganisha na nyingine sasa kama ni hivyo hakutakuwa na kosa kama mtu atasema kuwa uamuzi wowote kuzihusu unatakiwa uzingatie hekima na busara.

Na mbaya zaidi watu wameamua kuchagua vichache kati ya alivyovisema Mzee Mnguto pengine ili kupata kile ambacho kitawanufaisha wao na kukwepa kile ambacho hakiwafurahishi au kuwa na faida kwa upande wao.

Mzee Mnguto hakusema kuwa kanuni zisitumike na badala yake busara na hekima ndio zitumike bali alionyesha msisitizo kwamba penye jambo la kimpira pamoja na uwepo wa kanuni na taratibu, busara na hekima inapaswa kutumika katika kuzitumia hizo busara na kanuni.

Related Posts